Somo la Twite litadumu sana

Beki wa Yanga, Mbuyu Twite

Muktasari:

Twite ni Mkongo aliyelowea Rwanda na kufanikiwa kucheza soka la kulipwa nchini. Miaka yake mitano nchini haikuwahi kuwa ya hasara kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya Yanga ambayo imeona huduma yake kwa sasa imetosha.

MWANADAMU anaishi mara moja tu. Mbuyu Twite yupo mmoja tu na ameishi mara moja pale Yanga na sasa imefikia wakati wa kumpa mkono wa kwaheri. Hakuwahi kupendwa kama Haruna Niyonzima lakini umuhimu wake haukuwahi kubezwa.

Twite ni Mkongo aliyelowea Rwanda na kufanikiwa kucheza soka la kulipwa nchini. Miaka yake mitano nchini haikuwahi kuwa ya hasara kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya Yanga ambayo imeona huduma yake kwa sasa imetosha.

Wachambuzi mbalimbali wa soka pamoja na wadau wengine wa mchezo huo wamekiri kuwa mwisho umefikia kwa staa huyo ambaye amewahi kuichezea timu ya taifa ya Rwanda. Hata hivyo bado atabaki kuwa mchezaji wa aina yake kufanikiwa kucheza nchini.

Sakata lake na Simba

Rais wa zamani wa Simba, Aden Rage alikwenda Rwanda akazungumza na Mbuyu Twite kwaajili ya kumsajili kisha akamleta Dar es Salaam kwaajili ya utambulisho. Mabosi wa Yanga wakayaona mavitu ya Twite wakasanda, wakaona jamaa atakuja kuwatoa nishai.

Mabosi hao wakapiga simu pale APR Rwanda wakauliza kama Simba wameshawalipa mkwanja ili kumchukua Twite wakaambiwa wawasiliane na FC Lupopo ya pale Kongo. Mabosi hao wakachukua mkwanja fasta wakamalizana na Wakongo hao na Twite aliporejea nchini kwa mara ya pili alipokelewa na watu wa Yanga amba walimtengenezea jezi namba 4 halafu wakaiandika RAGE. Ni kejeli kubwa lakini Rage hakuwa na la kufanya na akakubali jamaa atue tu jangwani kiroho safi.

Hata hivyo baada ya miaka mitano sasa Yanga wamemwambia Twite kuwa inatosha na anaweza kurejea kwao Rwanda kula pensheni. Hata hivyo Twite anaondoka akiwa ameweka rekodi ya kucheza soka la kulipwa nchini kwa muda mrefu akiwa ameitumikia Yanga kwa miaka mitano na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu, moja la FA na matatu ya Ngao ya Hisani.

Uwezo wa kurusha mpira

Twite ndiye aliyewafanya watu wa Yanga kumsahau nyota wao wa zamani, Fred Mbuna ambaye alikuwa anarusha mpira kutoka Ubungo hadi Shekilango. Tambwe ambaye ni Mnyarwanda mwenye asili ya Kongo ana uwezo mkubwa wa kurusha mpira kuliko staa yeyote wa Ligi Kuu. Alifanikiwa kuvaa viatu vya Mbuna vilivyo. Twite akirusha mpira ni sawa na mpira wa kona kwani unafika katika eneo la hatari na unaweza kuleta madhara. Mpira wake wa mwisho wa kurusha uliokuwa na madhara ni dhidi ya Mbao FC ambapo ulizaa bao. Yawezekana ni kweli Twite ameporomoka kiwango lakini kamwe huwezi kumsahau kwa hili la kurusha mpira.

Kiraka

Simba wanafikiria kumchukua wampe nafasi ya Janvie Bokungu lakini bado hawajaafikiana. Mbuyu Twite alisajiliwa Yanga kama beki wa kulia lakini baadaye akabadilishiwa nafasi na kucheza kama beki wa kati. Baadaye akapelekwa kucheza kama kiungo wa chini nafasi ambayo alionekana kuimudu vizuri zaidi. Hata hivyo kutokana na mahitaji mbalimbali ndani ya timu, Twite alilazimika kucheza nafasi yoyote ambayo angepangwa. Mfano kuelekea mechi na TP Mazembe mwezi Juni mwaka huu mabeki wote wa kushoto wa Yanga hawakuwepo kwenye timu. Oscar Joshua alikuwa majeruhi na Mwinyi Haji alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu. Kocha Hans Van Pluijm alilazimika kumpanga Twite katika nafasi hiyo ambayo aliimudu vizuri kwa mchezo wote. Hii ndiyo tofauti kubwa ya Twite na wachezaji wengine. Katika moja ya mahojiano yake alisema amewahi kucheza nafasi karibu zote uwanjani isipokuwa ya kipa tu.

Nidhamu

Umewahi kusikia Twite ameleta usumbufu wowote ndani ya timu? Hata kama umewahi kusikia basi haikuwa kweli. Twite ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye nidhamu ya hali ya juu iwe ndani ama nje ya uwanja. Huwezi kusikia amechelewa mazoezini ama amegombana na kocha. Huwezi kusikia amekwenda kwao Rwanda akachelewa kurejea nchini kama ilivyowahi kutokea mara kadhaa kwa wachezaji kama Emanuel Okwi na Donald Mosoti. Twite ana nidhamu kubwa. Ana nidhamu ya mchezo na nidhamu ya nje ya uwanja. Huwezi kusikia ameonekana klabu ama katika viwanja ambavyo vinahatarisha kiwango chake. Kipindi cha nyuma alikuwa akicheza mechi za Ndondo lakini baada ya viongozi wa Yanga kupiga marufuku aliacha mara moja.

Kiwango

Licha ya kuonekana ameshuka kiwango katika siku za karibuni lakini Twite ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni ambao wamecheza kwa kiwango hicho hicho kwa muda mrefu. Tangu alipotua nchini mwaka 2012, Twite amekuwa akicheza kwa kiwango kilekile na hata wakati alipotetereka alijipanga na kurejea tena katika makali yake. Ni katika nyakati chache ambazo ungemkosa Twite katika kikosi cha kwanza cha Yanga. Alikuwa mchezaji muhimu wa nyakati zote ambapo licha ya ujio wa wachezaji wapya bado ilikuwa ngumu kumuweka pembeni. Tangu alipobadilishwa kucheza nafasi ya kiungo na kocha Marcio Maximo, Twite amekuwa akiimarika katika nafasi hiyo na ameacha deni kwa Justine Zulu ambaye atarithi mikoba yake.