Hull City kutua nchini

KIKOSI cha Hull City kilichoihangaisha Manchester United wikendi kwenye mechi ya EPL na kulazwa  1-0 dakika za mwisho wa mchezo, kinaratibiwa kuchuana na Harambee Stars hapo baadaye katikati ya mwaka ujao.
Mpango huu unatokana na ufadhili wao  kutoka kwa kampuni kubwa ya kubeti ya humu nchini Sportpesa ambayo inadhamini jezi zao kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kima cha Pauni 10 milioni (Sh1.3 bilioni)
Shirikisho la Soka nchini FKF ambao wana uhusiano mzuri na Sportpesa wanaowapa udhamini wa Sh70 milioni, wamesema kwamba walifanya kikao na Meneja wa Mauzo wa klabu ya Hull City, Simon Keing pamoja na Mkurugenzi wa kampuni ya Samson Sport Consultancy kuhusu uwezekano wa kufanikisha mpango huo.
“Majadiliano tuliyokuwa nayo ni kuona jinsi tunavyoweza kuwaleta Hull City hapa wachuane na kikosi maalum cha Harambee Stars na vile vile waweze kutoa sarasa la soka kwa wasimamizi wa soka la hapa nchini,” Taarifa kutoka kwa FKF ilieleza bila ya kufafanua mengi.
Hata hivyo tumeweza kubaini kuwa mpango wa kuleta kikosi cha kwanza cha Hull City umepangiwa kufanyika mwishoni mwa msimu huu wa EPL,  ukipangiwa kati ya Mei na Agosti 2017 kwenye maandalizi ya kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa 2017/18
Kikosi hicho kitachuana na kile cha Harambee Stars kitakachowashirikisha mastaa watupo wakiwemo Victor Wanyama, Arnold Origi, Macdonald Mariga, Ayub Timbe, Jesse Were na Miachel Olunga katika uwanja wa Kasarani.