Wajumbe wamvuruga Hayatou Caf

Friday March 17 2017Issa Hayatou

Issa Hayatou 

By IBRAHIM BAKARI

OGOPA kura ya siri, ogopa wajumbe wanaopiga kura huku wanakuchekea na kukushabikia, ogopa. Ogopa watu wanaojifanya wako karibu na wewe kabla ya kupiga kura, kumbe wanakung’onga.

Wanakufariji kabla ya matokeo, wanakupa matumaini fifi ambayo kwa kuwa unataka nafasi, unaamini na kuona wewe bado ni hitaji la wajumbe.

Hali hiyo imemkuta Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) aliyemaliza muda wake, Issa Hayatou wa Cameroon, ambaye ni mwanariadha aliyeangushwa na kocha wa soka, Ahmad.

USHINDI WA AHMAD

Ahmad Ahmad aliyembwaga Hayatou kwa kura 34 kwa 20, ni Rais wa Shirikisho la Soka Madagasca aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa nia ya kutaka kuleta mabadiliko ya soka la Afrika.

Mwanzoni hakuwa akiungwa mkono zaidi ya Ukanda wa Cosafa na bosi wa NFF ya Nigeria, kasi ya kumnadi iliongezeka kadiri siku uchaguzi ulivyokuwa ukikaribia.

Ushindi wa Ahmad ni kama mshtuko kwa wadau wa soka, kwani amefanikiwa kuung’oa mbuyu uliokuwa na mizizi tangu Machi 1988.

ULIVYOKUWA

Baada ya matokeo kutangazwa, ukumbi ulilipuka shangwe. Kila mmoja alikuwa mwenye bashasha huku wajumbe wa kambi ya Hayatou wakionekana kana kwamba wamemwagiwa maji.

Ahmad, 57, baba wa watoto wawili, alikuwa mmoja wa wanasoka wakali wa Madagascar kabla ya kugeukia ukocha na baadaye kuwania uongozi katika Shirikisho la Soka Madagascar mwaka 2003.

MIPANGO SASA

Ahmad mpango wake ni kuleta mabadiliko ndani ya Caf na wajumbe walionekana kuwa na imani naye. Uzuri wa Ahmad analindwa na nguvu ya Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka ( Fifa), Gianni Infantino.

“Unapojaribu kufanya jambo, unamaanisha unaweza,” Ahmad aliwaambia waandishi wa habari baada ya matokeo kutangazwa. “Kama siwezi kufanya kitu, siwezi kusimama.”

WAPAMBE

Kila mahali hakukosekani wapiga mavuvuzela. Wapambe wa kambi ya Ahmad walikuwa wakishangilia, wakikumbatiana kila mahali huku wengine wakimbeba bosi huyo.

Mtumishi huyo mstaafu wa Serikali ya Madagascar ambaye anatumia jina moja kila mahali, Ahmad‚ atakuwa na kazi ya kufanya mabadiliko ya maendeleo ndani ya CAF.

Kati ya mambo hayo ni kusimamia suala la kuongeza timu za Afrika Kombe la Dunia, kuinua soka ya Afrika kikanda, kusimamia mabadiliko ya katiba na kutokomeza rushwa.

SIMANZI KAMBI YA HAYATOU

Wakati upande mmoja ukiwa umelipuka kwa furaha, wajumbe wa kambi ya Hayatou walikuwa kimya wakiwa hawaamini kilichotokea.

Hayatou 70, alianza kuongoza CAF tangu mwaka 1988 wakati huo mchezaji nyota wa Barcelona, Lionel Messi akiwa na umri wa miezi tisa tu.

Kiongozi huyo ambaye ni mkongwe katika Fifa, alianza kuongoza soka la Afrika, Machi 10, 1988 alikuwa akiwania kuingia ofisini kwa mara ya nane. Uchaguzi huo umefanyika katika mkutano mkuu wa 39 wa CAF.

Pamoja na mengine mengi, Hayatou anabaki na sifa kuongeza idadi ya timu katika fainali za Kombe la Dunia pamoja na kuongeza idadi ya wadhamini wa mashindano ya klabu na mataifa ya Afrika.

Hayatou hakuwahi kucheza soka, alikuwa mahiri katika kikapu na riadha. Aliiwakilisha Cameroon katika mpira wa kikapu na riadha mita 400 na 800 akivunja rekodi mbalimbali.

Ndani ya utawala wake, Hayatou aliwahi kupingwa na Armando Machado wa Angola na Ismael Bhamjee wa Botswana, lakini wakashindwa kumng’oa.

FITINA ZILIANZIA ZIMBABWE

Mapema Februari, Rais wa Chama cha Soka Zimbabwe, (Zifa), Phillip Chiyangwa aliitisha mkutano aliosema kuwa ni kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Aliwaalika wenyeviti na marais wa vyama na mashirikisho ya soka 24 Afrika waliohudhuria hafla hiyo ambayo alisema ni kushukuru kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika, (Cosafa).

Hayatou alituma ujumbe na kusema mkutano huo utaivuruga CAF na kutaka usifanyike.

Chiyangwa alisema amewaalika marafiki zake na hawatarudi nyuma kuhusiana na sherehe hizo. Bosi huyo wa Zimbamwe pia alikuwa ndiye meneja wa kampeni wa Ahmad.

Rais huyo wa Zifa alisisitiza kwamba mkutano huo ulikuwa ni hafla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, kuadhimisha miaka yake 58 na uzuri inafanyika wakati huo akiwa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika, (Cosafa) baada ya kuchaguliwa mapema Desemba mwaka jana. Hayatou hakualikwa kwenye hiyo hafla hiyo. Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura, kutoka Senegal, alihudhuria mkutano huo wa Harare na bilionea wa Afrika Kusini, Patrice Motsepe naye alikuwa mmojawapo.

Hafla hiyo ilihudhiriwa pia na Rais wa Fifa, Infantino ambaye alitumia nafasi hiyo ‘kumwaga sumu’ akisema anataka kuona mabadiliko ndani ya CAF.

Infantino alisema anataka kuona kunakuwa na mabadiliko, wakongwe wakiondolewa kama ilivyokuwa kwa Rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter.

Infantino alisema kitendo cha Blatter kupoteza nafasi yake Fifa, kimetoa nafasi kwa vijana kuingia kwenye utawala na kufanya mambo kisasa zaidi, kama ambayo Ahmad anataka kuyafanya.

Rais huyo wa Fifa alionyesha waziwazi kumkataa Hayatou kwa kile kinachoelezwa alihusika kuwashawishi wajumbe wa CAF wampigie kura, Rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa kwenye uchaguzi wa mwaka jana wa Fifa, ambao Infantino ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Uefa, alishinda kwa kura 88 kati ya 115 katika raundi ya pili.

Infantino, aliyekuwa Afrika Kusini kwa ziara ya siku tatu kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Fifa aliwataka waziwazi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CAF kumpigia kura  Ahmad kwani itakuwa faida kwao na hata kwa Fifa.

Rais Infantino, aliwaeleza wakuu wa vyama vya soka waliokusanyika Harare, Zimbabwe kwamba ni wakati sasa wa kumtosa Hayatou kwa kutaka kujimilikisha madaraka ya CAF, wakati hakuna maendeleo ya maana katika soka Afrika.