Tajiri:Singida Utd bingwa

Muktasari:

Mwandami ambaye hafahamiki miongoni mwa wadau wa wa soka nchini, anasema itaitwa Singida United FC Limited na wameanza mazungumzo na kampuni kubwa duniani zinazotengeneza vifaa vya michezo, lengo likiwa kupata vifaa bora pamoja na kuwa wakala na mambo yakikaa sawa Puma huenda ikawa ya kwanza.

TAJIRI wa Singida United, Yusuph Mwandami, ametangaza rasmi kuwa timu hiyo mpya Ligi Kuu Bara msimu ujao, imekuwa kampuni na ameziambia Simba na Yanga kwamba habahatishi.

Mwandami ambaye hafahamiki miongoni mwa wadau wa wa soka nchini, anasema itaitwa Singida United FC Limited na wameanza mazungumzo na kampuni kubwa duniani zinazotengeneza vifaa vya michezo, lengo likiwa kupata vifaa bora pamoja na kuwa wakala na mambo yakikaa sawa Puma huenda ikawa ya kwanza.

Ameenda mbali kwa kusisitiza kwamba wanataka kujiimarisha kiuchumi kupitia vyanzo vyake mbalimbali na fedha watakazozipata kwenye udhamini wa Vodacom, Azam TV na wadhamini wengine wa ligi wazitumie kuzizungusha kufanya biashara ambazo itafanya kampuni iimarike zaidi na timu itishe.

Lakini pia amewaambia mashabiki kuwa timu hiyo itaingia na moto kwenye ligi ili kuhakikisha kuwa mwezi mmoja kabla ya ligi kumalizika, wanatangazwa mabingwa.

 

KAMPUNI

“Tutakuwa na maduka ya wakala wa Kampuni ya Puma hapa kwetu Tanzania. Tukifanikiwa, tutafungua maduka Kanda ya Kati na mikoa mingine ikiwamo Mwanza,” alifafanua mkurugenzi huyo huku akiongeza wako kwenye mpango na wanasheria wao kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kuanza kuuza hisa za Kampuni ya Singida United FC Limited.

“Kampuni itakapokuwa na wachezaji wazuri, itaharakisha biashara ya kuuza hisa. Hisa zetu zitakuwa katika mtindo unaofanana na wa Vodacom. Kiasi chochote cha fedha hata shilingi mia, zitapokewa. Ni matarajio yetu kwamba itafika siku kampuni itakuwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe pamoja na kulipa mishahara ya wachezaji na viongozi wa kampuni,”alisema.

Anasisitiza kwamba hawataiga utamaduni wa timu za Simba na Yanga wa kutembeza bakuli, kila msimu wa usajili unapofika. Lengo ni Kampuni ya Singida United FC Ltd itengeneza fedha kwa ajili ya kijigharimia.

 

USAJILI

Mwandami anasema kwa sasa bado hawajaanza rasmi kusajili wachezaji, kinachofanyika ni makubaliano ya awali na hasa kwa wachezaji kutoka nje ya nchi na wameshamalizana na wawili kutoka Zimbabwe na watasajili wageni saba wa maana. Usajili wa ndani utaanza baada ya Ligi Kuu kumalizika.

“Ukianza usajili wa sasa kwa wachezaji wa ndani ya nchi wakati Ligi Kuu inaendelea, utaleta vurugu. Ukisajili mchezaji na timu yake inashiriki ligi, hataichezea timu yake vizuri,”anasema mmiliki huyo.

Hata hivyo, wanadhamiria kuendelea na wachezaji wengi waliopandisha timu ambao wako kwenye kiwango kizuri, kuna mapengo machache ndio yatazibwa usajili wao hautajikita kwa wachezaji wenye majina makubwa, isipokuwa utazingatia vijana zaidi ambao watafanya kazi ili majina yao yawe makubwa kisoka.

Mkurugenzi huyo anasema kampuni yao haitakimbilia kusajili wachezaji wenye majina makubwa kwani wamebaini ni wasumbufu na makocha waliopo wana uzoefu na hali hiyo. Anasema watasajili chipukizi ambao watatumika kwa muda mrefu.

