SIMBA NOMA: Rekodi za Simba zinavyoitesa Yanga kimataifa

Muktasari:

  • Simba ambayo imewahi kushinda mataji 18 ya Ligi Kuu Bara, ndiyo timu kutoka Tanzania ambayo ina mafanikio makubwa zaidi katika medani ya kimataifa. Rekodi hizo ni kama zinaitesa Yanga ambayo ipo katika dalili ya kukosa nafasi ya kusonga mbele katika mashindano ya mwaka huu.

YANGA imeweka rehani nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Zanaco juzi Jumamosi jijini Dar es Salaam. Timu hizo zitakutana mjini Lusaka, Zambia wikiendi hii katika mechi ya marudiano.

Wakati Yanga, ikiendelea kusaka rekodi katika mashindano ya kimataifa ikiwemo Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho Afrika na kombe la Kagame, kumbe Simba walishamaliza zamani mambo hayo. Yaani Simba ndiyo wababe wa rekodi za maana.

Simba ambayo imewahi kushinda mataji 18 ya Ligi Kuu Bara, ndiyo timu kutoka Tanzania ambayo ina mafanikio makubwa zaidi katika medani ya kimataifa. Rekodi hizo ni kama zinaitesa Yanga ambayo ipo katika dalili ya kukosa nafasi ya kusonga mbele katika mashindano ya mwaka huu.

Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti pekee la michezo linalochapwa Tanzani na Kenya, linakuletea rekodi kali za Simba katika mashindano ya kimataifa ambazo zinaipa Yanga wakati mgumu. Pengine itawachukua Yanga muda mrefu kuzifikia.

Kombe la CAF

Rekodi ya kwanza ya Simba katika mashindano ya kimataifa ni ile ya kufanikiwa kutinga fainali ya kombe la CAF mwaka 1993. Simba ikiwa chini ya Kocha Abdallah Kibadeni ilifanya maajabu hayo na                            ilicheza fainali ya mashindano hayo makubwa ya Afrika. Licha ya Simba kupoteza mchezo wa fainali kwa Stella Abidjan ya Ivory Coast, bado inabaki kuwa timu pekee kutoka Tanzania kuweza kufuzu hatua hiyo ya juu zaidi.

Maajabu ya Mufulira

Simba siyo timu ya mchezo ati. Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu waliwahi kuisimamisha Zambia baada ya kuitungua Mufulira Wonderers ya nchini humo kwa mabao 5-0, tena nyumbani kwao. Iko hivi, Mwaka 1979 Simba ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kukutana na timu ya Mufulira kutoka Zambia.

Mabingwa hao wa zamani wa Zambia walitinga Dar es Salaam kwa kujiamini na kuitandika Simba mabao 4-0. Wakati wadau wote wa soka nchini wakiamini kwamba Simba inakwenda Zambia kukamilisha ratiba, timu hiyo ilishangaza. Simba iliitandika Mufulira mabao 5-0 ugenini na kusonga mbele. Yanga haiwezi mambo makubwa kama haya.

Kuwatoa Waarabu

Katika kipindi cha karibuni Yanga angalau imeanza kuonyesha kwamba inaweza kupambana na timu kutoka ukanda wa Afrika Kaskazini. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita licha ya kujitahidi, Yanga ilitolewa na timu za Al Ahly na Etoile Du Sahel kwa nyakati tofauti. Mwaka 2012, Yanga ilitolewa pia na Zamalek ya Misri.

Wakati Yanga ikiteseka na Waarabu, Simba ndiyo kiboko yao. Mwaka 2003, Simba ilifanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwaondoa Zamalek. Haikuwa kazi rahisi kwani Zamalek walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo. Simba ilishinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaal kabla ya kupoteza kwa idadi kama hiyo kwenye mchezo wa marudiano pale Misri. Simba ilifanikiwa kusonga mbele kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.

Kukusanya pointi nyingi

Yanga licha ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 na kisha hatua kama hiyo katika kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana, imejikuta ikishindwa kuvunja rekodi ya Simba. Mwaka 1998, Yanga pamoja na kufuzu hatua hiyo, ilimaliza mechi zote za hatua ya makundi bila kupata ushindi hata mmoja. Mwaka jana Yanga ilikusanya pointi nne tu katika mechi zake zote za hatua ya makundi.

Matokeo hayo yaliifanya Simba kuendelea kushika rekodi ya kuwa timu pekee ya Tanzania ambayo imewahi kukusanya pointi nyingi zaidi katika hatua ya makundi. Simba ilikusanya pointi saba wakati ilipofuzu hatua ya makundi kwa mara ya mwisho mwaka 2003 idadi ambayo haijawahi kufikiwa na Yanga.

Nusu fainali

Simba ndiyo timu pekee ya Tanzania ambayo ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mabingwa wa CAF. Simba walifanya hivyo mwaka 1974. Mafanikio hayo yaliwafanya Simba kuwa klabu ya Tanzania iliyoweza kucheza hatua ya juu zaidi ya mashindano hayo ya CAF. Kwa sasa michuano hii haipo tena hivyo Simba imeacha rekodi isiyofutika.

Kombe la Kagame

Kwa kuonyesha kwamba haibahatishi, Simba ndiyo klabu iliyoshinda taji la Kagame mara nyingi zaidi. Mashindano hayo yanashirikisha timu kutoka Afrika Mashariki na Kati. Simba imewahi kushinda taji hilo mara sita na kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi katika michuano hiyo.

Rekodi hiyo ya Simba imedumu kwa muda mrefu na licha ya kushindwa kutwaa taji hilo kwa miaka 15 sasa, hakuna klabu iliyoweza kuwafikia. Yanga kwa upande wake imewahi kutwaa taji hilo mara tano tu.