Wamefunika mbaya Taifa

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilikuwapo uwanjani mwanzo mwisho kufuatilia mtanange huo. Hapa imewapa alama hizi ambazo ni chini ya kumi kwa nyota waliocheza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

ZILE tambo za pambano la watani zimeisha. Hiyo ni baada ya juzi Jumamosi timu hizo kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba waliokuwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani zao Yanga.

Mwanaspoti lilikuwapo uwanjani mwanzo mwisho kufuatilia mtanange huo. Hapa imewapa alama hizi ambazo ni chini ya kumi kwa nyota waliocheza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

YANGA

Dida-6

Mashambulizi yote makali yaliyoelekezwa langoni mwake yalizaa mabao katika mechi hiyo ya juzi, licha ya kuwa likizo kwenye muda mwingi wa kipindi cha kwanza.

Aliruhusu mpira wa krosi ndani ya eneo lake na kuisaidia Simba kujipatia bao la kusawazisha, pia alifanya uzembe wa kukaa na mpira mkononi zaidi ya sekunde sita na kuipa Simba faulo ambayo ingeweza kuwapa bao wapinzani.

Juma Abdul- 6

Hakuwa katika kiwango chake cha siku zote, kwani hakupandisha mashambulizi na alionekana kuchoka mapema jambo lililoufanya upande wake usitengeneze nafasi za mabao kama ilivyozoeleka.

Alimfanya Ibrahim Ajibu atawale kwenye upande huo kuiweka matatizoni safu ya ulinzi ya Yanga.

Haji Mwinyi- 5

Alianza mchezo vizuri kwa kupandisha timu na kujitahidi kumdhibiti Ibrahim Ajibu, lakini alichoka kwenye kipindi cha pili hasa baada ya Kichuya kuingia na mabao yote mawili yaliyofungwa na Simba yalitokea upande wake.

Andrew Vincent- 6

Alipata wakati mgumu kumdhibiti Laudit Mavugo na alicheza faulo za mara kwa mara ambazo ziliirudisha Simba mchezoni hasa kipindi cha pili.

Kelvin Yondani- 8

Alifanya kazi kubwa ya kurekebisha makosa ya Andrew Vincent na alikuwa imara kwenye mapambano ya kutumia nguvu dhidi ya mastraika wa Simba. Hata hivyo matokeo yamemwangusha.

Justine Zulu-7

Aliilinda vyema timu kipindi cha kwanza na kupiga pasi nyingi sahihi ambazo zilifikia walengwa kwa usahihi, ingawa baadaye alionekana kupungua kasi kabla muda ulivyosonga mbele na hatimaye kutolewa kumpisha Juma Mahadhi.

Simon Msuva-7

Alifunga bao pekee la Yanga kwenye mchezo huo kwa mkwaju wa penati dakika ya tano ya mechi.

Alijaribu kuwasumbua mabeki wa Simba hasa Mohammed Hussein ingawa dakika za mwishoni alionekana kuchoka.

Thabani Kamusoko-6

Alicheza kwa dakika 44 kabla ya kuumia na kutolewa kisha nafasi yake ikachukuliwa na Said Juma ‘Makapu’

Kwa muda aliocheza alimudu kutawala eneo la kiungo na kuilazimisha Simba kufanya mabadiliko ya mapema dakika ya 26 kwa kumtoa Juma Luizio na kumuingiza Said Ndemla ilikuimarisha safu ya kiungo.

Obrey Chirwa-7

Kasi yake iliwapa wakati mgumu mabeki wa Simba ambao walimchezea faulo za mara kwa mara zilizoipa faida Yanga kwa kupata penalti dakika ya tatu napia kumponza Janvier Bokungu wa Simba kulimwa kadi nyekundu dakika ya 55.

Amissi Tambwe-5

Hakuwa na kipya ndani ya uwanja na alitiwa mfukoni na Abdi Banda kabla ya kutolewa dakika ya 70 na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke.

