Vipigo vya kihistoria

Muktasari:

  • Unakumbuka kipigo cha 5-0 walichokipata Yanga mbele ya watani wao wa jadi, Simba Septemba 11, 2012 hicho hakijasahaulika na ni kovu ambalo litadumu kwa miaka mingi sana.

KUFUNGWA kunauma bwana asikwambie mtu, hakuna shabiki anapenda kushughudia timu yake ikifungwa na ndio maana si ajabu kuona mashabiki wanaanzisha vurugu uwanjani.

Wakati mwingine wanaanzisha vurugu kutokana na timu kuonewa, kuzidiwa idara zote hivyo, hawana cha ziada zaidi ya kuvuruga mchezo ili wakajipange upya.

Lakini, kitu cha kushangaza ni namna mashabiki wa soka wanavyosahau kwa haraka sana maumivu wanayoyapata mioyoni baada ya timu zao kufungwa.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa, vipigo vitakatifu hutengeza makovu katika mioyo na akili ya mashabiki na wachezaji kiasi kwamba sio rahisi kusahaulika.

Unakumbuka kipigo cha 5-0 walichokipata Yanga mbele ya watani wao wa jadi, Simba Septemba 11, 2012 hicho hakijasahaulika na ni kovu ambalo litadumu kwa miaka mingi sana. Sasa achana na hayo hebu twende kimataifa kushuhudia baadhi ya vipigo vya maana ambavyo mpaka kesho vitaendelea kukumbukwa.

LINCOLN RED IMPS 1-0 CELTIC

Hivi umewahi kusikia klabu inayoitwa Lincoln Red Imps? Klabu hii haijawahi kutambulika kokote katika ulimwengu wa soka hadi hivi karibuni ilipoiduwaza Celtic ya Scotland.

Tuki hili lilitokea miezi kadhaa iliyopita, katika mechi za kufuzu michuano ya klabu bingwa Ulaya. Mtu anaweza kujiuliza inakuwaje ushindi wa 1-0 ukawa dili kiasi cha kujadiliwa vijiweni, ishu iko hivi, klabu hii haina tofauti na Panone iliyoasisiwa na mafundi wajenzi. Kikosi karibu kizima cha wababe hao wa Celtic, ni wachezaji wa ‘misheni town’ yupo dereva teksi, Polisi na zima moto.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba kabla ya mechi hiyo, mchezaji mmoja alikuwa ndiyo kwanza amemaliza shifti ya kuendesha teksi, kabla ya kujumuishwa kikosini. Kwa timu ya aina hiyo, kocha yeyote angetegemea kuvuna pointi na mabao mengi, lakini mambo yalikuwa tofauti kwa Brendan Rodgers, akapigwa moja, mchezo ukaishia hapo.

Mechi ya marudiano, iliyopigwa nchini Scotland, ilikuwa na nafuu kwa Rodgers aliyetimuliwa Liverpool, kwani vijana wake walifanikiwa kuwafunga kwa taabu, ‘wahuni hao wa mtaa’ mabao 3-0 na baadaye kuendeleza fomu nzuri ikiwemo sare ya 3-3 dhidi ya Man City lakini ni dhahiri kuwa kichapo kile bado inawauma!

UHOLANZI 5-1 SPAIN

Unakumbuka kile kichwa cha kuchupa cha Robin Van Persie? Hii mechi ilikuwa ni udhalilishaji mkubwa kwa Hispania iliyosheheni kila aina ya tambo na ufundi. Hispania ilikuwa na kikosi imara ambacho hakijawahi kutokea katika kipindi cha miaka sita ya soka la kimataifa, naamanisha katika levo ya timu ya taifa.

Kikosi cha La Furia Roja, ilikuwa ni moto wa kuotea mbali. Ilianza kwa kutoa dozi ya 1-0 kwa Wajerumani (2008), wakatwaa ndoo ya Euro, wakaendeleza moto katika michuano ya Kombe la Dunia (2010), kabla ya kutetea ubingwa wa Euro (2012). Nani angeweza kuwadhibiti vijana wa Vicente del Bosque?

