RIPOTI MAALUM: Duh! TFF ya Malinzi imepoteza mvuto- 1

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Muktasari:

  • Katika utafiti huo, dodoso 100 zilisambazwa na hadi chapisho hili linafanyika ni dodoso 72 zilizokuwa zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 72

UTAFITI unaonyesha kuwa katika soka la Tanzania vitu maarufu ni vitatu tu. Ni Simba, Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Zikaushie Simba na Yanga hapo juu, katika siku za karibuni kumekuwa na malamiko mengi kuhusu TFF jambo ambalo limeonyesha kuwa kuna kitu kinahitajika kufanyika kuhusu shirikisho hilo.

Kwa kufahamu hilo, Mwanaspoti ambalo ndilo gazeti pendwa zaidi la michezo nchini limefanya utafiti kwa kushirikiana na wadau wakubwa wa soka nchini ambao ni klabu za soka za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na wanachama wao ili kufahamu taswira waliyonayo juu ya TFF.

Katika utafiti huo, dodoso 100 zilisambazwa na hadi chapisho hili linafanyika ni dodoso 72 zilizokuwa zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 72 ya dodoso zote. Rais wa TFF, Jamal Malinzi naye alipangua hoja mbalimbali zilizotolewa dhidi yake.

Waliojaza dososo

Katika dodoso hizo wadau wa soka wenye umri kati ya miaka 36-45 ndiyo waliojaza kwa wingi zaidi na ni asilimia 37.5 ya watu wote waliojaza dodoso hizo. Wenye miaka kati ya 26-35 walijaza kwa asilimia 33.3, miaka 46-60 walikuwa 23.6, miaka 60 na kuendelea walikuwa 0.4 huku wenye miaka 18-25 wakiwa ni asilimia 0.1.

TFF ya Malinzi mmh?

Katika utafiti huo ambao ndiyo mkubwa zaidi kufanyika nchini juu ya mwenendo wa TFF, asilimia 86.1 walisema hawaridhishwi na mwenendo wa TFF chini ya Rais wake Jamal Malinzi huku asilimia 13.9 tu wakidai kuwa shirikisho hilo limekuwa na mwenendo mzuri.

Miongoni mwa waliodai kuvutiwa na mwenendo wa TFF walitetea hoja zao kwa madai kuwa soka la Tanzania limeanza kupata mwelekeo na kudai kuwa kilichopo sasa ni changamoto ndogo ndogo tu za kufanyiwa kazi.

“Uongozi wa TFF ni mzuri, lakini panatakiwa parekebishwe kwenye kamati ya Maadili na pili marefarii (waamuzi) waonywe kwa tabia zao za upendeleo,” alisema mmoja wa wahojiwa hao.

“Soka letu hapa Tanzania ni zuri isipokuwa kuna figisu sana Shirikisho la Soka na wamekuwa hawana maamuzi mazuri katika soka,” mwingine alieleza.

“Navutiwa na soka letu kwa sababu wachezaji wanaocheza wanajua majukumu yao na unaona mpira umekuwa sehemu ya kazi,” mwingine alisema.

Hatuvutiwi  Kabisa

Ambao walidai kutovutiwa na mwenendo wa shirikisho hilo walitetea hoja zao pia. “Hakuna uwekezaji wenye tija kwenye soka letu.

TFF na klabu zote havijaweka msisitizo kwenye misingi ya maendeleo ya soka kama vile viwanja na akademia,” alisema mmoja wa wahojiwa.

“Kwanza kabisa malalamiko yamekuwa mengi kwa waamuzi. TFF wanachangia kuzorotesha ligi yetu mpaka inafikia kuziruhusu timu kwenda kucheza bonanza,” alieleza mwingine.

“Kwanza TFF hawako makini katika mambo mbalimbali, maamuzi yao siyo makini, hakuna ukweli wa dhati kama kweli wanapenda soka letu,” alieleza mwingine.

“Mambo mengi hayaendi sawa, mfano kudorora kwa timu ya taifa, mfumo mbovu wa ligi ya taifa,” alieleza mwingine, wakati huo huo mwingine alisema, “Mfumo wa soka letu ni mbovu sana, inatakiwa ubadilike na hata Jamal Malinzi ameshindwa kusimamia soka letu.”

“Kuna mifano mingi, kama masuala ya upangaji matokeo katika ligi zetu na kutosikiliza baadhi ya malalamiko ya timu na kutosikiliza rufaa kwa muda mrefu,” anaeleza.

“Hakuna maendeleo yoyote kwenye soka, Tenga (Leodger) alifanikiwa kujenga miundombinu na kuleta imani ya wafadhili, hakuna maendeleo baada ya hapo,” alieleza mwingine.

