FKF yasaka kunusuru soka la Kenya

Tuesday January 23 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Baada ya wadhamini wakuu wa soka la Kenya kujitoa katika kudhamini mchezo huo, Serikali kupitia wizara ya michezo imeamua kuingilia kati kuokoa jahazi.
Katika mpango huo serikali inatarajia kuziba pengo la mabilioni ya pesa katika nyanja zote kuanzia kwenye haki za matangazo, klabu, ligi kuu na shirikisho lenyewe.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (FKF), Nick Mwendwa, katika kuhakikisha wanaziba mapengo yaliyoachwa na Sportpesa waliotangaza kusitisha udhamini wao, FKF ilikutana na serikali kuona namna tatizo hilo linatatuliwa.
"Kumekuwa na jitihada za kuhakikisha mambo yanakuwa sawa, tumekutana na wizara, tumewaandikia na wameonesha nia ya kutusaidia kuziba pengo lililoachwa na Sportpesa," alisema rais huyo.
Mwendwa alisema mbali na jitihada zinazofanyika kuishawishi serikali iingilie kati, pia wameanza mazungumzo na Sportpesa kuona kama kuna uwezekano wa kuwashawishi kufikiria upya uamuzi wao wa kuondoa udhamini nakuona kama wanaweza wakarudi.
"Hatujalala, tunajua itakuwa kazi ngumu lakini tunazungumza na wadhamini wetu Sportpesa tuone kama tutaweza kuwashawishi watafakari upya kuhusu uamuzi kwa mustakabali wa soka letu," alisema.
Mwendwa amesema tangu wadhamini wao wajitoe, shirikisho imekuwa ikijiandesha kwa kujikokota jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa soka nchini.
Alisema Serikali imekuwa ikiidhamini timu ya taifa Harambee Stars, katika michezo ya kimataifa pekee huku maswala mengine ya uendeshaji wa kawaida tu yakisalia kuwa ni mzigo wa FKF.
Aidha, Rais Mwendwa alisema kwa sasa wanajaribu kufanya juhudi za kupata mrushaji wa matangazo yote ya mpira ukizingatia kuwa Supersport walijitoa mapema mwaka Jana.
Zikiwa zimesalia takribani majuma mawili tu ligi ianze (February 02), Mwendwa alivitaka vilabu shiriki kujiandaa vilivyo huku akiwahakikishia kuwa kila ligi itaendelea kama ilivyo katika ratiba.
Kesi ya Muhoroni Youth
Kuhusu suala la kesi ya Muhoroni Youth, Mwendwa aliipongeza mahakama kwa kulitendea haki soka la Kenya kwa kutupia mbali kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, mwenyekiti wa Muhoroni Youth, Moses Adagala alienda mahakamani akiishitaki FKF na bodi ya ligi kuu ya Kenya (KPL), akipinga kushushwa daraja kwa kile walichodai ni njama za kuhujumu klabu yake.
Katika baadhi ya madai waliyowasilisha kama utetezi wake, Adagala alisema klabu yake ilishuka daraja kutokana na wachezaji wake kukosa morali katika michezo sita za mwisho kutokana na hujuma za Shirikisho na KPL, huku kidole la lawama akilielekeza kwa Rais wa FKF.
Mwendwa alisema kwa sasa suala hilo limemalizika na kinachofuata ni kila mtu afanye kazi ya kukuza soka na siyo majungu.
"Kwanza nianze kwa kuipongeza Mahakama, uamuzi wao ni wa busara na kwa mara ya kwanza naona wadau wa soka wameanza kutuelewa, tunataka kuondoa uongouongo na ujanja unaofanyika kwenye soka," alisema Mwendwa.