Mwaka 2014, Hispania wakawasili nchini Brazil wakiwa ni moja ya mataifa yanayopigiwa upatu kutwaa Kombe la Dunia. Lakini tofauti na matarajio ya mashabiki wanaowahusudu, walikumbana na jinamizi linaloendelea kuwanyima raha mpaka sasa. Hawakuamini na bado hawaamini kilichotokea.

Mechi ya kwanza wakakumbana na Waholanzi. Xavi Alonso alipoanza kuifungia Hispania watu wakahisi shughuli itakuwa rahisi, kumbe Waholanzi walikuwa wanawaza tofauti. Zikiwa zimesalia dakika chache kipindi cha kwanza kimalizike, Robin Van Persie, alipiga kichwa cha kuchupa (flying header) na kuisawazishia timu yake.

Baada ya hapo shughuli nzito ikaanza na mwisho kilichowapata Hispania unakifahamu na kama hukujui basi angalia hapo juu.

REAL MADRID 5-0 BAYERN MUNICH

Klabu Bingwa Ulaya ni michuano mikubwa na ina heshima sana, ukiwakutanisha vigogo wa soka barani humo. Hii haimaanishi kuwa, michuano hii haina matukio ya kukatisha tamaa, kuna matukio kibao ya klabu kubwa kupokea vichapo vya mbwa mwizi.

Mwaka 2014, katika raundi ya kwanza, iliyopigwa Allianz Arena, Real Madrid iliitandika Bayern Munich, mabao 4-0 bila huruma, Unakumbuka?

Licha ya kuondoka na kichapo cha 1-0, cha kumshukuru Mungu, vigogo hao wa Ujerumani, walifanikiwa kukaza katika dimba la Santiago Bernabeu. Matokeo ya jumla yakawa ni 5-0! Hii ilikuwa ni kipigo cha aibu kuwahi kuikumba Bayern Munich bila kusahau bakora 4-0 walizopokea kutoka kwa Barcelona (2009).

Kipigo hiki kilikoleza rekodi mbaya ya Pep Guardiola katika michuano hii akiwa kama Kocha wa Bayern Munich. Mhispania huyu alipoteza mechi tatu za nusu fainali ya mashindano haya kwa mitatu mfululizo, dhidi ya Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid. Je, ataweza akiwa Man City?

STOKE CITY 6-1 LIVERPOOL

Msimu uliofuata baada ya Liverpool kukaribia kutwaa ubingwa wa KPL, ni moja ya misimu mibaya zaidi katika historia ya Majogoo hawa wekundu.

Mambo yalianza kwenda mrama punde baada ya kuondoka kwa Luis Suarez, aliyetimkia Barcelona huku Brendan Rogers akiwa hana hata wazo la kuwekeza katika warithi wake.

Siku chache baadaye, Nahodha Steven Gerrard naye akaamua kuhitimisha huduma zake pale Anfield, alipocheza mechi yake ya mwisho akiwa na jezi nyekundu, dhidi ya Stoke City katika dimba la Britannia. Tofauti na matarajio mechi hii ikachafua gazeti, Liverpool ikakumbana na kipigo cha kufa mtu.

Stoke iliitandika Liver 6-1, mabao matano yakipatikana katika kipindi cha kwanza huku bao pekee la kufutia machozi likifungwa na Gerrard mwenyewe tena katika dakika za lala salama. Mechi hii ikawa ni ya kwanza baada ya miaka 52, kwa Liverpool kuruhusu mabao matano kutikisa nyavu zao katika mechi moja.

Wanaanzaje kusahau kichapo, asikwambie mtu, tukio hili bado linamuuna ‘the fantastic Captain’ Steven Gerrard mpaka leo, atakosaje kuchukia wakati hii ndio ilikuwa funga dimba akiwa mchezaji wa Klabu aliyoitumikia kwa takribani maisha yake yote ya soka?

