STEPHEN AKHWARI: Wagiriki wampa Scania mbili mpya, waziri ampora

Muktasari:

Mbio zilishaisha muda mwingi tu, hata sherehe za kugawa medali zilimalizika pia, kila mtu akajua mambo yameisha na watu wakaanza kutoka uwanjani. Kwa mbali zikaonekana pikipiki za eskoti zinamsindikiza mtu anayekuja akitembea huku damu zikimvuja miguuni baada ya kuumia akiwa mbioni, alikuwa ni Akhwari.

JOHN Stephen Akhwari. Ni jina la mwanariadha mkongwe wa Tanzania mwenye rekodi ya kipekee katika kumbukumbu za kimataifa za mchezo huo. Mwaka 1968 katika mbio za Olimpiki kule Mexico, alipewa tuzo ya aina yake kutokana na tukio la ajabu alilolifanya.

Mbio zilishaisha muda mwingi tu, hata sherehe za kugawa medali zilimalizika pia, kila mtu akajua mambo yameisha na watu wakaanza kutoka uwanjani. Kwa mbali zikaonekana pikipiki za eskoti zinamsindikiza mtu anayekuja akitembea huku damu zikimvuja miguuni baada ya kuumia akiwa mbioni, alikuwa ni Akhwari.

Alipoulizwa kulikoni, alisema licha ya kuumia kwake kulikomfanya ashindwe kuendelea kukimbia, amelazimika kukataa kusikiliza ushauri wa kujitoa, hivyo kutembea mpaka kufika uwanjani hapo ili aweze kutimiza kile alichotumwa na nchi yake, yaani kumaliza mbio.

Dunia nzima ikamshangaa, wazungu wanavyojua kuthamini, hiyo ikawa rekodi inayoheshimika kimataifa mpaka leo na kuna tuzo imepewa jina lake ikiheshimu ari na moyo wa kujituma bila kukata tamaa.

Achana na hilo. Akhwari anayo stori nyingine kali isiyofahamika. Inahusu kuyeyuka kwa Scania zake mbili, unajua ilikuwaje?

 

TUMJUE KWANZA AKHWARI NI NANI

Alizaliwa mwaka 1938 wilayani Mbulu, Manyara akiwa ni mtoto wa saba kati ya watoto 18 wa familia ya mzee Stephen Akhwari aliyekuwa Mwalimu wa Dini katika Kanisa Katoliki. Mama yake aliitwa Veronica Qamara.

Riadha kwake amezaliwa nayo. Alianza mbio tangu utotoni hasa alipokuwa Darasa la Tatu katika Shule ya Endagikot. Hadi anamaliza Darasa la Nane (enzi za mkoloni) mwaka 1958, alishakuwa mahiri katika mchezo huo.

Ni mwanariadha wa kwanza Mtanzania kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya kukimbia katika mbio za Afrika Mashariki zilizotimka Kenya mwaka 1962, huko alipata tiketi ya kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika katika jijini Perth, Australia baadaye mwaka huo na kufanikiwa kushika namba sita.

Pia aliwahi kuzawadiwa soda katika mbio za Siku ya Malkia wa Uingereza enzi hizo za ukoloni.

“Nilikuwa bado mdogo, nilishindana na wakubwa na nikawa mtu wa 40, Bruce Ronaldson (aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu), akanizawadia soda ya Coca Cola maana nilikuwa mshiriki pekee mwenye umri mdogo. Enzi zile za ukoloni Mwafrika kunywa soda lilikuwa ni jambo lisilowezekana,” anasema.

 

STORI YA HIZO SCANIA

Anasema mwaka 1963 alikwenda Ugiriki kwenye mashindano ya kimataifa ambako alikumbana na wanariadha wengi maarufu kutoka kona mbalimbali za dunia na kwa kuwa alishaanza kupata uzoefu hakuwa na wasiwasi wowote.

“Kule nilishika nafasi ya pili, mshindi wa kwanza alipewa kikombe, jani ambalo ni heshima kwa utamaduni wa Wagiriki pamoja na hundi ya Dola 2000,” anasema Akhwari.

“Ilipofika zamu yangu niliyeshika nafasi wa pili, nilipewa pia kikombe, jani na hundi ya Dola 1,000. Sikuamini, zilikuwa fedha nyingi sana kwangu kwa wakati ule.

“Zilinipa wakati mgumu sana wa kupanga cha kuzifanyia, nakumbuka siku ile sikulala. Lakini nikiwa njiani wakati narudi nyumbani nikafikia uamuzi wa kununua scania mbili, maana enzi hizo scania moja ilikua inauzwa Sh50,000 na Dola 1,000 kwa wakati huo ilikuwa sawa na Sh100,000.

“Kwenda Ugiriki nilifadhiliwa na wananchi wa Ugiriki waliokuwa wakifanya kazi hapa nchini, ushindi wangu uliwashangaza wengi, hivyo niliporejea niliwakuta viongozi wengi pamoja na wananchi wakinisubiri pale Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam.

“Aliyeongoza mapokezi alikuwa Waziri wa Michezo na Utamaduni (Lawi Nangwanda Sijaona), baada ya kupiga picha akaniambia nimpe ile hundi kwa ajili ya usalama zaidi ili siku ya pili nikaifute ofisini kwake.

“Sikuwa na wasiwasi nikampa, lakini siku ya pili nilipomfuata ofisini kwake kibao kikageuka. Akasema Sheria ya Michezo hairuhusu kijana kuwa na fedha zaidi ya Sh14.

