Usibishe, huyu ndiye mkali

MBWANA SAMATTA

Muktasari:

  • Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa ambao, wamekuwa wakipigiwa utapu kuwa wanastahili tuzo ya kuwa mkali wa soka la Bongo kwa nyakati zote;

PENGINE unajiuliza kuwa ni mchezaji gani katika vizazi vyote kwenye soka la Tanzania anayestahili kuwa Mwanasoka Bora wa nyakati zote? Achilia mbali rekodi kubwa zinazoshikiliwa na baadhi ya wanasoka kama Abdallah Kibandeni staa pekee aliyewahi kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika mechi za watani wa jadi Simba na Yanga, akifanya hivyo Julai 19, 1977.

Achana na rekodi ya Omar Hussein kuwa mfungaji wa muda wote wa watani wa jadi nchini akifunga mabao sita, wala usiiweke rekodi nyingine kama ile ya Juma Kaseja, Iddi Pazi na Ally Mustafa ‘Barthez’ kufunga mabao katika mechi za Ligi Kuu na kuwa nyota pekee waliofanikiwa kufanya hivyo.

Hapa tujadiliane kwa kina nani anapaswa kuwa Mwanasoka Bora wa nyakati zote nchini? Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa ambao, wamekuwa wakipigiwa utapu kuwa wanastahili tuzo ya kuwa mkali wa soka la Bongo kwa nyakati zote;

Sunday Manara

Wadau wa soka walipenda kumuita Kompyuta (Computer) kutokana na soka lake ambalo kwa wakati huo lilionekana kuwa la miujiza kama ilivyo kwa  kifaa hicho cha kielektroniki.

Manara alikuwa na kipaji halisi cha soka. Kuna wakati aliufanya mpira kuwa kama kitu chepesi kwa kipaji alichokuwa nacho.

Staa huyo alitamba na Yanga katika miaka ya 1970 kabla ya kutimkia nchini Uholanzi ambako aliichezea timu ya Heracles na baadaye akaenda Marekani ambako alijiunga na New York Eagles na kisha Australia ambako alikwenda kucheza soka la kulipwa pia katika klabu ya Australian kabla ya kwenda Dubai katika klabu ya Al Nasri.

Mshambuliaji huyo alikuwa nyota wa kwanza wa Tanzania kuweza kucheza soka la kulipwa Ulaya jambo ambalo kwa miaka hiyo lilionekana kama ndoto kabisa.

Watu waliomuona Manara katika enzi zake wanadai Tanzania haijapata kuwa na nyota tishio kama yeye japo nyakati zinaonekana kutaka kubadilika sasa.

Peter Tino

Bao lake la kusawazisha dhidi ya Zambia katika mchezo wa marudiano wa kufuzu kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika pale Ndola, Zambia Agosti 26, 1979 ndilo liliipeleka Taifa Stars kwenye mashindano hayo mwaka 1980, mchezo wa awali hapa Bongo, Stars ilishinda kwa bao 1-0 mfungaji akiwa Mohammed ‘Adolph’ Rishard.

Peter Tino anatajwa kuwa miongoni mwa mastraika waliokuwa na uwezo mkubwa uwanjani ambapo, kuna wakati alipiga chenga wachezaji sita wa timu pinzani na kwenda kufunga.

Mafanikio yake na Taifa Stars, Yanga na Pan Africans yanamfanya Tino kuwa miongoni mwa vizazi vya dhahabu kwenye soka la Tanzania.

Duru zinaeleza kuwa kama sio jitihada binafsi za staa huyo katika mchezo wa marudiano kule Zambia, Stars isingekuwa imeshiriki Afcon mpaka sasa.

Edibily Lunyamila

Winga Edibily Lunyamila na kimo chake cha wastani,  upole wake na mwili wake kama alivyo, muone hivyo hivyo tu kama alivyo. Lunyamila ni miongoni mwa nyota wachache wa Tanzania ambao, walikuwa na vipaji halisi. Nyota huyo alikuwa na uwezo wa kuichambua timu pinzani kwa kadiri alivyojisikia.

Alikuwa na uwezo wa kufunga kwa kadiri alivyojisikia, kuna siku aliifunga timu ya RTC Kagera mabao sita peke yake wakati Yanga ikishinda kwa mabao 8-0. Nani anaweza kufanya hivyo?

Mwaka 1993 Lunyamila aliwashangaza Waganda baada ya kupiga mpira mwingi na kuisaida Yanga kuondoka na Kombe la Kagame nchini humo. Yanga iliifunga SC Villa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali ambapo Lunyamila alifunga moja na jingine likifungwa na marehemu Said Mwamba ‘Kizota’.

Alirudi tena mwaka 1999 na kufanya hivyo kiasi kwamba raia wa nchi waliandika jina la nyota huyo kwenye magari na migahawa yao. Nani aliyewahi kufanya hiyo? Hakuna ila ni Lunyamila tu!

Mrisho Ngassa

Winga mwingine mkali, Mrisho Ngassa anabaki kama alivyo lakini ni miongoni mwa vipaji vichache vya soka kuwahi kutokea nchini. Pengine angekuwa na utulivu angewahi kufika Ulaya kabla ya Mbwana Samatta.

Mwaka 2009 Ngassa alikwenda kufanya majaribio katika klabu ya West Ham  United ya Ligi Kuu England. Ni staa gani wa Tanzania amewahi kupata nafasi hiyo? Ngassa katika ubora wake alikuwa na uwezo wa kufanya anachojisikia uwanjani.

Alikuwa na uwezo wa kumchukua mtu kisha akamchukua tena na kwenda kufunga. Alibebwa na kimo chake kama ilivyo kwa Lionel Messi.

Staa huyu ndiye aliyeibeba Stars kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (Chan) mwaka 2009. Ngassa ndiye aliyeibeba Stars kwenye michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2012.

Rekodi kadhaa kama kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL 2009/10, Mfungaji Bora wa VPL 2010/11, Mfungaji Bora Kombe la Chalenji 2009 na kuwa Mfungaji Bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika 2014, zinamfanya awe mchezaji wa daraja la tofauti nchini.

Mbwana Samatta

Wakongo wanamuita Samagol. Watu wa Mbagala wanamuita Popa, lakini Wazungu pale Ulaya wanamuita Samantha. Hii ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupachika mabao.

Pale Genk tangu ametia maguu mwezi wa Februari, mwaka huu tayari amefunga mabao 10 ambapo sita ni katika mechi za mashindano na manne katika mechi za kirafiki.

Staa huyu kama asingekuwa amezaliwa hapo Mbagala na ushahidi kuonekana pengine Wakenya tayari wangeshaanza kusema ana chimbuko na nchi yao kama wanavyodai kuwa Mlima Kilimanjaro uko kwao.

Samatta amejizolea umaarufu mkubwa kutokana uwezo wake mkubwa wa kuliona goli.

Mapema mwaka huu alitangazwa kuwa Mchezaji Bora Afrika kwa nyota wanaocheza barani hapa, siku chache baadaye akajiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.

Samatta aliibuka pia Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana ambapo, pia alitwaa taji hilo na TP Mazembe sambamba na staa mwenzie Thomas Ulimwengu na kuwa Watanzania pekee wenye medali hizo.

Kwa sasa Samatta ndiye nahodha wa Taifa Stars inayonolewa na Boniface Mkwasa ‘Master’. Hata hivyo, katika timu ya taifa bado hajawa na mafanikio makubwa ya kujivunia.