Umefika wakati wa Arsene Wenger kuondoka Arsenal?

Muktasari:

Hii ni klabu inayopendwa na wengi ndani na nje ya England, ikipata mafanikio hapa na pale.

MWISHONI mwa Januari na mwanzoni mwa Februari hakijawa kipindi kizuri kwa Arsenal.

Hii ni klabu inayopendwa na wengi ndani na nje ya England, ikipata mafanikio hapa na pale.

Hata hivyo, wanapotarajiwa kufanya vyema huenda tofauti, hivyo kuwachanganya wadau, hata wale wasiokuwa mashabiki wao.

Ni miaka takriban 20 sasa wamekuwa chini ya meneja Arsene Wenger, lakini umepita muda mrefu mno bila ya kutwaa taji la England.

Walijifariji kwa Kombe la FA misimu miwili mfululizo kabla ya kupokwa msimu uliopita.

Ni kweli wamekuwa wakifuzu kwa nafasi nne bora miaka mingi sasa katika Ligi Kuu ya England (EPL) na kusonga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini nako huwa wanaishia mapema sana njiani.

Msimu huu walionekana kwamba ni washindani EPL, wakaenda vyema na kupita msimu wa sikukuu wakiwa wazuri, lakini vikwazo vikaanza, wakati watu wakishangaa jinsi vilivyochelewa.

Wamekuwa wakipata majeruhi mara kwa mara, lakini hata wasipokuwa nao, mechi ambazo ungetarajia washinde kirahisi wanaishia kupigwa, tena hata kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Emirates. Mashabiki walishapata kutoa mabango kutaka Wenger aondoke, lakini wakishafungwa halafu wakaja kushinda mechi nyingine, wanamwona mfalme, naye amekuwa kana kwamba hana wazo la kuondoka.

Mwenye hisa nyingi klabuni hapo, Mmarekani Stan Kroenke anaelekea kumuanini sana Wenger na aliwahi kusema kuwa hakuinunua klabu hiyo kwa ajili ya kutwaa vikombe.

Yeye yupo kibiashara zaidi, lakini ni wazi mwekezaji yeyote, kama Roman Abramovich wa Chelsea na Fahard Moshiri wa Everton wangependa walau siku moja kuona kombe linaingia nyumbani kwao.

Ya nini timusiyochukua taji? Ni kama vyama vya siasa; lengo lao ni kushika dola na itashangaza kama kuna chama cha siasa kisicho na lengo hilo. Mwenendo wa Arsenal umeanza kutia shaka, hata kama tunavyozungumza wapo ndani ya nne bora. Ilikuwa ni kituko waliposambaratishwa na Watford hapo Emirates, mashabiki walitarajia ilikuwa mechi ambayo wangejipatia ushindi wa mabao mengi. Haikuwa hivyo.

Mbaya zaidi ilikuwa mechi moja kabla ya kukabiliana na Chelsea wanaoongoza ligi sasa kwa pointi 59.

Kisaikolojia ni wazi wangeingia mchezoni Jumamosi iliyopita wakiwa wamenyong’onyea na ndivyo ilivyokuwa, wakapigwa 3-1.

Wapo wanaojipotezea kwamba Chelsea walisawazisha tu kwa sababu Arsenal hapo Emirates waliwafunga kwa idadi hiyo ya mabao, lakini iwe iwavyo,

Arsenal wapo nyuma kwa pointi 12 na kufikiria kwamba watawakamata Chelsea kwa kweli si kitu rahisi. Kuna mechi za kupoteza, za kwenda sare, kuumia wachezaji lakini pia Chelsea nao si kwamba watapoteza pointi zote hizo, maana wapo vyema.

Kifupi miaka imekwenda na halionekani jipya kwa Wenger na timu yake, lengo lao si vikombe bali kuwa na timu tu inayoingiza fedha; na kweli kama ni fedha inaingiza.

Naamini ni wakati sasa wa Wenger kutafakari hatma yake, kuona ikiwa kuna haja ya kuimarisha kikosi, benchi la ufundi au yeye kufikiria vinginevyo, ikizingatiwa mkataba wake unaelekea ukingoni.

Wachezaji wazuri anao, tena wapo vijana kwa wakongwe na hawezi kusingizia kuumia mtu muhimu, Santi Cazorla ndiyo tatizo lote hili. Amekuwa Arsenal tangu 1996, ana miaka 67 akiwa kocha anayeongoza kukaa klabu moja muda mrefu hivi sasa, lakini mkataba wake unamalizika kiangazi kijacho.

Walitwaa taji mara ya mwisho 2004 lakini ukweli mashabiki wao wana roho ngumu, hawawaachi, wanateseka na kwenda nao mbele. Ni kipindi kigumu sana kwa Arsenal na Wenger wao na itawafaa tu iwapo kisaikolojia watarejea vizuri kwa sababu vinginevyo wanaweza kuendelea kuoga mabao. Ni wakati pia wa wamiliki kuanza kufikiria juu ya mrithi wa Wenger, isije kuwa kama Man United ambao hadi leo bado hawajatulia tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson.

Ujio wa David Moyes ulikuwa jinamizi na kuondoka kwake kabla hata ya mwaka mmoja na kuingia Louis van Gaal hakufaa kitu na sasa Jose Mourinho aelekea kucheza kamari, japo wachezaji wanaanza kuzoeana.

Arsenal wana cha kujifunza na wangejifunza mapema na kufanya uamuzi kabla muda haujaenda zaidi na kuharibikiwa, ikiwa kweli nia yao ni soka na ubingwa.