Sukari ya macho

Muktasari:

  • Kocha yeyote yule mwenye kiu ya mafanikio katika soka la sasa, ana ndoto ya kupata Kombinesheni nzuri yenye uwezo wa kufumania nyavu wakati wote na katika nafasi yoyote ile. Huu ni utatu ambao ni jinamizi kwa mabeki wengi wa ligi mbalimbali za Ulaya.

RAHA ya mechi bao, asikwambie mtu. Soka safi inahusisha mambo mengi ukianza na ufundi, burudani, mbwembwe na mambo kibao, yote tisa kumi, soka safi bila mabao, ni kazi bure!

Kocha yeyote yule mwenye kiu ya mafanikio katika soka la sasa, ana ndoto ya kupata Kombinesheni nzuri yenye uwezo wa kufumania nyavu wakati wote na katika nafasi yoyote ile. Huu ni utatu ambao ni jinamizi kwa mabeki wengi wa ligi mbalimbali za Ulaya.

Real Madrid inajivunia kuwa na BBC (Bale, Benzema na Cristiano Ronaldo) huku wapinzani wao kwenye La Liga Barcelona inajivunia kuwa na utatu unafahamika kwa jina la MSN (Messi, Neymar na Suarez).

Hata hivyo, si kombinesheni hizo tu za utatu matata wa washambuliaji unaotesa kwenye ligi mbalimbali za Ulaya, ukizitazama utazipenda tu. Ni sukari ya macho!

SADIO MANE, COUTINHO, DANIEL STURRIDGE (LIVERPOOL)

Licha ya kuanza vibaya katika kampeni yao msimu huu, Liverpool ina kila sababu ya kujiamini kuelekea ubingwa wa EPL, na hii inatokana na uwepo wa Sadio Mane, ambaye ni mmoja ya usajili unaotazamiwa kufanya makubwa, Coutinho na Daniel Sturridge. Huu ukiwa ni msimu wa kwanza kamili chini ya Kocha Mjerumani, Jurgen Klopp, Liverpool, inayoshika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi, ikiwa na pointi tatu baada ya mechi mbili, ina kila sababu ya kutegemea makubwa kutokana na uwepo wa Klopp pale Anfield. Maneno mengi yalisemwa baada ya Liverpool kuamua kuingia sokoni na kumchomoa Sadio Mane pale Southampton, kwa ada ya uhamisho ya Pauni 34, lakini kutokana na kasi, aina yake ya uchezaji, ni moja ya mambo ambayo inaifanya Liverpool kuwa na uhai katika eneo la ushambuliaji, kitu ambacho kimekuwa kikikosekana kwa muda mrefu. Mbali na Mane, mchezaji bora wa klabu, misimu ya hivi karibuni, Coutinho msimu huu ni dhahiri kuwa atakuja na moto mara mbili, kwa lengo la kutetea wadhifa wake kama mchezaji bora wa klabu, hadhi ambayo inamweka katika meza moja na magwiji kama vile Jamie Carragher na ‘Super Captain’ Steven Gerrard. Kiungo huyo mchezeshaji, raia wa Brazil, ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi, kusumbua mabeki na kujipenyeza, sifa ambazo zinampa nafasi straika Daniel Sturrige kufanya kile alichofundishwa kukifanya tangu akiwa mdogo, kufumani nyavu tu.

ANTOINE GRIEZMANN, KEVIN GAMEIRO, YANNICK CARRASCO (ATLETICO MADRID)

Swali kuu ambalo limetawala mijadala mingi katika mitandao ya kijamii kwa sasa ni je, Kevin Gameiro atakuwa straika mwingine atakayetisha katika kikosi cha Atletico Madrid? Jibu la swali hilo tunamwachia Diego Simeone na uongozi wa klabu hii kulijibu.

Msimu uliopita, Atletico Madrid, ilipokonywa tonge mdomoni mara mbili, wakiikosa La Liga na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati ambapo dunia nzima ilikuwa imeshajiandaa kumshangilia bingwa mpya, kwa jina la Atletico Madrid. Msimu huu, Diego Simeone na vijana wake atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na Barcelona na Real Madrid na hapo ndipo umuhimu wa uwepo wa kombinesheni ya Antoine Griezman, Yannick Carraso na Kevin Gameiro inapokuja. Griezman alikuwa mmoja wa mastaa waliotikisa katika michuano ya Euro 2016 na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kiasi cha kumshawishi Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kuamini kuwa, alistahili kupewa tuzo ya Ballon d’Or kama sio kuwepo katika orodha ya tatu bora badala ya Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Luis Suarez. Unaiamini BBC na MSN? Subiri moto wa CGG (Carrasco, Gameiro na Griezman).

