Ingwe, Sharks acha ngoma itambae

Muktasari:

Lakini subiri, patachimbika nguo kuchanika uwanjani Kasarani wakati AFC Leopards ikipepetana na Kariobangi Sharks kwenye fainali ya Ngao ya GOtv.

Kenya. Mnavyofahamu, keshokutwa Ijumaa ni siku ya Mashujaa na Wakenya watasherehekea mashujaa waliopigania uhuru. Hamna kazi aise, ni mapumziko!
Lakini subiri, patachimbika nguo kuchanika uwanjani Kasarani wakati AFC Leopards ikipepetana na Kariobangi Sharks kwenye fainali ya Ngao ya GOtv.
Kilicho mkononi ni tiketi ya kuwakilisha taifa kwenye michuano ya mashirikisho mwakani na vile vile Kshs. 2 milioni kwa mabingwa.
Hizi ni timu mbili ambazo ziliibukia kutoka 64 zilizoanza mashindano haya. Sharks iliiondoa Sony Sugar 2-0 kwenye nusu fainali Leopards ikiwalaza Vihiga United ya daraja la pili 1-0.
Timu zote mbili zilikua na mechi ya ligi juzi Ingwe ikishinda Ulinzi Stars 1-0 nao Sharks wakabanwa 3-1 na mabingwa watarajiwa Gor Mahia mjini Kisumu.
Takwimu zinaipa upatu Sharks ambao wamewapiga Ingwe mara mbili msimu huu; 3-2 kirafiki na 2-0 mkondo wa kwanza wa ligi huku mechi ya marudiano ikiishia sare tasa.
Lakini, kocha wa Ingwe Robert Matano we acha tu! Jamaa anajua kushinda mataji kuliko William Muluya wa Sharks. Matano alishinda ubingwa akiwa na Tusker na Sofapaka.