Ya Aguero, Guardiola bado jeuri ni ileile

Saturday February 11 2017

 

By Edo Kumwembe

MWANADAMU ameumbiwa maringo, hasa anapokuwa katika ubora wake. Jioni ya Novemba 27, 2008, Pep Guardiola alimvuta Pedro anyanyuke katika benchi ajiandae kuchukua nafasi ya Thierry Henry katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya jijini Lisbon. Barcelona ilikuwa inaiangamiza Sporting Lisbon.

Pep alikuwa ameamua kumtoa Thierry Henry uwanjani na kumwingiza Pedro kwa sababu ya kushangaza katika soka. Kuna kitu Henry alikuwa amekosea uwanjani. Unajua alichokosea? Pep alikuwa amemwambia Henry akae katika winga yake tu. Henry akahama akahamia katika winga nyingine na akafunga.

Kama alidhani kufunga ulikuwa uhodari, basi alikuwa amekosea. Licha ya kufunga, lakini alikuwa amekiuka mipango ya Guardiola. Akamtoa nje akamwingiza Pedro. Hapa jeuri ilikuwa katika ubora wake. Jeuri katika ubora wa hali ya juu zaidi.

Sasa, Pep anajaribu kuonyesha pale Etihad kwamba mwanamume kamili ni yule anayesimamia misingi yake. Tofauti na kilichotokea Lisbon au chochote alichokifanya akiwa Barcelona na Bayern Munich, kule alikuwa anapitia katika raha. Hapa anajaribu kuonyesha misingi yake akiwa katika hali ngumu.

Mechi mbili zilizopita, Pep amemwacha katika benchi Sergio Aguero na nafasi yake inachezwa na kinda wa umri wa miaka 19 tu aliyetua Januari hii akitokea kwao Brazil, Gabriel Jesus. Unapomwacha nje Aguero inamaanisha unamwacha mshambuliaji bora katika Ligi Kuu England kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hakuna kama Aguero.

Amehamia mwaka 2011 tu lakini kwa sasa anashika nafasi ya tatu kwa ufungaji bora wa muda wote klabuni nyuma ya Eric Brook na Tommy Johnson. Ana mabao 154 katika mechi 234 tu. Bado kwa jeuri ile ile ya kumtoa Henry kule Lisbon ndio hii hii ambayo Pep anajaribu kumfanyia Aguero ingawa ni kwa mazingira tofauti.

Aguero haendani na mfumo wa Guardiola. Anafunga sana. Kuna klabu gani duniani haimhitaji Aguero? Kuna klabu gani ambayo Aguero anaweza kukaa benchi duniani?

Hata hivyo, Guardiola ana misingi yake. Nilidhani anajaribu kuisahau kwa sababu ya nyakati ngumu anazopitia England kumbe hapana.

Kifupi, Guardiola anampenda mchezaji anayeushiriki mchezo wote kwa jumla yake. Anamtazama Aguero sio kama mfungaji tu, anataka awe ana uwezo wa kupiga pasi za haraka, kufungulia njia wengine, kupasia wengine wafunge.

Aguero anaweza kukufungia mabao 32 katika Ligi Kuu kwa msimu mzima, lakini akatoa pasi ya bao moja tu. Guardiola hakitaki kitu hiki. Kwa Jesus kuna kitu amekiona. Anamwona anakaba, anafunga, anafungulia njia kwa wengine.

Hii ndiyo sababu ya msingi Aguero kuanza kusugua benchi. Hakuna sababu nyingine. Kwa Guardioala soka siyo mabao peke yake. Ndiyo maana Guardiola asingeweza kuishi na Cristiano Ronaldo na aliweza kuishi na Lionel Messi.

Messi anaweza kufunga, kupiga pasi za mabao, kuchezesha wenzake. Ronaldo pia ana uwezo huo lakini sio katika kiwango cha Messi. Kwa staili hii siyo kama Aguero ana nafasi tena katika kikosi cha City kama Jesus atakuwa na uwezo wa kufanya kazi hii hata kama atakuwa hafiki katika kiwango cha ufungaji cha Aguero.

Pia, Guardiola anataka mshambuliaji ambaye atashiriki katika ukabaji kuanzia mbele wenyewe wanaita ‘high field pressing’. Aguero ni mmoja kati ya wachezaji wavivu na wabinafsi. Anachofikiria yeye ni kuupata mpira na kujitafutia nafasi ya kupiga.

Aguero pia ni mchoyo mzuri wa pasi za mwisho kama ilivyo kwa yule rafiki yake wa Liverpool, Daniel Sturridge. Sehemu ambayo anaweza kupiga pasi ya mwisho mtu afunge yeye anataka kupiga au kuendelea kujitafutia nafasi ya kupiga na kumwacha mwenzake akishangaa.

Katika dunia ya soka la biashara, soka la mabao, unamuachaje Aguero nje? Katika dunia ya soka la misingi na la kanuni kama la Guardiola hatimaye amemwacha Aguero nje.

Tena amemwacha nje kwa sababu ya kinda ambaye licha ya kufunga katika mechi mbili za kwanza lakini bado hajathibitisha ubora wake katika Ligi Kuu England.

Haitakuwa mara ya kwanza. Pep aliwahi kuachana na Ronaldinho, Deco, Eto’o na hata Mario Mandzukic wakiwa katika ubora wao kwa sababu hizi hizi tu. Kuna kitu ambacho Pep anakiona halafu watu wengine hawakioni. Anakiletea ujeuri kwa sababu anaamini siku za usoni wote tutawasahau mashujaa anaoachana nao sasa.

Kwa Aguero safari nadhani imeiva na ambacho kitakuwa kinamkera zaidi ni ukweli kwamba nafasi yake imekwenda kwa kijana wa Brazil mwenye umri wa miaka 19.

Kama kuna kitu ambacho kinawakera Waargentina, basi ni kuporwa nafasi zao na Wabrazili. Kama kuna kitu kinawakera Wabrazili basi ni kuporwa nafasi zao na Waargentina. Wana upinzani mkali wa jadi.

Inapotokea wakashirkiana, kama vile Neymar na Messi, au ilivyokuwa kwa Diego Maradona na Careca pale Napoli, basi hakuna shida. Lakini kama mmoja anamweka nje mwenzake, maumivu yanazidi maradufu.