Bandari kusafisha kikosi chao

Wednesday October 25 2017

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF

MOMBASA. Bandari FC imeanza kutema cheche kwa wanasoka wanaotarajia kuwatema wakikamilisha mechi za msimu huu wa 2017.
Ofisa mmoja wa Bandari FC ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema wameanza kuangazia wanasoka watakaowaondoa kwenye kikosi cha msimu ujao wa 2018 na kuwataja wanne wao tayari wamepewa barua za notisi ya miezi miwili, kama sheria inavyotaka.
Wanasoka waliotajwa na ofisa huyo ni beki Noah Abich na mastraika watatu, Jacob Keli, Enock Agwanda na Tyron Owino. Lakini hakuweza kutoa sababu iliyowafanya kuwatema wanasoka hao wanne.
Meneja wa timu hiyo, Alfred Achayo Obwaka alisema wataendelea kuwakosa wanasoka wao wawili, Mwinyi Hamisi na Duncan Otewa ambao wanaendelea kupata matibabu ya majeraha ya goti.
Meneja huyo aliwataka mashabiki wa Pwani wawe na matumaini ya timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zao zilizobakia. “Nawaomba wafuasi wetu wasivunjike nguvu bali wafike kwa wingi  kiwanjani kuwashangilia vijana wetu wapate ushindi dhidi ya Ulinzi,” akasema Obwaka.