6. CHELSEA 6-0 ARSENAL

Hakuna kitu kilichokuwa kikimnyima usingizi Arsene Wenger kama kukutana na kikosi cha Jose Mourinho, kilichosheheni makamanda wa vita akiwemo kubwa la maadui, Didier Drogba.

Mfaransa huyu hajawahi kumfunga Mourinho kwenye mechi yoyote ya ligi kuu ya England, rekodi ambayo Mreno huyu mwenye kiburi na majivuno hasahau kutaja katika mikutano yake na waandishi wa habari.

Hata hivyo, vipigo vyote alivyovipata dhidi ya Chelsea havimuumi kama lile kimbunga la msimu 2013/14.

Ungemuona Babu Wenger mbona ungemuonea huruma, kipigo kile nusura kimpe kifafa kama sio kupooza.

Arsenal ilisafiri hadi Stamford Bridge kuikabili ‘The Blues’, huku wakiwa tayari wameshakata tamaa ya kuwepo katika mbio za ubingwa, kidonda chao kikatoneshwa zaidi na kipigo kutoka kwa kikosi cha kiburi huyu anayejiita Special One.

Arsenal walikuwa hawajielewi, hawajui wakabe au washambulie, ilikuwa ni balaa ila tukio la kuchekesha lilikuja baada ya Kieran Gibbs kuoneshwa kadi nyekundu badala ya Alex-Oxlade Chamberlain aliyezuia mpira uliopigwa na Eden Hazard kwa mkono.

5. BAYERN MUNICH 7-0 BARCELONA

Ubabe wa Barcelona kilichokuwa na kikosi hatari kilichoshindikana (2009 na 2011), ambacho kinadaiwa kuwa moja ya vikosi vya hatari kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka, chini ya uongozi wa Pep Guardiola, ulisitishwa kwa kipigo cha mbwa mwizi, mwaka 2012.

Licha ya ubora huu waliokuwa wakitukuzwa nao, Barcelona walikutana na Bayern Munich iliyojeruhiwa ikajeruhika vilivyo. Ilikutana na shughuli ya Arjen Robben na Frank Ribery, tambo zote zikabaki stori. Ilikuwa ni katika hatua ya Nusu fainali, ambapo vijana wa Pep Guardiola walipokula 7-0.

Robben na Ribery walihakikisha wanavuruga mipango yote ya Barcelona, vunjilia mbali mbwembwe za Xavi na Iniesta, huku Messi akiwekwa mfukoni na mwisho wa siku, katika dimba la Allianz Arena, watu wakajipigia 4-0 kabla ya mazishi yaliyofanyika rasmi Camp Nou, Barca akala 3-0, shughuli ikaisha.

4. BARCELONA 5-0 REAL MADRID

Kwa wale ambao hawana upnde wanaoushabikia, mechi za ‘Derby’ kama vile El Classico, huwa ni burudani tu, kwa wale ambao timu yao inashinda hujihisi ni kama wako peponi vile ila kwa wale wanaopokea kichapo sasa, Debi hizi huwa ni Jahanam kama sio jinamizi.

Historia inaitambua Real Madrid kama moja ya klabu hatari kwa kutembeza dozi za haja, lakini safari hii (Nov, 2010), Real Madrid, ikiwa chini ya Jose Mourinho, ambaye alikuwa anaongoza Los Blancos katika El Classico yake ya kwanza, ilisafiri hadi Camp Nou, na kukumbana na kipigo cha 5-0.

Licha ya kutofunga, Lionel Messi aliibuka shujaa wa mechi hiyo kwa kutoa ‘Assist’ tatu zilizozaa mabao. Huu ukawa ni mwanzo mbaya kwa Mourinho na mwanzo wa uhasama kati yake na Pep Guardiola.