“Timu zetu hazifanyi viizuri nje, timu za taifa na klabu kwa pamoja, kumekuwa na changamoto pia ndani ya klabu na uongozi, ligi zina changamoto ya pesa na usimamizi pia,” alieleza mwingine.

“TFF ina waamuzi ambao hawana viwango, hawajui hata offside (kuotea), maana kuna timu huwa haina offside, mfano Yanga, chunguza utaona,” alidai mwingine.

“Rushwa imekuwa kubwa sana tofauti na uongozi wa Tenga, upangaji wa matokeo, kushuka katika viwango vya Fifa pia,” alieleza mwingine.

“Kipindi kilichopita marefa (waamuzi) wazembe walipewa adhabu, kipindi chake marefa wazembe wengi hukumu zake si nzuri, soka letu linasuasua. Ukiwa kiongozi usiegemee upande wowote, yeye anaegemea upande wa Yanga,” alieleza mwingine.

“Ligi mbovu, waamuzi wabovu, upangaji wa matokeo. Kikubwa Jamal Malinzi alikuwa katibu wa Yanga hivyo basi ana kila namna ya kuibeba Yanga hata Kombe la FA ni hivyo hivyo tu,” alieleza mwingine.

“Kwa sababu maamuzi yao ni mabovu, wanachelewa kutoa maamuzi ya makosa mbalimbali, hawasimamii ligi kwa umakini,” alieleza mwingine.

“TFF hawaeleweki, na wala hawajitambui katika kuendesha mpira wa Tanzania hususani ligi zote, kwa mfano kila mdau wa soka anashindwa kuelewa kama Azam leo wanapokwa pointi tatu kwa kosa la kumchezesha Erasto Nyoni, siku zote walikuwa wapi, ukweli hawajitambui,” alieleza mwingine.

“TFF ya Malinzi haifai kabisa kuongoza mpira kwani imeonyesha udhaifu wa hali ya juu kuharibu soka letu, hii inatokana na uongozi wa juu kujihusisha na upangaji matokeo kwa marefa wanaowataka na kuwaagiza kuipendelea Yanga ili mradi ichukue ubingwa,” alieleza mwingine.

“TFF ndiyo kiini cha mpira wa Tanzania lakini wameshindwa kuendeleza mpira wa Tanzania kutokana na miundombinu mibovu,” alieleza mwingine.

“Nasema hapana, wao ndiyo wasimamizi wa ligi ama ligi ni yao lakini wamekuwa hawaifuatilii kwa umakini hivyo ligi imekosa mvuto mpaka muda huu hatujaona refa (Mwamuzi) hata mmoja kapewa adhabu, kwa hiyo hawafanyi makosa?” alihoji mmoja.

“Sijafurahishwa, sifurahishwi na utendaji wa TFF ya sasa kwa kushindwa kusimamia soka nchini kwa usawa. Mfano kuna klabu zinazodaiwa kupanga matokeo lakini klabu zile zilikaa rufaa kupinga adhabu lakini kabla rufaa zao kusikilizwa TFF wakatoa timu kuzipandisha daraja,” anaeleza mwingine.

“Hakuna weledi katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazotokea katika medani ya soka letu, hakuna commitment (kujituma) zaidi ya hayo kuna ushabiki na mapenzi ya timu zao kujali masilahi yao binafsi,” alieleza mwingine.

“TFF imeshindwa kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu badala ya kusonga mbele tunarudi nyuma, migogoro imezidi kuwa mingi pamoja na ubabe mwingi,” alieleza mwingine.

“Yaani wamefeli kila sekta, kila siku wanapiga watu faini zisizo na maana yoyote, yaani uongozi umejaa uozo mtupu, hakuna viongozi pale,” alieleza mwingine.

“TFF wanakuwa wanafanya mambo mengi kwa mazoea, hawatii katiba, hawafuati sheria na taratibu nzima za uongozi wa mpira wa miguu,” alieleza mwingine.

“Uongozi hauna maadili ya kiuongozi, utawala wa kindugu, TFF wameshindwa kuongoza mpira wa Tanzania, uandaaji wa timu ya taifa na udhamini wa ligi ni wa kibabe,” alieleza mwingine.

Malinzi ajibu

“Hili la kupanga matokeo watu wanapiga kelele badala ya kutupongeza kwa kuchukua adhabu kali kwa waliohusika, tumekuwa wa mfano kwa nchi nyingine kwa namna tulivyoshughulikia hilo tatizo,” alisema Malinzi katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

“Haya masuala ya ratiba huwezi kufananisha nchi za wenzetu na sisi, halafu watu wanasahau kitu kimoja kuwa mimi ndiye Rais wa TFF na nitaendelea kuwa hivyo hadi Oktoba mwakani, hayo mengine nisingependa kuyazungumzia sana” alieleza kiongozi huyo.

Usikose sehemu ya pili ya makala hii kesho Jumanne.