Dawo awachana mabosi Kogalo

Peter Dawo

Muktasari:

Amesema wakufunzi wazawa wana uwezo mkubwa wa kuendesha timu na kufanya vizuri badala ya kuabudu wazungu ambao wengi wameonekana kudidimiza timu badala ya kukua kiwango.

STAA wa zamani wa Kogalo, Peter Dawo, amewachana mabosi wa klabu hiyo akiwataka kuacha kuabudu wakufunzi kutoka nje na kuwafanya wazawa kuwa chaguo la pili.

Amesema wakufunzi wazawa wana uwezo mkubwa wa kuendesha timu na kufanya vizuri badala ya kuabudu wazungu ambao wengi wameonekana kudidimiza timu badala ya kukua kiwango.

Kauli ya Dawo inajiri wakati Kocha Mkuu wa Gor Mahia Jose ‘ Ze Maria’ Ferreira, akizidiwa kupigwa cheche na mashabiki kutokana na kikosi cha Kogalo kupoteza dira wakati ligi ikiwa kwenye hatua za lala salama.

Kati ya mechi saba ambayo Gor Mahia imeshiriki katika mzunguko wa pii, ni miwili pekee ndio imeandikisha ushindi huku mastraika wake wakipoteza uwezo wa kufumania nyavu.

“Hali ya Kogalo kwa sasa ni mbaya, nilidhani msimu huu mambo yangekuwa ni mteremko kwa kuwa na wachezaji hodari lakini imekuwa tofauti. Ni ngumu kusema tutahifadhi ubingwa mbele ya Tusker.

“Tatizo lipo idara ya ufundi na sio wachezaji kwa sababu waliosajiliwa msimu huu ni hodari sana uwanjani,” alisema Dawo aliyeshinda taji la Afrika la Mandela Cup mwaka wa 1987 akiwa na Kogalo.

Alisema baada ya kung’atuliwa kwa mkufunzi mzawa Zedekiah ‘ Zico’ Otieno mwaka 2012, mabosi wa Kogalo walianza kasumba ya kusajili makocha kutoka Ulaya, jambo ambalo limekuwa likiigharimu timu.

Baada ya kuondoka kwa Zico, Kogalo ilimpa mkataba kocha Logarusic kisha Bob Williamson baadaye Frank Nuttal na sasa Ze Maria, ambaye mbali na kuwa na kikosi hodari wangali wanapata matokeo ya kushangaza.

“Imefika wakati wa kuwathamini wakufunzi wetu kuliko wa kigeni ila ninachofahamu ni kwamba, mashabiki wa humu nchini hutaka matokeo mazuri kwa muda mfupi,” akasema Dawo.

Dawo alimtaja mkufunzi wa zamani wa timu hiyo James ‘Abawa’ Siang’a kama mmoja kati ya wakufunzi wazawa wenye ujuzi mkubwa aliyewahi kuifanyia timu hiyo mabadiliko makubwa na yalidumu kwa muda mrefu.