3. MANCHESTER UNITED 8-2 ARSENAL

Dakika chache kabla pazia la usajili, mwaka 2011, Arsene Wenger alikuwa bize kufanya biashara kichaa iliyoshuhudia usajili wa wachezaji watano. Wengi watakuwa wanajiuliza ilikuwaje mpaka ukichaa huu wa ghafla, ukampanda Babu Wenger?

Mzee alipaniki balaa baada ya kushikishwa adabu na mzee mwenzake, Sir Alex Ferguson. Wenger aligundua hana wanaume wa kazi bali amejaza ‘watoto wa shule’ katika kikosi chake baada ya kupigwa 8-2 na Man United. Kipigo hiki kinawauma ‘The Gunners’, ukitaka ugomvi nao wakumbushe machungu ya mechi hii.

Kwanini Wenger asiamue kuingia sokoni wakati katika kikosi chake kilichokwaana na United kilikuwa na makinda tupu huku wazoefu wakiwa ni Robin Van Persie, Theo Walcott, Alex Song, Tomas Rosicky na Andriy Arshavin tu? Kibaya zaidi hata katika benchi hakukuwa na mchezaji mwenye jina.

2. MAN UNITED 1-6 MANCHESTER CITY

Sir Alex Ferguson alikuwa na muda mzuri katika kipindi chote alichohudumu kama kocha wa Man United, tajriba na heshima aliyoiweka pale Old Trafford haijawahi kuchafuliwa na yeyote na ndio maana mpaka sasa mashetani wekundu wanahaha kupata mrithi sahihi wa mikoba yake.

Hata hivyo, katika mambo ambayo mkongwe huyu atazidi kukumbuka ni udhalilishaji aliyofanyiwa na mahasimu wakubwa wa Man United katika Jiji la Manchester, Man City. Timu zote ziliingia katika dimba la Old Trafford, zikiwa katika fomu, Man United kama kawaida wakaanza na mchecheto kabla ya kuzimwa na Yaya Toure na wenzake.

Kipindi cha pili mchezaji mmoja wa Man United akatolewa nje kwa nyekundu ikawa ndio kiyama chao, City wakaanza kujipigia tu ambapo mabao matatu kati ya mabo sita walizofunga siku hiyo, zilipatika ndani ya dakika 10 za mwisho.

1. BRAZIL 1-7 GERMANY

Bila ubishi hakuna tukio lolote la aibu lililowahi kutokea katika soka la kimataifa katika miongo yote iliyopita achilia mbali karne, kama hili la Brazil kutandikwa 7-1 na Wajerumani wale wenye roho mbaya.

Mechi hii haihitaji utambulisho wala kibwagizo chochote, ilikuwa ni dhahama ambayo daima itabaki kuwa kovu nyeusi ya maumivu katika historia ya soka la Brazil, unategemea vipi Wabrazil walisahau tukio hili wakati lilitokea mbele ya macho yao, tena katika ardhi ya nyumbani kwao?

Ilikuwa ni michuano ya Kombe la Dunia, mwaka 2014, iliyofanyika nchini Brazil. ‘Samba Boys’ kama wanavyofahamika, chini ya Captain Dunga, kilianza michuano kwa kusuasua huku ikiimarika kila hatua kabla ya kukutana na rungu la Ujerumani katika hatua ya Nusu fainali.

Kibaya zaidi ni kwamba, mshambuliaji wao Neymar na beki wa kati, nahodha Thiago Silva hawakuwepo katika mechi hii.

Majanga hayo yaliyowakumbuka usiku ule, umekuwa ni  kumbukumbu mbaya lisilofutika katika akili za mashabiki waliojazana kushuhudia udhalilishaji katika dimba la Bela Horizonte.

Wakiwa wanamkosa nahodha na kiongozi wao, Thiago Silva, jahazi likayumba vibaya mno.

Ujerumani ikaiduwaza dunia kwa kufunga mabao matano ndani ya dakika kati ya 10-15, ya kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza mengine mawili katika kipindi cha pili na kuvuruga ndoto za Brazil za kutwaa kombe la dunia baada ya kulokosa ndani ya kipindi cha miaka 12.