THIS IS YANGA BWANA

Muktasari:

Tambwe alikuwa akiungwa mkono na mashabiki wa Yanga kwa waliokuwa wakitamka maneno hayo baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto Africans uliowahakikishia kutwaa taji kwa mara ya tatu mfululizo, huku watani zao walikuwapo Uwanja wa Taifa, wakiishia kusonya.

       MSEMAJI wa Simba, Haji Manara hupenda kusema This is Simba Bwana!

Manara hutamka hivyo kila Simba inapofanya vizuri, lakini sasa jana Jumanne, Amissi Tambwe, alithibitisha ukweli wa msemo huo kwa kutamka ‘This is Yanga Bwana’ baada ya kuifungia bao timu yake na kuiwezesha kubeba taji la Ligi Kuu Bara kwa nyingine tena.

Tambwe alikuwa akiungwa mkono na mashabiki wa Yanga kwa waliokuwa wakitamka maneno hayo baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto Africans uliowahakikishia kutwaa taji kwa mara ya tatu mfululizo, huku watani zao walikuwapo Uwanja wa Taifa, wakiishia kusonya.

Mashabiki wa Simba walijitokeza uwanjani hapo ili kulishuhudia pambano hilo la kiporo na kupata mzuka baada ya kuona Toto ikikaza mwanzo mwisho na kuamini ngoma ingeishia hivyo na kuipa afueni timu yao kuelekea mechi ya kufungia msimu.

Toto ambayo sasa inasubiri miujiza tu kuepuka kushuka daraja katika mechi yao ya mwisho uwanjani itakapovaana na Mtibwa Sugar, ilionyesha soka la ushindani na kuinyima Yanga mabao kwa muda mrefu.

Jambo hilo liliwafanya mashabiki wa Simba kujisahau kwa muda na kuishangilia timu hiyo inayowasumbua kwenye mechi zao, kabla ya Tambwe kuunganisha vema krosi pasi iliyopigwa na beki Juma Abdul na kutua kichwani mwake.

Hilo lilikuwa bao la 11 kwa Tambwe msimu huu na lilitosha kuifanya Yanga kutangaza ubingwa kwa msimu huu, japo ligi inamalizika mwishoni mwa wiki hii. Yanga imefikisha pointi 68 na mabao 57 ya kufunga na kufungwa 13 hivyo kuwa na wastani nzuri dhidi ya watani zao waliopo nafasi ya pili na alama zao 65.

Ili Simba iweze kupindua matokeo ya ubingwa wa Yanga wikiendi hii ni lazima ishinde mechi yao na Mwadui si chini ya mabao 12, huku ikiombea Yanga ifungwe na Mbao zaidi ya bao 1-0.

Bao hilo la Tambwe aliyewahi kuchezea Simba kabla ya kutemwa kitatanishi misimu miwili iliyopita, iliwafanya mashabiki hao wa Wekundu wa Msimbazi kuishia kusonya kwa hasira na kuondoka uwanjani sura zimewashuka baada ya kubaini kuwa umeingia msimu wa tano bila timu yao kubeba taji hilo la Bara.

Yanga imetwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo na kuwa lao moja kwa moja huku wakiandikisha rekodi ya kulibeba taji la Ligi Kuu kwa mara ya 27 tangu ligi iliyoanzishwa rasmi mwaka 1965, ikiiacha Simba ikisaliwa na mataji 18.

Mtibwa Sugar inafuatia kwa kutwaa mataji mawili huku klabu za Cosmopolitan, Pan Africans na Azam zote za Dar es Salaam, Mseto ya Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya na Coastal Union za Tanga zikitwaa kila moja mara moja.

Katika mchezo wa jana uliochezeshwa vema na mwamuzi, Florentina Zablon, akisaidiwa na Abdallah Uhoka na Julius Kasitu, Yanga ilishindwa kuipenya ngome imara ya Toto iliyokuwa chini ya Ramadhani Malima na Yusuf Mlipili.

Mashambulizi mengi yaliyozalishwa na Yanga yalishindwa kutinga wavuni na kufanya mpaka mapumziko matokeo yawe 0-0, jambo lililowashutua mashabiki wa Yanga ambao wamezoea kuiona timu yao ikijipigia Toto itakavyo Uwanja wa Taifa.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha George Lwandamina kwa kumtoa Juma Mahadhi na kumwingiza Deus Kaseke, yaliifanya Yanga kupata uhai ingawa Toto bado iliendelea kukaza na kushambulia kwa kasi lango la wapinzani hao.

Ndipo shambulizi lililotokea pembeni kwa krosi iliyopigwa na Juma Abdul kutua kichwani mwa Tambwe na kuiandikia bao pekee, lililofanya kasi ya mashambulizi ya Yanga kuzidi maradufu japo hayakuweza kuisaidia kuandika bao jingine.

Mara baada ya pambano hilo kumalizika wachezaji wa Yanga walijimwaga uwanjani kushangilia ubingwa wao, huku wakiungwa mkono na mashabiki wao waliojazana majukwaani na wengi wao walikuwa wakiwakejeli watani zao Simba.

MITAANI SHANGWE

Huko mitaani nako mashabiki walikuwa wakiserebuka na kuwatania watani zao ambao wanaingia msimu wa tano wakitoka kapa bila ya taji tangu walipotwaa mara ya mwisho msimu wa 2011-2012.

Yanga wamepata jeuri ya kuwatania Simba kutokana na ukweli kwa muda mrefu wapinzani wao hao walikuwa wakiongoza ligi, lakini wakaja kupoteza kiulaini kwa Yanga na sasa wanasubiri kunyakua taji lao la kwanza kupitia Kombe la FA.

Simba itasafiri mpaka Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri, kuvaana na Mbao Jumapili ya Mei 28 na kama itashinda itapata nafasi kwa mara ya kwanza tangu 2013 kushiriki michuano ya kimataifa.

KESSY KAMA ZALI

Kitendo cha Yanga jana kutwaa taji hilo kimemfanya beki Hassan Kessy kuwazidi ujanja wachezaji wenzake aliokuwa nao Simba kwa kubeba taji katika kipindi kifupi tangu ajiunge Yanga sawa na ilivyo kwa kipa Beno Kakolanya.

Wakati huohuo, Yanga leo Jumatano inatarajia kusaini mkataba wake wa udhamini na SportPesa ambao unatajwa kuwa na thamani ya Sh950 kwa mwaka.

Mkataba huo unatarajiwa kuiokoa Yanga kutoka kwenye hali ngumu ya kiuchumi na unasainiwa siku chache baada ya Simba kusaini wa kwake na SportPesa pia ambao una thamani ya Sh888 kwa mwaka.