Niyonzima-6

Alipiga pasi nyingi za pembeni na alipiga chenga nyingi zisizo na msingi ambazo hazikuisaidia Yanga.

Walioingia

Said Juma ‘Makapu’-5

Deus Kaseke-6

Juma Mahadh-4

SIMBA

Agyei- 8

Simba wamepata bahati ya kuwa na kipa mwenye sifa zote znazohitajika kwa kipa kuwa nazo langoni.

Aliituliza timu vizuri na kuokoa michomo yote iliyoelekezwa kwake. Bahati mbaya alishindwa kuokoa penati ya Msuva ingawa alifanya kazi kubwa ya kuokoa mipira ya krosi ambayo ilikuwa inatesa Simba.

 Alifanya vizuri muda mwingi wa mechi, lakini alikuja kufanya kosa la kumchezea rafu Chirwa aliyekuwa anaenda kufunga, ambalo lilimfanya aonyeshwe kadi nyekundu.

Mohammed Hussein-6

Alisumbuliwa na Msuva katika kipindi cha kwanza jambo lililomfanya ashindwe kupandisha mashambulizi.

Hata hivyo aliamka kipindi cha pili na kumficha Msuva huku akihusika katika kuanzisha mashambulizi langoni mwa Yanga.

Novaty Lufunga-3

Amekuwa na tatizo sugu la kutojiamini huku pia akikosa uamuzi wa haraka juu ya wapi apeleke mpira pindi anapokuwa na mpira mguuni. Mfano wa hilo ni pale aliposababisha penalti iliyozaa bao la kufutia machozi la Yanga.

Abdi Banda-8

Alifanya kazi nzuri ya kudhibiti mashambulizi ya ana kwa ana dhidi ya mastraika wa Yanga. Aliokoa vizuri mipira ya chini na juu huku akiweza kumficha Amissi Tambwe.

Muzamiru Yassin-6

Alikuwa na wakati mgumu kwenye kipindi cha kwanza mbele ya Thabani Kamusoko na hakuweza kuipandisha timu, lakini alirudi mchezoni kipindi cha pili hasa baada ya kubebwa na uwepo wa Said Ndemla.

Ibrahim Ajibu-9

Anastahili kuwa mchezaji bora wa mechi ya jana. Alihaha uwanja mzima kuhakikisha anawaweka mabeki w Yanga kwenye wakati mgumu.

Uwezo wake wa kumiliki mpira uliipa mwanya Simba kuibana Yanga jambo lililoifanya iweze kuibuka na ushindi.

James Kotei-8

Aliweza kutengeneza uwiano mzuri wa kuzuia na kushambulia na aliziba njia za ambazo Yanga wamekuwa wakizitumia kumpelekea mipira Amissi Tambwe.

Laudit Mavugo-8

Ameanza kuonyesha umuhimu wake ndani ya kikosi cha Simba na alikuwa mwiba kwa mabeki wa Yanga hasa Andrew Vincent.

Bao lake alilofunga ni la tatu kufunga kwenye mechi tatu mfululizo jambo lililomfanya aweke rekodi ya kipekee.

Mohammed Ibrahim-6

Hali ya kuwa majeruhi muda mrefu inaonekana kumgharimu mchezaji huyo kwani hakuonyesha makali yake ambayo humfanya aogopwe na timu pinzani.

Hata hivyo kuna wakati alijitahidi kuonyesha uwezo binafsi, lakini alipata kigugumizi cha miguu mara kwa mara kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mkude.

Juma Liuzio-5

Mechi ilimkataa na alimpa kazi ngumu beki wake Mohammed Hussein kuwadhibiti Juma Abdul na Saimon Msuva na haikushangaza kuona akitolewa dakika ya 26 na nafasi yake kuchukuliwa na Ndemla.

Walioingia

Said Ndemla-7

Shiza Kichuya-8

Jonas Mkude-7