Mwandami anasema tayari wameisha kuandaa kikosi cha pili kitakachukuwa na vijana 60 wenye vipaji vyao. Wale watakaofanya vizuri watapandishwa kwenye kikosi cha kwanza lengo ni kampuni izalishe wachezaji wake na kusajili nje ya kampuni iwe kwa kiasi kidogo.

 

BENCHI NA KAMBI

Bosi huyo anasema benchi la ufundi litaongozwa na Kocha Mholanzi, Hans Pluijm na Fred Felix Minziro na Jumanne Chale. Makocha hao watasaidia kampuni hiyo kupata kocha bora wa makipa.

Anasema wanatarajia kuweka kambi jijini Mwanza, kupisha uboreshaji wa uwanja wa nyumbani wa Namfua na utakapokamilika watarejea Singida kwenye uwanja wao.

“Hapa niwatoe hofu wakazi wa Singida na mikoa jirani, kwamba timu yao itacheza michezo ya Ligi Kuu hapa hapa Singida,” aliongeza.

“Nimeahidiwa na CCM mkoa, kuwa uwanja utakamilika kabla ya ligi haijaanza msimu ujao, sisi pia tutaweka nguvu zetu kusaidia ukarabati huo.”

Anasema wakati wowote watakaa kikao kwa ajili ya kutengeneza bajeti itakayokidhi mahitaji ya msimu mzima. Bajeti hiyo itatumika pia kugharamia usajili na uendeshaji wa timu.

 

WAWEZESHAJI

Anasema mbali ya yeye ambaye ni Mkurugenzi Mkuu na mmiliki, anapata sapoti kubwa ya Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.

Bosi huyo anasema wadau mbalimbali na makampuni wameonyesha nia ya kusaidia timu na wataandaa mikataba maalumu ya makubaliano ya uendeshaji baina yao na makampuni hayo.

 

SIMBA NA YANGA

“Hizi timu siyo kubwa kama inavyodaiwa.Simba na Yanga ni timu za kawaida kabisa, sema tu zina umri mkubwa kuliko timu nyingine zitakazozishiriki Ligi Kuu,” alisema.

“Ukitaka kujua si timu kubwa angalia ushiriki wa Simba na Yanga kwenye mashindano ya makombe ya Afrika. Miaka yote huwa zinatolewa mapema, tena kwa aibu kubwa,” anasema kwa kejeli huku akisema wanataka kufanya ilichofanya Leicester City England msimu uliopita.

“Kwa usajili utakaofanyika na walimu wazuri tulionao, timu itatoa burudani ya aina yake. Safari hii hatuendi Ligi Kuu kuchungulia, tunaenda kupambana kikamilifu.

“Kabla Ligi haijamalizika msimu ujao mwezi Aprili mwakani, Watanzania watajua lengo letu ambalo ni kubeba ndoo mapema kabisa.

“Tukifanikiwa kunyakua kombe, kitendo hicho kitakuwa chachu tosha kwa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu Tabora, Dodoma, Manyara na Arusha na yenyewe itapata hamu kuwa na timu za Ligi Kuu,” anasema huku akiahidi burudani ambayo haijawahi kuonekana miaka kumi na tano iliyopita.

 

KUBEBWA

“Kuna kila dalili Simba na Yanga hubebwa kuanzia kuandaa ratiba ya ligi msimu mzima. Baadhi ya viongozi kutokana na mapenzi yao binafsi, hata kabla ligi haijaanza wanaanza kuzitabiria ubingwa timu hizo za Dar es Salaam, si haki hata kidogo.

“Mimi niwaombe waamuzi watakaochanguliwa kuchezesha mechi za Ligi Kuu msimu ujao, wazione Simba na Yanga kuwa zipo sawa na timu nyingine zitakazocheza ligi hiyo.

“Wakifanya hivyo atapatikana bingwa halali ambaye kwenye mashindano ya kimataifa ataleta ushindani wa kweli,” anasema.

Anaongeza kuwa kwa vile timu yake ni kampuni, haitakufa itaendelea kuwepo na kama itakufa, itakuwa ni makubaliano ya hao wanahisa watakaoingia lakini yeye ataendelea.

 

YEYE NI NANI?

Mwandami ni mfanyabiashara maarufu wa madini Kanda ya Ziwa, mmiliki wa hoteli, pia mwanachama na kiongozi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Singida.