Bandari FC kuifanyia Gor Mahia kitu mbaya

Muktasari:

Akizungumza kuhusiana na mechi hiyo ya Ligi Kuu Kenya ambayo itachezwa Uwanja wa Kenyatta, Odhiambo anaamini timu yake imejiandaa vizuri na hana wasiwasi wa ushindi dhidi ya mabingwa hao wa soka nchini.

MOMBASA. WAKATI kikosi cha Bandari FC kikiondoka kesho Alhamisi kuelekea mjini Machakos kuifuata Gor Mahia kwa ajili ya mechi ya keshokutwa Jumamosi, kocha wa vijana hao wa Pwani, Ken Odhiambo, amesema wamejizatiti vya kutosha ili kuangusha mbuyu.

Akizungumza kuhusiana na mechi hiyo ya Ligi Kuu Kenya ambayo itachezwa Uwanja wa Kenyatta, Odhiambo anaamini timu yake imejiandaa vizuri na hana wasiwasi wa ushindi dhidi ya mabingwa hao wa soka nchini.

“Tumeshaiva vizuri sasa, tunaweza kucheza soka la hali ya juu. Ninajua mechi hii itakuwa kali kwani tutacheza dhidi ya mabingwa w nchi,” alisema.

“Gor wanacheza soka la pasi, hawana piga-piga kuondoa lawama. Tumewasoma na tumejipanga kuumiliki mpira mbele yao. Niwaombe tu mashabiki wafike kwa wingi kujionea kandanda ikitandazwa.”

Naye kocha wa makipa wa timu hiyo, Razak Siwa, ambaye ana ingizo jipya baada ya wao kumnasa Mnyarwanda, Bashunga Abouba, kutoka Rayon Sports, alisema makipa wake wote watatu wako sawa na anaamini yeyote atakayepangwa atadaka vizuri.

“Ninaloweza kukwambia ni kuwa makipa wote wako tayari na yeyote anaweza kuwa langoni, lakini siwezi kukwambia ni lini Abouba ataanza kudaka, utajionea mwenyewe wakati wake ukifika,” alisema Siwa.

Bandari ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane ilizokusanya katika mechi nne hali Gor Mahia ni ya pili kwa alama tisa baada ya kucheza mechi tatu. Mathare United iliyocheza mechi nne ndiyo ipo kileleni ikiwa na alama 10.