Usajili umeiangusha Azam FC msimu huu

Tuesday May 9 2017

 

By Gift Macha na Charles Abel

KATIKA toleo la jana Jumatatu tuliona sehemu ya kwanza ya mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Azam, Nassoro Idrissa ‘Father’ ambaye alipandishwa kushika kiti hicho mwishoni mwa mwaka jana.

Katika sehemu hiyo ya kwanza, Father alieleza namna walivyoamua kuachana na Kocha Stewart Hall pamoja na kwamba aliwapa mafanikio makubwa.

Kiongozi huyo alieleza namna pia walivyomleta kocha raia wa Hispania, Zeben Hernandez na walivyotofautiana katika baadhi ya mambo na kuamua kupeana mkono wa kwaheri.

Leo tunaendelea na mwendelezo wa mahojiano hayo maalumu yaliyozaa makala haya ambapo, Father anaendelea kueleza mambo kadhaa ambayo yanaendelea

katika klabu hiyo. Endelea naye...!

Usajili ni tatizo

Father anaelezea namna ambavyo usajili umekuwa tatizo kubwa katika timu yao kiasi kwamba sasa wameamua kujikita zaidi katika timu yao ya vijana.

“Usajili ni miongoni mwa kazi ngumu sana kwenye soka, kwanza ni bahati nasibu kwani unaweza kumsajili mchezaji mzuri, lakini bado akashindwa kufanya vizuri. Imetokea siyo kwetu tu bali hata kwenye timu nyingine.

“Mfano wakati tunamtazama Kipre Tchetche akiwa na timu ya taifa ya Ivory Coast hapa nchini (mwaka 2010) tuliona namna alivyokuwa na uwezo mkubwa. Baadaye tulikwenda kwao na kumsajili, lakini alipokuja hapa msimu wake wa kwanza ulikuwa tatizo,” anasema.

“Tulikwenda kucheza Tanga watu wakatucheka na kusema pengine tumeuziwa yule pacha wake (Kipre Bolou), lakini baadaye alifanikiwa kutulia na kuwa mshambuliaji hatari.

“Kuna mchezaji anaitwa Ismail Diara, alisajiliwa hapa kwetu lakini baada ya muda tukawa tunajiuliza, hivi ni kweli tulimtazama huyu mchezaji kabla ya kumsajili? Alikuwa na kiwango kibovu sana. Ajabu ni kwamba baada ya kuondoka hapa kwetu amekuwa mshambuliaji hatari huko Rwanda, anacheza Rayon Sports.”

Hata Chelsea ilichemka

Father anasema katika usajili wamejaribu kutumia njia mbalimbali ili kuhakikisha wanapata wachezaji mahiri, lakini bado imekuwa ni tatizo kubwa japo sio kwao tu bali hata kwa timu nyingine duniani.

“Unaweza kuona hata Chelsea iliwahi kumsajili Fernando Torres akiwa katika kiwango cha juu, lakini alishindwa kutamba. Waliwahi pia kumsajili Andriy Shevchenko lakini akashindwa kufikia ubora aliokuwa nao awali,” anasema.

“Kwa hapa kwetu tumejaribu kufanya skautini (scouting), tukatumia mawakala na pia wakati mwingine kuwaleta wachezaji hapa wafanye majaribio, ila bado imekuwa ni changamoto kubwa kupata wanaofiti moja kwa moja.

“Kwa sasa tumefanya tathmini na kubaini kwamba wachezaji wenye msaada mkubwa kwenye timu yetu wametoka katika timu ya vijana.

“Unaweza kuona wachezaji kama Aishi Manula, Gadiel Michael, Himid Mao, Mudathir Yahya na Shaaban Idd wamekuwa wazuri, kwa sasa tutawekeza zaidi huko.

“Kwa msimu ujao kuna wachezaji kama wanne kutoka katika timu yetu ya vijana ambao tumeona tuanze nao hao kwa kuwapa nafasi kwenye timu, pengine njia hii inaweza kutusaidia zaidi kuliko kuzunguka huku na kule.”

