Soka la England na kashfa ya unyanyasaji wa kingono

Aliyewahi kuwa Kocha wa timu ya vijana ya Newcastle,

George Ormond

Muktasari:

Wachezaji kadhaa wamejitokeza na kuweka bayana kwamba, walidhalilishwa na ama makocha au viongozi wa klabu husika. Wachezai hao wa zamani ambao, sasa ni watu wa makamo waliamua kuachana na kuficha majina yao na kuzungumza hadharani huku wakilia juu ya kilichowapata miaka ya ’1970 na ya ’80.

NOVEMBA mwaka huu yamefumuka mambo ambayo yanaeleza uozo kwenye soka la England, kwa maana ya unyanyasaji wa wachezaji chipukizi kingono uliofanyika miaka kadhaa iliyopita na kuhusisha na mabosi wa klabu.

Wachezaji kadhaa wamejitokeza na kuweka bayana kwamba, walidhalilishwa na ama makocha au viongozi wa klabu husika. Wachezai hao wa zamani ambao, sasa ni watu wa makamo waliamua kuachana na kuficha majina yao na kuzungumza hadharani huku wakilia juu ya kilichowapata miaka ya ’1970 na ya ’80.

Udhalilishaji huo kimsingi unahusu wachezaji waliokuwa bado watoto na baadhi ya klabu zilizotajwa hadi sasa ni pamoja na Chelsea, Crewe Alexandria, Manchester City, Newcastle na Southampton, lakini huenda kuna zaidi ya hizo na waathirika wengine wameamua kukaa kimya na siri zao.

Haya ndiyo mambo ya nyuma ya pazia kwenye soka, ambapo makocha au viongozi walitumia nafasi zao kukidhi matamanio yao kutoka kwa watoto wa kiume ambao, ilibidi waridhie kwa sababu ilimaanisha kwamba iwapo wangekataa wangeweza kuondolewa kwenye timu na wakikubali walipewa nafasi za kuendelea kusonga mbele katika akademia na kuwa na uhakika wa kuingia kwenye vikosi vya wakubwa na hata vikosi vya kwanza.

Kuna waliopata kushitakiwa kwa unyanyasaji wa kingono wa watoto hao na hata kutiwa hatiani na mahakama na kufungwa jela, akiwamo George

Ormond, aliyekuwa kocha wa timu ya vijana ya Newcastle aliyetupwa jela miaka 200 na Skauti Mkuu wa zamani, Eddie Heath wa Chelsea. Kadhalika kuna madai mazito kwamba, klabu zilikuwa zikijaribu kufunika uchafu huo na hata kuwalipa fedha watoto husika ili wafiche siri, Chelsea wakitajwa kuhusika katika hilo.

Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Gary Johnson amejitokeza miaka karibu 40 tangu adaiwe kufanyiwa vitendo hivyo na Heath. Ameibuka na kusema alitendwa mara kadhaa na klabu hiyo tajiri walimlipa pauni 50,000 ili aufunge mdomo wake kuhusiana na kashfa hiyo.

Alikuwa mchezaji kijana enzi hizo na anasema ameteseka sana na jambo hilo ila sasa anaamini kwamba, haki itatendeka.

Anadai alifanyiwa vitendo vya udhalilishaji na Heath kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, lakini si Polisi wala Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) waliomsaidia kwenye hilo.

Baada ya kuona hakuwa na la kufanya, Johnson ambaye sasa ana umri wa miaka 57, anasema aliwaendea mabosi wa klabu ambao hata hivyo, walikataa kupokea lawama zake mwaka jana ila wakampatia pauni 50,000 na kumwambia akae kimya.

Ameamua kuachana na mpango wa kukaa kimya au kutotajwa jina lake ili aeleze uzoefu wake kwenye hilo na kuunga mkono waathiriwa wengine wa unyanyasaji huo.

Nyota huyo alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Chelsea kuanzia 1978 hadi 1981, anasema ni kweli Heath alimjenga kisoka lakini mbaya ni kwamba alianza kumfanyia matendo hayo machafu akiwa na umri wa miaka 13 na kwamba, anaona aibu kuwa utoto wake uliharibiwa kwani tangu afanywe hivyo, hadi kufika umri wa miaka 20 alikuwa na mtikisiko mkubwa wa kiakili na kisaikolojia.

Hadi Desemba Mosi, mwaka huu, kulikuwa na watu karibu 350 ambao waliamua kuripoti mambo hayo ya zamani katika vituo vya polisi nchini Uingereza, lakini wengine wamepiga ripoti kwa Chama cha Soka cha England (FA) na wengine wakiamua kuziendelea moja kwa moja klabu husika.

Hapa Uingereza imetolewa namba maalumu kwa ajili hiyo na mwitikio ni mkubwa, japokuwa inawezekana katika hao kuna wengine wanadanganya, baadhi wanatafuta huruma au uwezekano wa unafuu wa maisha kwa kulipwa fidia, lakini kwa ujumla lisemwalo lipo na kama halipo linakuja.

Suala hili limeshika kasi hapa London na miji mingine, na ni moja ya mada kubwa kwenye vijiwe mbalimbali na hata mitandao ya jamii.

Kwa mfano, polisi wa Greater Manchesrter wanasema kwamba, tayari wanaendesha uchunguzi juu ya ripoti za watu 35 na tayari wana watuhumiwa 10 ambao wametambuliwa. Jijini London hakuko kimya kabisa, uchunguzi wa kina umeshaanza na kasi yake ni kubwa kwelikweli.

Inavyoelekea waathirika wengi zaidi watajitokeza kusema hili na lile dhidi ya kocha mmoja au wawili na bila shaka Polisi watakuwa na kazi kubwa ya kufanya kwenye hili, kama ambavyo klabu nazo zitabeba misalaba juu ya uhusika wao na kushindwa kuwalinda wachezaji hao kwa namna moja ama nyingine. Waathirika England ndioa wameanza, tusubiri mataifa mengine.