Yanga kumbe ukuta!

Muktasari:

  • Baada ya msoto wa muda mrefu Yanga ilifanikiwa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kufuzu hatua hiyo baada ya kuwahi kufuzu pia hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1998.

UNASEMA eti yule Mzee Akilimali kapindua kofia? Aaah...wapi! Muulize vizuri Mzungu atakwambia. Tatizo lililowavuruga Yanga kwenye mechi za kina TP Mazembe. Kumbe ni ukuta bwana. Pale nyuma ni tatizo.

Baada ya msoto wa muda mrefu Yanga ilifanikiwa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kufuzu hatua hiyo baada ya kuwahi kufuzu pia hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1998.

Hata hivyo Yanga imeshindwa kufurukuta katika hatua ya makundi baada ya kumaliza katika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake ambapo timu za TP Mazembe na MO Bejaia zimefuzu kucheza hatua ya nusu fainali. Katika hatua hiyo Yanga imeshinda mechi moja pekee dhidi ya Bejaia na kuambulia sare dhidi ya Medeama matokeo yote hayo ikipata nyumbani.

Makala hii inakuletea orodha ya mambo ambayo yamefichuka katika safari ya Yanga kwenye mashindano haya ya Afrika mwaka huu

Kumbe ni ukuta bwana!

Yanga licha ya kuwa na mapungufu kadhaa bado ina nafasi ya kufanya maboresho kidogo ya kikosi chake kwa ajili ya mashidano yajayo. Yanga ina tatizo kubwa katika safu ya kiungo ambapo inahitaji mtu mmoja katika eneo la kiungo mkabaji ili kutoa uhuru kwa Thaban Kamusoko katika eneo la kiungo mshambuliaji. Kwenye ukuta wao kuna tatizo. Inahitaji beki mwingine wa kati mwenye uzoefu ambaye anaweza kupunguza hatari pindi beki wao kisiki, Vincent Bossou anapokosekana. Bossou ndiyo beki pekee ambaye anaonekana kuwa fiti zaidi kwa sasa kwenye ukuta wa Yanga pale kati.

Itakuwa ni jambo la kushangaza kwa Yanga kama itaendelea kuwategemea Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani katika eneo hilo wakati tayari wameonekana kuchoka kimwili na kushindwa kuwa na msaada kwenye ukuta wa Taifa Stars na hata Yanga kabla ya ujio wa Bossou. Andrew Vincent bado anajaribu kuzoea mazingira hivyo anaweza asiwe msaada mkubwa katika siku za usoni.

Tofauti ya viwango

Kuna tofauti kubwa kati ya wachezaji wa Yanga wanaoanza katika kikosi cha kwanza na wale wanaokaa benchi. Ni wachezaji wachache wanaokaa benchi ambao wakiingia uwanjani wanaweza kubadili matokeo. Kuna tofauti kubwa kati ya Donald Ngoma na Malimi Busungu. Kuna tofauti kubwa kati ya Matteo Antony na Amissi Tambwe. Kuna tofauti kubwa kati ya Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya. Kuna tofauti kubwa pia kati ya Andrew Vincent na Vincent Bossou. Tofauti hii imeifanya Yanga kupata wakati mgumu pindi inapomkosa nyota yeyote wa kikosi cha kwanza. Tofauti hii imeifanya Yanga kushindwa kupata matokeo pindi kikosi chake cha kwanza kinapofeli maana nje kunakuwa hakuna mchezaji mwenye uwezo wa kufanya mabadiliko hayo.

Wachezaji wa kigeni

Ni ukweli ulioko wazi kwamba wachezaji wa kigeni wa Yanga wana uwezo mkubwa kuliko wale wazawa. Bossou na Ngoma wamewaacha mbali sana Busungu na Yondani. Hata hivyo bado kuna tofauti kubwa miongoni mwa wachezaji hao wa kigeni. Mbuyu Twite si wa daraja la juu kama Bossou. Obrey Chirwa siyo wa daraja la juu kama Donald Ngoma. Niyonzima siyo wa daraja la juu kama alivyokuwa Kamusoko. Hapa ndipo tatizo linapokuja. Yanga inahitaji kuboresha wachezaji wake wa kigeni na kutafuta wa daraja la juu kama ilivyo kwa Rainford Kalaba na Solomoni Asante pale TP Mazembe. Inatakiwa kutafuta wachezaji wa kigeni wa daraja la juu kama ilivyo kwa Jonathan Bolingi ama Thomas Ulimwengu. Kwa wachezaji wa kigeni wa sasa ni ngumu kufika inapowaza kufikia.

Nidhamu ya mchezo

Katika mechi sita za hatua ya makundi tumeshuhudia wachezaji wawili wa Yanga wakipewa kadi nyekundu huku beki wao Mtogo, Vincent Bossou na straika wao Donald Ngoma wakikosa baadhi ya michezo kutokana na kupewa kadi mbili za njano. Kabla ya kufuzu hatua hiyo ya makundi tuliona Yanga ikipigwa faini ya Dola 10,000 (Sh 20 milioni) kutokana na wachezaji wake wengi kupewa kadi za njano katika mchezo dhidi ya GD Sagrada Esparanca.

Nadir Haroub Cannavaro alipewa kadi nyekundu pia wakati Thaban Kamusoko, Juma Abdul, Amissi Tambwe na Kelvin Yondani wakikosa mechi moja kila mmoja kwa nyakati tofauti kutokana na kupata adhabu ya kadi mbili za njano.

Mlolongo wa kadi hizi ni ishara ya nidhamu mbovu kwa wachezaji wa Yanga jambo ambalo limewagharimu katika baadhi ya mechi.

Mipango ya mechi

Timu ya MO Bejaia imefuzu hatua ya nusu fainali baada ya kufunga mabao mawili tu katika mechi sita za hatua ya makundi. Bejaia iliifunga Yanga bao 1-0 kabla ya kupata matokeo kama hayo dhidi ya Medeama juzi Jumanne. Timu hiyo ilipata sare tasa dhidi ya Mazembe na Medeama ugenini. Katika hatua hiyo Bejaia iliruhusu mabao mawili tu ambapo moja ni dhidi ya Yanga na jingine dhidi ya TP Mazembe. Timu hii inatoa mfano mzuri wa mipango ya mechi katika hatua ya makundi. Yanga haikuwa na mipango hii. Yanga haikufahamu inahitaji kitu gani katika kila mchezo.

Haikufahamu mchezo gani inahitaji sare ama mchezo gani inahitaji ushindi. Hili limeigharimu Yanga ambayo imeshindwa kufuzu nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia.

Yanga pia ilishindwa kupata pointi hata moja ugenini jambo ambalo linaonyesha kuwa timu hiyo bado haijawa na ushindani wa kutosha. Miongoni mwa mitihani mikubwa katika soka la Afrika ni kuweza kupata matokeo walau hata ya sare ugenini. Yanga inatakiwa kuhakikisha inafanikiwa pia katika hili.

Matumizi ya nafasi

Yanga haijawahi kuwa na tatizo kubwa katika kutengeneza nafasi za kufunga. Angalau katika kila mchezo Yanga ilitengeneza si chini ya nafasi nne za kufunga lakini tatizo limekuwepo katika kuzibadili nafasi hizo kuwa mabao.

Mechi dhidi ya Medeama na Bejaia zinaweza kuwa mifano mizuri ambapo Yanga ilikuwa na uwezo wa kushinda kwa mabao zaidi ya matatu lakini ilijikuta imefunga bao moja katika kila mchezo jambo ambalo liliwagharimu baadaye.