Ufupi wao ndio utamu wao

Monday March 13 2017'TSHABALALA'

'TSHABALALA' 

By MWANAHIBA RICHARD

WAKATI mwingine unaweza kuwachukulia poa. Wana miili midogo. Wakisimama na mabeki wenye miili nyumba kama Vincent Bossou ama Method Mwanjali, unaweza kujiaminisha hawataweza kufurukuta kabisa.

Hata hivyo, kama unawachukulia hivyo, umeumia. Jamaa wanateleza kama kambare na wamekuwa wakiwatesa mabeki wa timu pinzani kwa kasi na usumbufu wao, licha ya kuwa na maumbile hayo.

Wataalamu wa soka wanasema wachezaji wafupi na wenye miili midogo wako fiti sana kukipiga katika nafasi za mabeki wa pembeni na winga kwa kuwa miili yao inawapa uhuru mkubwa wa unyumbulifu na uwezo wa kuchanganya miguu kwa haraka.

Kweli? Katika kuthibitisha hilo, Mwanaspoti limetupia jicho katika soka la Ligi Kuu Bara kwa kuwaangalia nyota kadhaa waliotamba katika nafasi za beki wa pembeni na winga katika timu na miaka mbalimbali na kubaini ukweli fulani.

Wafuatao ni baadhi tu ya wachezaji wenye maumbo hayo madogo lakini wamekuwa na msaada mkubwa kwenye timu zao wakicheza nafasi hizo za pembeni.

Ngassa/Msuva/Kichuya

Kwa sasa Mrisho Ngassa anaichezea Mbeya City baada ya kushindwa kumudu maisha Uarabuni alikokuwa akiichezea Fanja FC. Ngassa ana kipaji, mbunifu na anajituma.

Aliwahi kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akiwa Azam FC, alitamba pia na Yanga na Taifa Stars kabla ya kwenda Afrika Kusini. Jamaa ni mfupi lakini balaa.

Katika kikosi cha sasa cha Yanga, anayeweza kufananishwa naye kwa asilimia fulani ni winga Simon Msuva.

Mmoja wa makocha maarufu wa soka nchini, Joseph Kanakamfumu, anasema: “Tanzania huwa hatuangalii mchezaji wa pembeni awe na umbo gani, lakini mara nyingi anayecheza winga au beki wa pembeni anapaswa kuwa mnyumbulifu na anayechanganya miguu kwa haraka, wachezaji wengi wafupi wana sifa hizo. Angalia alivyo winga wa Simba, Shiza Kichuya, pale ndiyo mahala pake.

“Ngassa na Kichuya wana vipaji, wabunifu na wanaweza kubadilisha mchezo muda wowote, Msuva anapaswa kuongeza mazoezi ili kuwa kwenye kiwango cha juu.”

Tshabalala/Mwasapili/Baba Ubaya/Kessy

Hawa ni mabeki wa pembeni na wote wana maumbo madogo, lakini shughuli yao ni kubwa. Wasumbufu wawapo na mpira au wanapousaka, wana kasi na wanageuka kwa haraka. Si sawa na mabeki warefu.

Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliposajiliwa Simba alimnyang’anya namba Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ambaye sasa yupo Mtibwa Sugar, japo Baba Ubaya alizidiwa kete kutokana na hali yake ya majeraha.

Tshabalala ana namba ya kudumu Simba na unaweza kusema amejenga kibanda kabisa.

Ramadhan Kessy yupo Yanga anafanya mambo. Alifanya mambo pia Simba alikotua akitokea Mtibwa, anaimudu mno nafasi yake kiasi hawezi kulala njaa.

Hali ni hivyo kwa Hassan Mwasapili, beki wa kulia wa Mbeya City, yupo na kikosi hicho tangu kilipokuwa Daraja la Kwanza, bahati mbaya kwa sasa ni majeruhi, lakini ni wazi akipona ataendelea kukimbiza kama kawa.

SMG

Winga mzoefu, Said Maulid ‘SMG’ kwa sasa yupo Angola. Kimo chake kifupi hakikuwa kizuizi cha kutamba Simba, Yanga, Taifa Stars na sasa yupo Angola anakozidi kukimbiza.

Jamaa anakipiga soka la juu tangu mwaka 1995.

Kuhama kwake katika timu ni kufuata masilahi, si kushuka kiwango.

Shomary Kapombe/Shadrack Nsajigwa

Kapombe anaichezea Azam, lakini Nsajigwa tayari amestaafu soka baada ya kuichezea Yanga kwa kipindi kirefu. Wawili hao wameichezea Taifa Stars.

Ingawa wameingia kwenye soka la ushindani kwa nyakati tofauti, lakini wote walianzia nafasi ya winga kabla ya makocha wao kuwabadili na kuwa mabeki wa pembeni. Kila mmoja akabamba kweli kweli.

“Nafasi nyingine nimecheza pia, lakini huku pembeni nilikuwa mahiri zaidi katika kutimiza majukumu kwa mujibu wa maelekezo ya kocha,” anasema Nsajigwa.

“Winga ni rahisi kuchezeshwa beki wa pembeni kwa sababu anakuwa na uwezo mkubwa wa kupanda na kushuka kwa haraka, anakaba na kushambulia kwa urahisi, ndizo sifa za mawinga na mabeki wa pembeni.”

Mwambusi aunga mkono

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi anakiri kuwa wachezaji wafupi ni mahari mno katika nafasi hizo za pembeni akisema wengi wao wanamudu kasi kutokana na vimo vyao.

“Ni wepesi wa kufanya lolote na hiyo ndiyo sifa kubwa ya beki wa pembeni au winga,” anasema.