EDINSON CAVANI, LUCAS, ANGEL DI MARIA (PSG)

Baada ya kumpoteza Zlatan Ibrahimovic aliyetimkia Manchester United, Kocha wa Paris Saint-Germain, Unai Emery itamlazimu kuziba pengo lililoachwa na ‘Ibracadabra’ katika safu ya ushambuliaji. Sawa PSG imempoteza Ibrahimovic lakini asikudanganye mtu, bado ni moja ya timu hatari ambayo hutakiwi kuomba kukutanishwa nayo na hii inatokana na uwepo wa utatu wa Edinson Cavani, Lucas Moura na ‘magnificent’ Angel Di Maria. Kuondoka kwa Zlatan kunamaanisha kuwa sasa Cavani atarudi katika nafasi yake aliyoizoea tangu akiwa Napoli huku winga machachari wa Brazil, Moura akiwa ameanza kuonyesha makucha yake na bila shaka Unai Emery atakuwa na kila sababu ya kutopata presha kwa sababu yuko mtu anayeitwa Moura uwanjani. Kasi na ufundi wa Lucas ambao unashabihiana na ule wa Di Maria utazidi kuongeza ladha katika safu ya ushambuliaji ya PSG, na kwa sababu Chelsea na Arsenal wamezoea kuinyanyasa PSG, waanze kukaa mkao wa tahadhari, kwani mnyama safari hii kawa Simba hasa!

WILLIAN, DIEGO COSTA, EDEN HAZARD (CHELSEA)

Kocha Antonio Conte atakuwa na matarajio kibao kutoka kwa kombinesheni hii ya Willian, Costa na Hazard. Ukiwa na straika ambaye yuko tayari hata kurusha ngumi ili mradi tu afumanie nyavu, kama kocha unahitaji nini tena kama siyo kuendelea kutabasamu na kumwacha aendelee kufanya yake. Ukiwa na winga mwenye nguvu, ufundi na kasi kama alivyo Willian na kiungo mshambuliaji mjanja kama Hazard, unachosubiri ni kuona tu wapinzani wakiteseka uwanjani.

Licha ya hapo awali kudaiwa kwamba Costa anataka kuachana na timu hiyo, mwanzo wake mzuri kwenye Ligi Kuu England unabadili kila kitu na kufungua matumaini mapya ya kuendelea kubaki Stamford Bridge. Costa alifunga mabao ya ushindi katika mechi zote mbili walizocheza kwenye ligi na hivyo kuifanya Chelsea kuanza kwa gia nzuri msimu huu. Willian ambaye msimu uliopita alikuwa ni mchezaji bora wa Chelsea, ni mmoja wa wachezaji wanaomvutia Conte na kuna kila dalili kuwa msimu huu akawa moto wa kuotea mbali bila kusahau Hazard ambaye anaonekana ni kama kazaliwa upya chini ya kocha huyo Mtaliano tofauti na alivyokuwa msimu uliopita.

WAYNE ROONEY, ZLATAN IBRAHIMOVIC, PAUL POGBA (MANCHESTER UNITED)

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu ni nani hasa anastahili kujiita ‘Mungu’ wa Old Trafford kati ya Zlatan Ibrahimovic aliyejiunga msimu huu na gwiji wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona. Zlatan amekuja na matumaini makubwa ya kuibeba United kama ambavyo

amekuwa akifanya katika klabu alizopitia japo usajili wa Paul Pogba nao ukionekana kuongeza ladha fulani katika kikosi cjha United.

Ni mwanzo mpya na utawala mpya wa United, chini ya ‘Special One’, Jose Mourinho na bila shaka baada ya kuanza vizuri kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii na baadaye kuanza kwa ushindi katika mechi zao mbili za mwanzo kwenye Ligi Kuu England, ambapo Ibrahimovic amefunga katika mechi zote hizo. Rooney naye ni matata na jina lake limeshaingia kwenye ukurasa wa waliotikisa mabao kwenye ligi huku akitoa asisti matata pia. Ujio wa Pogba, staa mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na pasi za hatari unaifanya Man United kuwa na utatu matata ambao hakika utakuwa mtihani mzito kwa timu pinzani pindi itakapoingia uwanjani kukabiliana nao.

MARCO REUS, PIERRE-EMERICK AUBAMEYANG, MARIO GOTZE (BORUSSIA DORTMUND)

Mario Gotze na Marco Reus watakuwa na nafasi ya kuwasha upya moto wao, ambao umekuwa ukizinyima usingizi beki nyingi za Bundesliga.

