Yohana Mkomola, Umri mdogo, mpira mkubwa

Nahodha Azam FC U-17 na timu ya taifa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Yohana Mkomola

Muktasari:

Staa huyo ambaye ni mshambuliaji, alipata umaarufu kutokana na namna alivyojitolea katika kikosi hicho cha Serengeti Boys kilichotolewa hatua ya mwisho ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana na timu ya Kongo-Brazzaville. Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekata rufaa kwa madai kuwa Kongo ilikuwa na vijeba kibao kwenye kikosi chake.

MPAKA Home safari hii ilikuwa maeneo ya Temeke Pile katika mtaa wa Kitomondo B ambako, anaishi nahodha Azam FC U-17 na timu ya taifa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ Yohana Mkomola.

Staa huyo ambaye ni mshambuliaji, alipata umaarufu kutokana na namna alivyojitolea katika kikosi hicho cha Serengeti Boys kilichotolewa hatua ya mwisho ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana na timu ya Kongo-Brazzaville. Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekata rufaa kwa madai kuwa Kongo ilikuwa na vijeba kibao kwenye kikosi chake.

Mkomola anaishi katika chumba kimoja, alichopangiwa na meneja wake, Kambi Zuber anayemuhudumia na kumsimamia katika kila kitu kinachohusiana na masuala ya soka na maisha ya kawaida.

Mambo yake mazuri, kwani utakapoingia geto kwake hautajiuliza anayeishi hapo ni mtu wa aina gani, kila pande kuna viashirikia vya soka kama medali mbalimbali, mipira na viatu.

Ukutani amefungiwa televisheni kubwa ya kisasa kwa ajili ya kuangalia mipira na mambo mengine ya kumsogezea muda kama Play Station wanayotumia kucheza.

NYUMBANI

Mwanaspoti: Hodi!

Mkomola: Karibu, hapa ndio nyumbani, naishi mwenyewe katika chumba hiki kama unavyoniona. Sehemu hii nilipangiwa na meneja wangu, Kambi ambaye ndiyo ananishughulikia kwa kila kitu.

Mwanaspoti: Vipi maisha ya hapa nyumbani ni sahihi kutokana na mazingira yako ya mpira?

Mkomola: Ni sahihi kabisa, ni mahali tulivu nafanya mambo yangu bila kusumbuliwa na mtu yeyote na kuna usalama wa kutosha, kiujumla naishi kama niko nyumbani au Chamazi.

Kuhusu mazoezi, kwangu ni rahisi kwenda Uwanja wa Taifa au Chamazi kwa sababu tupo katikati.

Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani huwa unafanya shughuli gani na mapumziko yako unayatumia vipi?

Mkomola: Shughuli ninazofanya hapa ni usafi katika chumba changu na kufua, chakula ninachokula kuna madada hapa wanapika. Ratiba yangu ya chakula asubuhi ni chai na vitafunwa, mchana wali au ugali samaki au nyama na mboga nyingi na jioni huwa hivyo. Pamoja na msosi wote huo ila ni mpenzi wa ugali samaki.

Katika mapumziko yangu hapa nyumbani muda mwingi nakuwa pale (anaonyesha) kwenye play station nacheza game, wakati mwingine naangalia mechi tofauti za ligi ya hapa nyumbani na nchi tofauti.

Ni mpenzi wa muziki pia na wasanii ninaowapenda kwa Tanzania ni Diamond na nje ya nchi ni Fally Ipupa.

MAPENZI

Mwanaspoti: Hivi unaye mchumba au rafiki wa kike?

Mkomola: Dada umri wangu bado mdogo sina. Rafiki wa kike pia sina nilionao ni wale mnaokutana na kuzungumza, lakini yule wa kubadilishana naye mawazo kabisa hayuko.

Mwanaspoti: Lakini wachezaji wengi wenye mafanikio wamekuwa wakisumbuliwa na wanawake ambao, huwapigia simu na kuwaambia matamanio yao ya mapenzi na wapo wanaowashawishi kwa pesa kwako wewe ipoje?

