Simba kugongwa 2-0? Haiwezekani!

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo ni kwamba Yanga na Simba zilikutana mara ya kwanza Februari 10, 1983 na pambano kumalizika kwa sare isiyo na mabao kabla ya Simba kufa mara mbili mfululizo katika mechi zilifuata ndani ya mwezi huo kwa misimu tofauti.

ACHANA na Amissi Tambwe kuonekana ndiye mchezaji anayeiliza Simba katika miaka ya karibuni, lakini ukweli ni kwamba Simba haijawahi kushinda mechi yoyote dhidi ya Yanga katika pambano linalochezwa Februari.

Katika mechi tano ambazo timu hizo zimewahi kukutana katika Ligi Kuu ndani ya mwezi huo, Yanga imeishinda Simba mara tatu tena kila moja kwa mabao 2-0, kitu kinachowapa jeuri mashabiki wake kuamini hata safari hii itajirudia tena.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo ni kwamba Yanga na Simba zilikutana mara ya kwanza Februari 10, 1983 na pambano kumalizika kwa sare isiyo na mabao kabla ya Simba kufa mara mbili mfululizo katika mechi zilifuata ndani ya mwezi huo kwa misimu tofauti.

Awali ilipigwa 2-0 katika pambano la Februari 26, 1994 kisha kugongwa tena 2-0 Februari 25, 1996 na miaka miwili baadaye katika pambano la Februari 21, 1998 timu hizo ziliishia kufungana bao 1-1 kabla ya Februari 20 mwaka jana, Simba kulala tena 2-0.

Mbali na Yanga kubebwa na Februari, ila uwepo wa Tambwe kikosini unaelezwa kuwakosesha raha mashabiki wa Simba kwani amekuwa na bahati ya kuwalaza mapema kwa mabao yake ambapo mechi tatu zilizopita Mrundi huyo amefunga mara zote, jambo hilo limewapa mzuka mashabiki wa Jangwani.

Baadhi ya mastaa wanaoishabikia Yanga kama Kulwa Kikumba ‘Dude’, Mike Sangu na Jacquiline Wolper, wameitabiria Yanga kuilaza Simba mabao mawili, lakini mashabiki wa Simba waliposikia utabiri huo wamekataa wakidai thubutu yenu!

William Mtitu na Jennifer Kyaka ‘Odama’ kila mmoja ametamba kuwa safari hii Simba lazima amkalishe Yanga Taifa kwa ushindi murua.

Odama alisema anaamini Simba itashinda mabao 2-1, wakati Mtitu akitamba kuwa watashinda mabao 3-0 na wadungaji lazima wawe Shiza Kichuya, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib ili kukamilisha utatu wao maarufu kama KIAMA.

Mgosi afunguka

Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema ni kweli Yanga imekuwa na bahati na Februari, lakini sio kwa mwaka 2017 kwani ni lazima Simba ishinde kwa namna walivyojiandaa na wachezaji wao walivyo na mzuka wa kutupia.

“Hizo ni historia, we njoo Taifa uone nani atakayefungwa, mwaka 2017 tumekuja kivingine na lazima Simba tuwanyamazishe Yanga,” alisema Mgosi.

Mgosi alisema Simba ni lazima itawapiga Yanga mabao 2-1 na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani.

“Yanga tutawafunga tu tena siyo hata bao nyingi mbili tu kama unabisha utaona na wakipambana sana wanaweza kupata bao moja tukamaliza na ushindi wa 2-1.”

“Mpira hauangalii historia, mpira unachezwa uwanjani kama wao wana historia ya kutufunga mwezi wa pili, safari hii wajue kabisa ni zamu yao,” alisema Mgosi.