Kocha Eymael wa AFC Leopards achanganyikiwa

Muktasari:

  • Wikiendi iliyopita timu hiyo ilipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kulala mabao 3-1 mbele ya Chemelil Sugar na hivyo kushuka hadi nafasi ya sita ikisalia na alama 32. Awali ilikuwa imechapwa 2-1 na Tusker.

KILA akipiga hesabu zake hapati jawabu. Sasa kocha wa AFC Leopards, Mbelgiji Luc Eymael, amekiri wazi kuchanganyikiwa akisema tatizo linaloisibu timu yake inayoendelea kuboronga katika mechi za Ligi Kuu Kenya.

Wikiendi iliyopita timu hiyo ilipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kulala mabao 3-1 mbele ya Chemelil Sugar na hivyo kushuka hadi nafasi ya sita ikisalia na alama 32. Awali ilikuwa imechapwa 2-1 na Tusker.

“Ni wazi kuna tatizo ambalo hatujalipatia tiba. Tulifanya mazoezi makali ya wiki moja kabla ya mechi hii, lakini ni kama hakuna lolote tulilofanya,” alisema kocha huyo ambaye pia aliwakosa mabeki Jonas Nahimana na Peter Opiyo.

“Kwa kweli nawalaumu wachezaji wangu. Sielewi kwa nini huwa  wanarudia makosa. Sijui ni nini kinachowasumbua, tunafungwa mabao ya kizembe mno.”

Kuhusiana na mchezo huo uliochezwa Jumamosi, kocha huyo alisema wachezaji wake walipoteza umakini kwa kiasi kikubwa na ndiyo sababu ya kufungwa mabao hayo.

“Ukiyatazama mabao ya Chemelil Sugar utaona yalitokana na masihara tuliyoyafanya. Hakuna bao lililofungwa kwa ustadi kwa kutuzidi maarifa,” alifoka.

Lawama zake zimeenda zaidi kwa makipa wake anaosema ndiyo wanaostahili zaidi kubebeshwa msalaba.

“Nilipomweka benchi Matasi (Patrick) katika mechi dhidi ya Tusker na kumpanga Musalia (Martin), mashabiki walilalamika sana wakimtaka, leo (Jumamosi) nimemrudisha langoni kavuruga tena, sijui nifanye nini,” alilalamika.

Wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni, kuna kila dalili kuwa itakuwa vigumu kwa AFC Leopards kutwaa taji.