Wamekula mkwanja, wakasepa zao

Pape Ndaw aliyewahi kuichezea SImba

Muktasari:

HARAKATI za usajili kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara zinazidi kupambamoto kwa klabu kupigana vikumbo kuwania saini za mastaa mbalimbali.


HARAKATI za usajili kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara zinazidi kupambamoto kwa klabu kupigana vikumbo kuwania saini za mastaa mbalimbali.

Klabu kongwe za Simba na Yanga na nyinginezo nchini zinaendelea kuwapa presha wachezaji hususani wazawa juu ya kujua wataibukia wapi msimu ujao.

Presha zaidi inakuja baada ya kuibuka kwa utamaduni wa kunyakua nyota kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakipokezana katika klabu hizo, hata kama wakati mwingine huwa hawana umuhimu wa kusajiliwa na klabu hizo.

Klabu hizo kubwa zimekuwa zikiingizwa chaka kwa kusajili wachezaji wa kigeni kwa kuwaangalia katika mechi moja tu ama kudokezwa kipambe na wapiga hela wanazitumia klabu kujinufaisha kabla ya kushtuka wameliwa.

Kuna baadhi ya nyota kutoka nje wamekuwa mzigo kwa klabu zilizowanyakua, yaani ni kama wanakuja nchini kuvutwa mkwanja kisha wanasepa zao kilaini kutokana na kushindwa kufanya vile ambavyo mashabiki wamekuwa wakiwatumainia.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya wachezaji ambao walikuja nchini lakini ghafla kwa kushindwa kufanya lolote la maana wakapotezwa na kutimka zao wakiwa wameshavuna chao mfukoni.

 

BRIAN MAJWEGA

Winga huyu alipotua Azam kwa mara ya kwanza alikua winga mwenye nguvu ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Lakini ghafla mambo yakaanza kubadilika na kuwa ndivyo sivyo hali iliyomfanya awe anaishia benchi kabla ya kutimka kwao na baadaye kurejea msimu uliopita kuichezea Simba.

Licha ya mashabiki wa Simba kumtumainia Mganda huyo kutokana na jinsi Kocha Dylan Kerr alivyomkubali, hali haikuwa shwari kwani baada ya Kocha huyo Muingereza kutimuliwa, Majwega alipata wakati mgumu mbele ya Jackson Mayanja ambao hawakuweza kuendana sawa, hivyo kukosa namba kikosini hapo na hata akipangwa anakua katika kiwango cha kawaida cha kumshawishi kocha.

 

YOSSOUF BOUBACARY

WINGA huyu alipokuja nchini walimpachika jina la ‘Mzee wa Faulo’ kwa jinsi ambavyo alikuwa na ufundi katika upigaji wa mipira iliyokufa.

Katika kombe la Mapinduzi alicheza vizuri na watu wakiweka matarajio kuwa atafanya vizuri zaidi katika ligi lakini hali iligeuka kuwa tofauti na mashabiki wakaanza kumbeza kuwa ni mchezaji wa faulo ambaye hana kazi nyingine yoyote uwanjani na klabu hiyo imetangaza kuachana naye.

 

ALLAN WANGA

Straika huyu alikuwa katika kiwango kizuri alipokuwa Al Merreikh ya Sudan na Azam ikavutiwa naye na kumsajili ili kuongeza nguvu katika kikosi chao kwa vile Azam ilikuwa ikihitaji zaidi nguvu ya ushambuliaji katika mashindano ya kimataifa.

Wanga alivyokuja Azam hajaonyesha cheche zozote ambazo ziliwashawishi viongozi wa Azam kumsajili kutokea Sudan na msimu ulivyomalizika wameamua kuachana na mchezaji huyo na kurejea kwao Kenya.

 

KPAH SHERMAN

Alipofika ukimuangalia tu kwa jinsi anavyoonekana utasema kuwa jamaa ni bonge la mchezaji kweli kweli kwani alikuwa na mwili wa kimichezo uliojaa misuli na pia alikuwa na kimo cha kuvutia.

Sherman alishindwa kuendelea na Yanga kutokana na kiwango chake kuwa cha kawaida mno, hivyo kuifanya Yanga imuuze katika klabu ya Mpumalanga inayoshiriki Ligi Kuu nchini Afrika Kusini, lakini pia hata alipofika huko alicheza na kisha kutolewa kwa mkopo katika klabu ya Cape town Santos.

 

PAPE NDAW

Kati ya usajili mbovu ambao Simba iliufanya msimu uliopita basi ni huyu jamaa aliyekuwa mrefu kupita nyota wote nchini, Pape N’Daw kutoka Senegal.

Straika huyo hata kama hakupewa fedha za usajili, lakini mishahara na posho alivuta sana Msimbazi, licha ya ukweli hakuwa mtu wa soka uwanjani zaidi ya vitimbi.

N’Daw ‘Mr Power Bank’ kwanza aliwahi kuingia uwanjani akiwa na viatu aina ya Adidas ambavyo vilikuwa vimechoka kwa kuchanika chanika lakini pia alitoa kali ya wiki kwa kuingia na hirizi uwanjani hali ambayo ilizua mtafaruku kwa wapenzi wa soka. Mpaka anaondoka nchini alikuwa hajaifanyia lolote timu hiyo.

 

SIMON SSERENKUMA

Huyu jamaa alikuja na kaka yake Dan Sserenkuma. Simon alionekana kuwa na kipaji cha hali ya juu zaidi ya kaka yake ambaye hakuendana na kasi kabisa ya timu na kujikuta akitimuliwa mapema.

Hata hivyo Simon, hakumudu sana Msimbazi kwani alionekana kuchemka kama kaka yake tu na hatimaye kutimuliwa, kwani haikuisaidia Simba kama ilivyotarajiwa.

 

RAPHAEL KIONGERA

Licha ya kuwa alikuwa akipewa kifua na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo nyota huyu alishindwa kuwashawishi makocha Kerr na Mayanja kuweza kumuamini na kumpanga.

Awali Kiongera alikuwepo Simba, lakini aliachwa baada ya kuwa majeruhi na kutimkia India na hata aliporudi alijiunga na timu ya Kenya ya KCB na baadaye kurudi Simba ambapo hakuonyesha jipya.