Gor Mahia yahaha kumbakiza straika Tuyisenge

Wednesday October 11 2017

 

By Na THOMAS MATIKO

Huku duru zikiarifu kuwa klabu ya Killimarnock ya Scotland imeanza kumfukuzia kocha Dylan Kerr, Gor Mahia wamezidishiwa maumivu na taarifa za kuwepo kwa ofa kwa staa wao ghali, Jaques Tuyisenge.
Straika huyo wa Rwanda alisajiliwa kwa kitita kizito cha Sh4 milioni na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali katika historia ya soka la Kenya. Tangu ajiunge na Gor, kiwango chake kimekuwa cha kuridhisha japo sio sana. Hata hivyo, mchango wake umekuwa mkubwa kutokana na uwezo wake wa kutengeneza asisti na pia kupasia nyavuni.
Taarifa zilizoibuka ni kwamba klabu ya nyumbani kwao miamba APR wanataka kumrejesha. Tayari duru zinaarifu kuwa APR ishamtuma skauti wake kuja Nairobi kuchonga na staa huyo kuhusu uwezekano wa kujiunga nao pamoja na kuwasilishia mapendekezo ya dili wanayokusudia kumpa kama akikubaliana na ombi lao.
Inaaminika kuwa Tuyisenge aliyewafumia Gor magoli tisa msimu huu, amekuwa akishiriki mazungumzo na skauti huyo kisirisiri pasi nyuma ya mgongo wa viongozi wa Gor kwa lengo la kurejea kwao Rwanda na kujiunga na APR Janauri mwaka ujao mkataba wake utakapokuwa umemalizika.
Hata hivyo, Gor tayari washashtukia kinachoendelea na wanasemekana wameanza kumshawishi Tuyisenge ili abaki kwa kurefusha mkataba wake.