Ligi Kuu Kenya kuwaka nyasi

Muktasari:

Kogalo iliwanyuka Nakumatt 4-0 kwenye mtanange wa ufunguzi wa ligi msimu huu mjini Machakos na sasa inataka kusaka alama nyingine tatu katika uwanja huo wenye kumbukumbu tele kwao.

BAADA ya kusajili ushindi muhimu wa mabao 2-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi iliyopita, mabingwa wa soka nchini Gor Mahia sasa wanarejea kwenye Ligi Kuu Kenya alasiri ya kesho Alhamisi dhidi ya Zoo Kericho uwanjani Kericho.
Kogalo iliwanyuka Nakumatt 4-0 kwenye mtanange wa ufunguzi wa ligi msimu huu mjini Machakos na sasa inataka kusaka alama nyingine tatu katika uwanja huo wenye kumbukumbu tele kwao.
Ni hapo hapo Kericho walishinda mechi tatu msimu uliopita mojawapo ikiwa ni ile dhidi ya Ulinzi Stars iliyowahikikisha ubingwa kukiwa kumesalia mechi nne.
“Ni mechi nyingine tunatafuta ushindi maana mbio ndio zimeanza na alama tatu  ni muhimu ili kutetea taji letu,” alisema nahodha, Harun Shakava.
Hayo yakijiri, Kogalo imetengeneza Ksh363,100 yakiwa ni malipo ya viingilio vya milangoni katika mechi yao ya Ligi ya Mabingwa huku mahasidi wao AFC Leopards wakipata Ksh1,041, 830 kwenye sare yao 1-1 na Fosa Juniors katika mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika iliyopigwa Kaunti ya Kakamega.
Kwinginenko, droo ya Nane Bora imesongeshwa mbele. Bodi ya KPL ilitarajiwa kufanya droo hiyo juzi Jumanne, lakini ikabadilisha hadi watakapozindua mfadhili wa kombe hilo linalorejea baada ya kukosekana mwaka jana.
Gor, Sofapaka, Kariobangi Sharks, Posta Rangers, Kakamega Homeboyz, Tusker, Ulinzi Stars na Ingwe ndio watakaoshiriki kwa kumaliza ndani ya Nane Bora katika msimu uliopita wa KPL.