Bandari, Tusker FC patashika nzito GOTV

Saturday July 1 2017

 

By ABDULRAHMAN SHERIFF, MOMBASA

KUTAKUWA na ‘Patashika nguo kuchanika’ katika Uwanja wa Kinoru mjini Meru kesho Jumapili wakati mafahali wa Tusker FC ambao ni mabingwa watetezi wa GOTV Shield watakapopambana na Bandari FC kwenye mechi ya Ligi Kuu ya SportPesa.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ya kuvutia hasa kutokana na timu hizo kupata ushindi kwenye mechi zao za GOTV Shield mwishoni mwa wiki iliyopita.

Tusker iliitandika SS Assad FC ya Ukunda mabao 5-0 Uwanja wa Mbaraki Sports Club na Bandari kuilaza Uweza 3-1 uwanjani Machakos.

Kocha wa Tusker FC, George Nsimbe aliliambia Mwanaspoti baada ya mechi ya GOTV Shield timu yake ilipoitandika SS Assad FC mabao 5-0 kuwa wanaitambua Bandari kuwa timu kali lakini ana matumaini makubwa ya timu yake kupata ushindi.

“Tunafahamu tunakutana na Bandari katika mechi ya Ligi Kuu na tunaitambua timu hiyo kuwa na wachezaji wazuri na kocha mzuri lakini na sisi tumejiandaa vya kutosha na tunatarajia kupata ushindi,’ alisema Nsimbe.

Bandari iliondoka Mombasa Alhamisi kuelekea Nairobi huku wachezaji wake wakiwa na morali wa kupata ushindi dhidi ya Tusker hapo kesho.

Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo hawakutaka kutajwa majina walisema wanakwenda Meru kupata pointi zote tatu.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu wa Ligi Kuu na Tusker na wiki itakayofuata dhidi ya Gor Mahia katika pambano la GOTV.

“Tunakwenda huko kwa mechi hizo za ugenini tukiwa tuko tayari kushinda,” alisema mwanasoka mmoja wa timu hiyo ya Pwani.

Kumekuwa na tatizo la kuwapata maofisa wa timu ya Bandari kuzungumzia juu ya ziara ya mechi zao hizo mbili. Ofisa wa klabu hiyo alithibitisha kuwa timu iliyondoka Alhamisi lakini maofisa wa benchi la ufundi la timu hiyo hawakupokea simu kwa siku nzima ya Alhamisi.