Ikiwa ni moja ya timu ambazo ni nadra kusikia inachukiwa na shabiki yeyote wa soka duniani, Borussia Dortmund kwa muda mrefu sasa imekuwa ni moja ya timu zilizofanikiwa kujenga vikosi bora vya soka katika siku za hivi karibuni. Msimu huu wamenunuliwa washambuliaji wenye vipaji vikubwa akiwemo Ousmane Dembele na Emre Mor, lakini usajili ambao umeonekana kuwaridhisha mashabiki wengi ni usajili uliomrejesha ‘mwana mpotevu’ Mario Gotze.

Utatu mkuu wa ushambuliaji unaoundwa na Marco Reus, Pierre-Emerick Aubameyang na Mario Gotze, ni wenye uwezo wa kuitikisa ngome ya timu yoyote pinzani na wengi wanaitaja Dortmund kama ‘farasi mweusi’ itakayokimbiza ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kimya kimya. Kasi na umaliziaji mzuri wa Aubameyang, ufundi na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira alionao Marco Reus bila kusahau pasi za mwisho na hatari (penetration killer passes) na jicho la mwewe alionao Mario Gotze zikiletwa pamoja unapata kitu kinaitwa Sukari ya Macho!

DOUGLAS COSTA, ROBERT LEWANDOWSKI, THOMAS MULLER (BAYERN MUNICH)

Robert Lewandowski na Thomas Muller ni kati ya washambuliaji bora kwa sasa duniani huku Bayern Munich inayonolewa na mmoja wa makocha wenye uzoefu na mafaniko makubwa, Carlo Ancelotti, ni moja ya klabu bora katika ulimwengu wa sasa wa soka.

Lewandowski, Muller na Mbrazili Douglas Costa bila ubishi ni moja ya kombinesheni hatari zinazotawala soka la sasa ambapo katika enzi za Pep Gurdiola, Douglas alikuwa ni kipenzi na chaguo la kwanza ambapo mara kadhaa alinukuliwa akimwagia sifa: “Ni mmoja wa mawinga wazuri kwa sasa, ana uwezo na kipaji ambacho ni ngumu kukipata kwa mchezaji mwingine, anajua kuchezea mpira, na ndiyo maana aliweza kumweka nje Ribery.”

GARETH BALE, KARIM BENZEMA, CRISTIANO RONALDO (REAL MADRID)

Balaa la BBC lilionekana msimu uliopita baada ya kuiongoza Real Madrid kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 11, mbele ya mahasimu wao, Athletico Madrid na tangu hapo kumekuwa na shauku miongoni mwa mashabiki wa Los Blancos, wengi wakijiuliza kuwa je, Bale, Benzema na Ronaldo wataweza kumsaidia Zinedine Zidane, kutwaa Ubingwa wa UEFA msimu huu?

Bale, Benzema, Ronaldo, unapotaja majina hayo usiwe na papara na badala yake unapaswa kuwaza jibu la swali hili, kuna klabu yoyote ambayo haihitaji huduma ya wachezaji hawa? Jibu lake baki nalo, lakini ukweli ni kwamba hakuna beki ambaye anaweza kuzima moto wa BBC pale wanapoamua kuteketeza msitu.

Hata hivyo, mabingwa hawa wa kihistoria wa Ulaya, ambao wana kila sababu ya kujiamini huku wakiwa na sapoti ya bilionea jeuri, Florentino Perez wameweza kujenga kikosi hatari na imara. Kama huamini katika uwezo wa BBC, nakushauri umuulize Diego Simeone. Tangu alipojiunga na Real Madrid, Bale ameshaisaidia klabu yake kushinda mataji mawili ya Ulaya.

MESSI, LUIS SUAREZ, NEYMAR (BARCELONA)

Hili ni balaa lingine katika soka la sasa ambalo litakusahaulisha enzi za Ronaldinho Gaucho, Lionel Messi, Thiery Henry na Samwel Eto’o.

Utatu mtakatifu wa Barcelona unaoundwa wachezaji watatu kutoka katika soka la Amerika Kusini, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar Jr.

MSN ni habari nyingine katika kutikisa nyavu za timu pinzani. Msimu uliopita MSN iliweka rekodi ya kupachika jumla ya mabao 131, mabao ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangia Barcelona kubeba mataji mawili Copa del Rey na La Liga.

Kila mtu anaufahamu uwezo wa Messi awapo uwanjani, lakini unapoongeza vipaji viwili vya Suarez na Neymar kinachotokea hapo ni hatari tupu na ndiyo maana mabeki wengi hupata shida pindi wanapokutana na watu hawa.

Ukiachilia mbali uwezo binafsi walionao, Messi, Suarez na Neymar pia wamefanikiwa kutengeza moja ya kombinesheni hatari na inayoelewana kiasi kwamba wanapocheza unaweza ukadhani ni mtu mmoja yuko pale mbele; jinsi wanavyoonana.