WACHOVU: Yanga ya Lwandamina haiwezi kushinda mechi kubwa

Muktasari:

  • Licha ya kufungwa, Yanga ilitafuta mpira kwa tochi. Wachezaji 10 wa Simba walitulia, wakaupiga mpira wa kutosha. Fedheha hii isingeweza kutokea enzi za Kocha Hans Pluijm. Yanga ya Pluijm ilikuwa inacheza soka la kuvutia.

ALIANZA mechi na Azam katika Kombe la Mapinduzi akapokea kipigo cha mabao 4-0. Ikafuata mechi na Simba pia ya michuano hiyo na kupata sare tasa kabla ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalti. Akafuata mechi na Simba tena, safari hii ya Ligi Kuu Bara akala mabao 2-1. Mechi kubwa zimemshinda.

Ubaya zaidi ni kwamba kipigo cha juzi Jumamosi kutoka kwa Simba kilikuwa kibaya zaidi kwa kocha George Lwandamina raia wa Zambia. Hofu kubwa ni pale unapogundua kuwa Yanga ya Mzambia huyo ilifungwa na Simba iliyokuwa na mchezaji mmoja pungufu uwanjani kwa dakika 35. Ni fedheha kubwa.

Licha ya kufungwa, Yanga ilitafuta mpira kwa tochi. Wachezaji 10 wa Simba walitulia, wakaupiga mpira wa kutosha. Fedheha hii isingeweza kutokea enzi za Kocha Hans Pluijm. Yanga ya Pluijm ilikuwa inacheza soka la kuvutia. Ilikuwa inashambulia muda mwingi. Isingekubali kupoteza mchezo dhidi ya Simba iliyokuwa pungufu. Isingewezekana ikafungwa mabao 4-0 na Azam. Haijawahi kutokea chini yake.

Makala hii inakuletea orodha ya mapungufu yanayojionyesha katika kikosi cha Yanga cha sasa kinachonolewa na Lwandamina.

Timu haipo ‘siriazi’

Yanga baada ya kufunga bao la mapema haikuwa makini tena na mchezo. Kipa Deo Munishi ‘Dida’ hakuwa makini hata kidogo. Alitumia muda mwingi kupoteza muda. Kuna wakati aliushika mpira kwa muda mrefu hadi kusababisha adhabu ya ndani ya eneo la hatari. Timu nzima ya Yanga haikuwa na haraka tena na mchezo. Mpira ukiwa wa kurusha na mchezaji wa Yanga yupo karibu bado angesubiri Juma Abdul ama Mwinyi Haji atoke mbali kwenda kurusha. Timu haiwezi kwenda kizembe namna hii.

Katika hali ya kustaajabisha kocha alikuwa ameduwaa tu nje, hakuwa mkali kwa wachezaji wake. Yanga ilikuwa imeukamata mchezo na hakuchukua jukumu la kuwaambia wachezaji wake wacheze kwa kasi zaidi. Yanga ilipopata mpira wa adhabu haikuwa na haraka. Wangeweza kusubiri kipa wao atoke mbali kwenda kupiga. Mambo yanakwenda kienyeji sana katika kikosi cha Yanga cha sasa. Bahati mbaya ni kwamba Simba hawakuwa na ujinga huo. Mpira ulipokufa waliuchukua haraka na kuanza kucheza. Hawakukubali kupoteza muda hata wakati wanaongoza.

Mabadiliko ya ajabu

Kuna uwezekano mkubwa Lwandamina hana uwezo mkubwa wa kusoma mchezo akiwa nje. Wachezaji wanaotokea benchi wamekuwa na mchango kidogo uwanjani. Katika mchezo wa Jumamosi wakati Yanga inaongoza na Simba wakiwa pungufu bado aliendelea kucheza na viungo wawili wazuiaji. Yaani wapinzani wako wako pungufu halafu unaweka wachezaji wengi wa kuzuia uwanjani wa kazi gani? Kulikuwa na haja gani kwa Yanga kuendelea kucheza na viungo Said Juma ‘Makapu’ na Justine Zulu wakati Simba wakiwa pungufu? Anafahamu Lwandamina.