“Nilirudi nyumbani nikiwa na mawazo tele kichwani na hata usiku sikuweza kulala maana nilijua ndoto zangu zimeanza kupotea kwa sababu ya tamaa ya mtu mmoja kwani hakuniambia zile fedha zinapelekwa wapi. Scania zangu zikapotelea hapo.”

Anasema hakukubali kirahisi kwani aliamini huo ni uporaji, hivyo aliporudi kwao Mbulu akashtaki kwa Mkuu wa Wilaya, Shamshama na kwa Mbunge wake, Herman Sarwat.

“Lakini haikusaidia kitu hata na wao waligonga mwamba, ndipo nikaamua kuachana na riadha kwa kuamini wanariadha wengi watakuwa wanadhulumiwa stahiki zao tena na viongozi wakubwa,” anasema.

 

JESHI LAMRUDISHA KWENYE RIADHA

Anasema alisusa kabisa. Lakini ilipofika mwaka 1965 aliitwa na Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Mirisho Sarakikya, ambaye alimshawishi aingie jeshini ili aweze kuendelea na riadha.

“Nilimwamini yeye baada ya majadiliano marefu, nilipewa mkataba wa miaka sita hivyo nikaendelea na riadha nikishiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi, lakini baada ya miaka hiyo nikaachana kabisa na mchezo huo.”

 

 

AFAFANUA KISA CHA MEXICO

Katika mbio zile za Olimpiki kule Mexico, anasema alikwenda akiwa na ndoto za kurejea na medali kwa vile wengi wa waliokwenda huko, alikuwa amewashinda katika mbio zilizofanyika Kampala, Uganda za Afrika Mashariki mwaka mmoja uliotangulia na yeye hakuwa ameshuka kiwango.

“Nilianza vizuri mbio zenyewe (za kilomita 42), lakini mambo yalibadilika zikiwa zimebaki kilomita 10. Kosa lilifanyika hapa kwetu wakati wa maandalizi, kambi ilikuwa Dar es Salaam ambapo umbali kutoka usawa wa bahari ni nyuzi sifuri (low sea level), hivyo pana Oxygen nyingi,” anasema.

“Kule Mexico tulikokwenda kushindana pako nyuzi 7,000 kutoka usawa wa bahari (high sea level) ambako oksijeni inakuwa ya shida hasa kwa mwanariadha wa mbio ndefu.

“Matokeo yake nilipokuwa ninakimbia katika hali hiyo ya hewa ambayo mwili wangu haukuwa umejizoesha nayo, mishipa ya damu kwenye misuli ikaziba na damu ikakosa pa kupita, hatimaye ikapasuka na damu kuanza kunitoka miguuni kabla ya kufungwa bendeji na watoa huduma. Walinipiga picha nyingi huku wakinishauri nijitoe. Sikuwa tayari kwani nilipanga kumaliza mbio kwa hali yoyote ile, sikutaka kuishia njiani.”

Katika mbio hizo zilizoshirikisha wanariadha 75, ni wakimbiaji 57 tu ndio walizimaliza. Kwa kilichomtokea, Akhwari alikuwa wa mwisho na alitumia muda wa 3:25.27 wakati Mamo Wolde raia wa Ethiopia alitumia saa 2:20.26 na kuwa mshindi.

 

ANAVYOSIKITISHWA NA NCHI HII

“Viongozi wa nchi hii wananisikitisha sana, hawajali michezo. Baada ya kuacha kukimbia nimejaribu kutoa ushauri mbalimbali weee juu ya riadha, lakini mwitikio unakuwa hafifu mno,” anasema kwa masikitiko.

“Mfano mzuri ni yale maneno niliyoyasema Mexico mwaka 1968 kuwa ‘Nchi yangu haikunituma kuja hapa kuanza mbio, bali kumaliza mbio’. Kwa wenzetu yanatumika hadi sasa kujenga hamasa, lakini Tanzania sijawahi kuona yakitumika na wala watu hawana habari.

“Mwaka 2003 Kuna wafadhili walijitokeza kutoka Australia ambao walitaka kunijengea kituo cha riadha kiitwe John Stephen Akhwari Athletic Foundation, kwa ajili ya heshima yangu.

“Tulipata eneo la ekari 200 pale Ngaramtoni, enzi zile Mkuu wa Mkoa wa Arusha alikuwa Daniel Ole Njoolay. Mipango ilikuwa inaenda vizuri, mpango ulikuwa hivi, asilimia 60 ya mapato ingekuja kwangu, asilimia 40 ingeingia serikalini na asilimia 10 ingetumika kwa ajili ya shughuli za kituo. Sijui kulitokea nini serikalini, mpango ukafa.”

 

APEWA NISHANI

Anazo tuzo tatu za nishani ya heshima alizopewa na marais watatu wa Tanzania waliopita. Wa kwanza ni Ally Hassan Mwinyi (Nishani ya Heshima, mwaka 1992), Benjamin Mkapa (Nishani ya Uzalendo wa Taifa, 2001) na Jakaya Kikwete (Nishani ya Ushujaa wa Taifa, 2013).

Akhwari mwenye miaka 79, ana watoto sita, wawili wa kiume. Kati ya wanaye, ni mmoja tu (Rogath Stephen) ndiye aliyefuata nyayo zake katika riadha. Rogath amewahi kuiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali yakiwamo ya Paris Marathon.