Simba na Yanga

Miongoni mwa mambo yaliyoipa sifa kubwa Azam ni kuweza kuzitikisa Simba na Yanga kwa kuchomoa nyota muhimu wa klabu hizo, ila kwa sasa wamekubaliana kwa kauli moja kuwa hawatachukua tena wachezaji kutoka timu hizo.

“Awali tulikuwa na kiu kubwa ya kuona timu yetu inakwenda mbali kwa haraka. Tulitazama namna ya kufanya na ni kama tulikuwa na kasi zaidi. Hii ndiyo sababu tuliamua kumsajili mchezaji kama Mrisho Ngassa kutoka Yanga,” anatoa siri.

“Unaweza kuona baadaye tulifanya tena usajili wa Frank Domayo na Didier Kavumbagu kutoka Yanga. Kwa kweli hii imetuletea shida kubwa na sasa tumeona ni vyema tukaachana na utaratibu huo,.

“Unajua katika soka la Tanzania Simba na Yanga ndiyo zimelishika zaidi. Unapokuwa unashindana na timu hizi siyo jambo jema kutengeneza uadui nao, hivyo ni busara tukawaacha wafanye mambo yao nasi tufanye yetu.

“Unapomsajili mchezaji kutoka Yanga ama Simba unakuwa siyo tu umetengeneza uadui na viongozi wa timu hizo, hapana. Unakuwa umetengeneza uadui na Watanzania wengi na hata ukienda mikoani watu wanakuwa na chuki na wewe.”

Mzigo mzito

Father anasema kutokana na uimara wa Simba na Yanga, ni vigumu kushindana nao hasa katika zama hizi ambazo timu nyingine zote zimewaachia mzigo huo.

“Ukitazama soka la Tanzania utaona Simba na Yanga ndiyo timu zenye malengo ya ubingwa, ukiachana nao labda utaizungumza na Azam. Timu nyingine zote zinashiriki Ligi ili ziendelee kuwepo na siyo kwa nia ya kutwaa ubingwa.

“Unaweza kuona nje ya hizo timu mbili tumebaki wenyewe tu, wenye nia ya ubingwa. Kuzipiku Simba na Yanga kutwaa ubingwa inakuwa siyo kazi ndogo na ndiyo maana unaona tunapata changamoto nyingi,” anaeleza.

“Tunapata moyo kuona timu kama Singida United inaonyesha nia kama ya kushindania ubingwa, pengine hili linaweza kuwa sehemu ya mabadiliko. Lakini siyo Singida tu, tungependa kuona timu zenye nia ya ubingwa zinaongezeka na kuwa nyingi zaidi.

“Unafikiri hizi timu nyingine ni kwamba haziwezi kutwaa ubingwa? Zinaweza, ila ni kama wachezaji na viongozi wao watakuwa na nia.

“Mbona wanaweza kuzifunga Simba na Yanga? Tatizo ni kwamba wakicheza na timu nyingine hawachezi kwa ushindani mkubwa kama wanavyofanya pindi wakikutana na Simba na Yanga ama Azam,.

“Ni jambo la aibu kwamba katika wachezaji zaidi ya 450 wa timu za Ligi Kuu, ni wachezaji wasiozidi 90 tu ambao wanawaza kutwaa ubingwa.

“Tunatengeneza ligi mbovu wenyewe kutokana na mfumo ambao siyo rafiki kwa timu hizi pamoja na wachezaji ambao hawana kiu ya mafanikio. Ni vyema tukabadilisha hili.”

Unajua Father amezungumza kitu gani kuhusu straika wa Simba Ibrahim Ajib na Kocha Joseph Omog? Je unajua kwanini wamekuwa hawafanyi vizuri katika mashindano ya kimataifa? Usikose kusoma hitimisho la mahojiano haya na Father keshokutwa Alhamisi.