Ramani haisomeki

Saturday February 11 2017Haji Ugando ,mchezaji wa simba

Haji Ugando ,mchezaji wa simba 

By Thobias Sebastian

KAMA wahenga walivyosena kuwa, ngoma bwana ikivuma sana, lazima ipasuke. Ndani ya soka la Tanzania kuna baadhi ya wachezaji walioibuka na kutamba katika klabu mbalimbali kabla ya kuzimika kama hawapo vile.

Baadhi yao wamezimika baada ya kujiunga na klabu kubwa na sasa hawasikiki tena, hivyo wakitakiwa kufanya kazi ya ziada kurejesha makali yao, la sivyo wanaweza kusahaulika kabisa.

Mwanaspoti inakuletea baadhi ya nyota hao ambao waliwika kwa nyakati tofauti na sasa wamebaki majina tu, kitu kinachowapa changamoto kubwa ya kufufua ukali wao uwanjani ili waendelee kuimbwa na mashabiki kama zamani.

Hassan Kessy

Mmoja kati ya mabeki wa kulia waliotamba msimu uliopita kabla ya kuwa na mwisho mbaya ndani ya klabu yake ya Simba.

Kessy baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na mabosi wake wa Msimbazi aliamua kuhamia Yanga katika usajili uliokuwa na utata, lakini uliompa fursa ya kuicheza Jangwani. Hata hivyo mpaka sasa hajawa na hali nzuri Yanga kutokana na kukosa namba mbele ya Juma Abdul.

Kessy kabla ya kusajiliwa na Yanga alikuwa akisikika kama mmoja wa mabeki bora wa upande wa kulia lakini hivi sasa amekuwa kimya kana hayupo kwa sababu Abdul ameendelea kuwa chaguo la kwanza kwa kocha George Lwandamina kama ilivyokuwa kwa Hans Pluijm. Ana kazi kubwa ya kurejesha makali ili kusikika kama zamani.

Juma Mahadhi

Alisajiliwa na Yanga akitokea Coastal Union baada ya kuonesha kiwango kizuri katika zile mechi mbili za ligi na hata katia Kombe la FA.

Winga huyo alianza kwa makeke ndanji ya Yanga walipovaana na TP Mazembe katika mechi ya kimataifa na watu kumtabiria kuwa tishio, lakini mambo yameenda sivyo ndivyo, kwani ni kama kazimika kimtindo.

Mahadhi ilitarajiwa kufanya makubwa katika klabu hiyo kutokana na umri wake kuwa mdogo na uwezo wake mkubwa, alionao hata kwa namna mambo yalivyomuendea ni lazima apambane kwelikweli ili asisahaulike mapema.

Geofrey Mwashuiya

Winga mwingine chipukizi wa Yanga aliyetua Jangwani akitokea Kimondo na kutabiriwa makubwa kutokana na kasi na uwezo wake wa kupiga mashuti ya mwendo kasi.

Mwashiuya ameshindwa kuwapiku wazoefu, Simon Msuva na Deus Kaseke, licha ya kupewa nafasi mara kadhaa bado hajaonyesha makali kama wakati aliposajiliwa na kucheza mechi za kitaifa na kimataifa.

Kwa namna ushindani uliopo ndani ya Yanga, lazima Mwashiuya akaze buti la sivyo atasahaulika kama walivyowahi kusahaulika nyota wengine waliowahi kusajiliwa na kuichezea klabu hiyo.

Haji Ugando

Kabla ya kunyakuliwa Simba alikuwa akicheza zake soka Italia na baada ya kutua hapa nchini wengi walimtabiria makubwa kwa umri aliokuwa nao. Chini ya makocha Dylan Kerr na hata Jackson Mayanja, Ugando alikuwa akipata nafasi ya kuonyesha kipaji chake, lakini alishindwa kulinda namba yake na sasa amekuwa akiwa mchezaji wa jukwaani zaidi kuliko benchi ama uwanjani.

Chini ya Kocha Joseph Omog, winga huyo hajacheza mechi hata moja, hali inayowafanya mashabiki kuanza kumsahau na ni jukumu lake la kupigana kufa na kupona kuonyesha kuwa bado wamo.

Peter Manyika ‘Jr’

Mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga na Mtibwa Sugar, Manyika Peter tangu msimu uliopita amepotea kabisa masikioni na machoni pa mashabiki wa soka.

Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi alipewa mechi kadhaa, kabla ya kurejea benchini kumpisha Mghana, Daniel Agyei kama alivyokuwa akikalishwa benchi na Vincent Angban raia wa Ivory Coast ambaye ameshatimuliwa klabuni.

Manyika ni kati ya makipa chipukizi wenye vipaji na kama angekaza kwa sasa angekuwa anakula sahani moja na Aishi Manula wa Azam, hivyo kazi kubwa anayo kurejesha imani kwa makocha wake.

Baada ya kufanya kweli kwenye mechi ya watani, Simba na Yanga iliyoisha kwa sare isiyo na mabao, wengi walimtabiria kutisha nchini kama baba yake, lakini bahati mbaya amezimika na ni wajibu wake kurejesha majali yake tena.

Ramadhani Singano

Winga machachari anayefahamika zaidi kama Messi, alitisha alipokuwa Simba. Aliishirikiana na vijana wenzake ndani ya Simba tangu mwaka 2013 kufanya makubwa kabla ya kuamua kuzinguana na mabosi wake na kuhama.

Singano aligoma kuendelea kuichezea Simba katika utata wa mkataba wake na kuhamia Azam ambapo tangu atue hapo amepoteza makali yake. Ingawa makocha wa timu hiyo tangu enzi za Stewart Hall, Zeben Harnandez na Idd Nassor ‘Cheche’ walimpa nafasi mara kwa mara kucheza, bado hajarudi kwenye makali yake ya zamani yaliyomfanya aimbwe kama Messi kwelikweli.

Naye ana kazi kubwa kurejesha makali yake, kabla ya kuzikwa kwenye kaburi la sahau la mashabiki wa soka nchini.

Atupele Green

Mshambuliaji matata wa zamani wa Yanga, Coastal Union, Kagera Sugar, Ndanda na sasa akikipiga JKT Ruvu amepotea kama utani. Hana tena makali aliyokuwa nayo kama zamani hasa msimu uliopita alioshinda mpaka tuzo ya Mfungaji Bora wa Kombe la FA akimpiku Hamis Kiiza aliyekuwa Simba.

Atupele kama straika mwingine wa klabu hiyo ya Maafande wa JKT Ruvu, Saady Kipanga amezimika na ana kazi kubwa ya kurejesha makali yake, huku akiwa na hali mbaya zaidi kwa sababu JKT haifanyi vizuri ikichungulia kaburi la kushuka daraja kwenda FDL.