Mkomola: Ni kweli kabisa, hata mimi nimeshapigiwa simu na kutumiwa meseji za hivyo, lakini sijali huwa napuuzia tu. Mtu akinipigia na kuniambia nakupenda, namwambia asante nashukuru basi, akiendelea na ujinga, naachana naye, tena wapo wengine waliingia na gia hiyo ya pesa.

Siwezi kushawishika na pesa kwa sababu meneja wangu ananipa kila kitu ninachokihitaji na Azam wananilipa pia, hivyo suala la pesa sio tatizo kwangu.

Mwanaspoti: Kwa nini unayakimbia mapenzi?

Nina malengo na maisha yangu najua mambo haya yapo tu. Nikiwa mkubwa na maisha yangu mazuri, nina gari, nyumba na biashara nyingine tofauti na kazi yangu ya mpira ndiyo naweza kufikiria mambo hayo.

Nikijiunga huko nitaharibu ndoto zangu zote kwani, ni ngumu kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja. Nimepata bahati kama hivi kuwa na meneja ambaye anataka nifanikiwe hivyo kamwe siko tayari niharibikiwe.

Mwanaspoti: Utakapokuwa tayari, mke wako unataka awe wa aina gani?

Mkomola: Nataka kuwa na mwanamke anayejiheshimu, mstaarabu, mpole, asiwe mpenda starehe mambo ya disco sijui ufukweni hapana.

Kimwonekano nataka awe wa kawaida, asiwe mweupe kwa sababu nitakuwa nimeolea wenzangu. Mke akiwa mweupe mzuri ni shida, nawaogopa wanawake weupe, wangu nataka awe mweusi sio mzuri sana na wala mbaya sana wa katikati.

KAULI YA MENEJA

Mwanaspoti: Meneja Kambi kwa nini uliamua kumchukua Mkomola na sio mchezaji mwingine?

Kambi: Niliamua kumchukua, Mkomola kutokana na bidii zake, ana maadili ya mpira. Ana nidhamu na anajituma, kiujumla ni mchezaji anayependa mafanikio ndiyo maana nikachukua jukumu la kumwendeleza.

Mwanaspoti: Kwa nini ulimpangia chumba hapa na sio kwingine?

Kambi: Hapa ni karibu na familia yangu hivyo, atakuwa chini ya ungalizi salama na hata mimi ni rahisi kumsimamia na kujua maendeleo yake. Nina jukumu la kumfanya afikie malengo yake uwanjani na kimaisha pia.

MAISHA YA MPIRA, AKATISHA MASOMO

Mkomola anatoka katika familia ya soka ni mdogo wa Stanley na Stephano Mkomola, ambao wamecheza JKT Ruvu na Samwel Mkomola anayekipiga KCM sasa.

Chipukizi huyo amekuwa maarufu kutokana na kufanya kwake vizuri ndani ya kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ pamoja na klabu yake ya Azam.

Ni miongoni mwa wachezaji 14 waliochaguliwa kwenda kwenye kambi ya mafunzo ya soka Afrika Kusini akashiriki mashindano tofauti.

Mwanaspoti: Maisha yako ya mpira yako vipi na Azam upo vipi na uliingiaje?

Mkomola: Nashukuru nilipofika lakini natakiwa kufanya bidii zaidi ili nifanikiwe.

Ni mchezaji wa Azam lakini sina mkataba pale na timu yoyote ikifanya mazungumzo na meneja wangu kwa sasa wakakubaliana naondoka labda kama wao watanisainisha.

Nilijiunga na Azam baada ya kupita kwenye majaribio tulifanyia na kocha, Babu Cheche kabla ya hapo nilicheza Twalipo.

Mwanaspoti: Safari yako ya masomo ipo vipi?

Mkomola: Nilimaliza Shule ya Msingi Mtoni Sabasaba, nikasoma Sekondari ya Kimbiji lakini kwa sababu ya umbali, nilikatisha masomo yangu na kuishia kidato cha pili. Bado ninatamani kusoma, nitazungumza na meneja wangu kujua tunafanyaje.

Natambua elimu ndio kila kitu hasa katika maisha ya sasa hivyo, nina imani kubwa nitarejea shuleni na soka nitaendeleza kama kawa.