Ajabu zaidi ni kwamba baada ya Simba kusawazisha bao alichukua uamuzi wa kumtoa Amissi Tambwe na kumpa nafasi Deus Kaseke. Yaani timu inatakiwa kushambulia na kupata mabao unapunguza straika na kuongeza kiungo? Huyu kocha wakati mwingine anakuwa muongo. Baadaye wakati mpira unakaribia kumalizika ndipo anakubali kumtoa Zulu na kumpa nafasi Juma Mahadhi. Hata hivyo ni maamuzi ya kuchelewa sana. Ajabu zaidi ni kwamba pamoja na kuwa na wachezaji wengi wa kuzuia bado timu ilikubali kufungwa. Kulikuwa na faida gani ya kufanya hivyo?

Dante wa nini?

Yanga imecheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na Kelvin Yondani katika baadhi ya mechi na kufanya vizuri. Cannavaro alicheza katika ushindi dhidi ya Stand United, Mwadui na Ngaya De Mbe ya Comoro na mechi zote hizo alicheza kwa kiwango cha juu. Ni wazi kwamba Cannavaro alikuwa anacheza kwa kuwa Andrew Vincent ‘Dante’ alikuwa majeruhi, lakini bado hakukuwa na umuhimu wa kumbadili katika mchezo wa Jumamosi. Hata kama Vincent Bossou aligoma kucheza bado hakupaswa kucheza Dante ambaye ametoka kwenye majeraha na hajacheza mechi yoyote ya ushindani.

Matokeo ya kubadili beki ya kati yalipelekea beki ya Yanga kuwa uchochoro. Yondani alicheza vizuri, lakini hakuweza kumaliza makosa yote peke yake. Matokeo yake Dante alikuwa akimsindikiza Laudit Mavugo wa Simba. Kuna wakati Mavugo aliwafedhehesha kwa kuwapiga chenga wachezaji wanne kabla ya shuti lake kugonga mtambaa wa panya. Aibu iliyoje.

Mkata Umeme mmh!

Yawezekana ndiye kiungo mweye pasi zenye macho tulizoambiwa. Yawezekana akawa kiungo anayepunguza hatari ya mashambulizi kwa timu yake. Yawezekana ndiye kiungo wa kiwango cha mashindano ya kimataifa tuliyeambiwa, lakini siyo yule aliyecheza na Simba Jumamosi. Zulu alikuwa taratibu katika muda mwingi wa mchezo. Hakuweza kupunguza hatari ya mashambulizi kwa timu yake. Alipopitwa na mchezaji wa Simba alimfuata kwa nyuma taratibu kama dume la Nyani. Hakuwa na haraka kabisa. Wakati akiwa na mpira hakuweza kupiga pasi zenye macho. Kuna wakati alipotea kabisa na akawa anawasindikiza wachezaji wa Simba. Kazi ipo kwa Yanga kama ni kweli wanamtegemea kiungo huyu katika mechi za kimataifa. Ni wa kawaida sana. Thabani Kamusoko ni bora mara 200 kuliko Zulu.

Viwango vya wachezaji

Tangu Lwandamina amechukua timu viwango vya wachezaji wa Yanga vimeshuka. Deus Kaseke wa enzi za Pluijm siye Kaseke wa sasa. Niyonzima wa enzi za Pluijm siye huyu wa sasa. Tambwe wa enzi za Pluijm siye wa sasa. Juma Abdul wa enzi za Pluijm siye wa sasa. Sijui wamekumbwa na kitu gani. Pengine ana mazoezi magumu na wamekuwa hawayaelewi kabisa.

Ubaya ni kwamba wachezaji wa Yanga wanaokaa benchi uwezo wao ni duni zaidi. Kuna tofauti kubwa kati ya mchezaji wa Yanga anayeanza na yule ambaye yupo benchi. Mfano mastraika Matteo Antony na Malimi Busungu wamekwisha uwezo kabisa.

Geofrey Mwashiuya ambaye alikuwa akitegemewa kama mchezaji wa kubadili matokeo enzi za Pluijm amekuwa hovyo zaidi kwa sasa. Lwandamina ameimaliza Yanga kabisa.

Heshima kwa Omog

Baada ya yote unampongeza Kocha Joseph Omog wa Simba kwa uwezo mkubwa. Omog amedhihirisha kuwa sio kocha wa mchezo mchezo. Kwanza wachezaji wake wanaonekana kuwa fiti. Pili, viwango vya wachezaji wake vinapanda kila siku. Tatu, unampongeza kwa mabadiliko ya kuwapa nafasi Said Ndemla, Shiza Kichuya na Jonas Mkude ambao walibadili kabisa mchezo hiyo juzi. Simba iendelee kumvumilia Mcameroon huyo na itakula matunda  yake.