Nilikwepa mkataba wa kuzimu Msimbazi-2

Maneno Mbegu

Muktasari:

Alieleza namna alivyoigomea ofa ya Ngome iliyokuwa ikimtaka na kuamua kusalia CDA Dodoma, lakini kumbe bwana, Wekundu wa Msimbazi walikuwa wakimnyemelea ili atue klabu kwao.

WIKI iliyopita tulianza simulizi la nyota wa zamani wa klabu ya Breweries, SHYCOM na CDA, Maneno Mbegu akieleza namna alivyoanza maisha yake ya soka kutoka klabu moja mpaka nyingine.

Alieleza namna alivyoigomea ofa ya Ngome iliyokuwa ikimtaka na kuamua kusalia CDA Dodoma, lakini kumbe bwana, Wekundu wa Msimbazi walikuwa wakimnyemelea ili atue klabu kwao.

Je unajua dili lake la kutaka kutua Simba liliibukaje na liliishaje? Ungana naye katika sehemu hii ya pili na ya mwisho.

 

KOCHA TBL AMSETIA MAMBO

Anaeleza kuwa kila jambo lenye mwanzo huwa na mwisho wake, hivyo alikuwa akiwaza itakuwaje akimaliza soka lake, ndipo akapata wazo la kujiunga na Chuo cha Ualimu Chang’ombe baada ya kuwepo kwa nafasi.

“Nafasi ya kusoma stashahada ya Ualimu niliipata lakini ilinikatisha tamaa, lengo langu lilikuwa baada ya kutoka jeshini niende Chuo Kikuu ili niwe mtu mkubwa siku za mbele kama Meneja wa Kampuni au Ofisa erikalini lakini haikua hivyo.”

“Kwa bahati kipindi hicho timu ya TBL ilikuwa ikifanya mazoezi pale Jangwani na Kocha Mkuu akiwa Shaaban Marijani aliyekuwa pia akiinoa timu ya taifa ya Vijana,” anasema.

“Nikaenda kufanya nao zoezi hapo kwa kupitia mgongo wa kocha huyo, kumbe TBL ilikuwa ikijiandaa kukutana na Simba kwenye mashindano ya kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977.”

 

NYOTA YANG’AA TBL

Baada ya tizi la siku moja tu tayari TBL walivutiwa naye bila ya kufahamu na tayari kocha akamweka kwenye kikosi kitakachopambana na Simba, lakini siku ya pili hakwenda uwanjani na kocha akimsaka ili akae langoni.

“Nilikuwa moja ya makipa hodari enzi hizo, basi walipocheza wakatoka sare na mchezo ukatakiwa urudiwe ndipo nikaonesha uwezo wangu hapo kwani mchezo ulirudiwa mara tatu tukitoka suluhu na mchezo wa mwisho tuliweza kuwafunga Simba Sc ambao walikuwa na wachezaji kama kina Emmanuel Mbele, Jumanne Masimenti, Adam Sabu na Adamu Sakulu.

“Fainali ilitukutanisha na Yanga iliyosheheni mastaa kama kina Fadhil Bwanga, Mwinda Ramadhan na Burhan Hemed wakiongoza mashambulizi pale Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru). Yanga walikuwa mabingwa kwa kutufunga 3-1.”

Anasema kwenye mchezo huo dakika ya 88 Adam Sekulu aliwatoka walinzi wote, lakini alijitahidi kumzua na waligonga kiasi cha kupasuka usoni huku wengi wakijua amefariki kutokana na damu kumtoka, lakini kiubishi akiwa na hali ya Kijeshi alirudi langoni na ndipo TBL wakaamua kumpa mkataba na kuachana na ndoto za kwenda chuo.

 

AKWEPA SAINI YA KIFO MSIMBAZI

Baada ya kuwa langoni na TBL akicheza michezo 30 bila kuruhusu bao, mwaka 1978 klabu ya Simba ikamtaka ajiunge nao sambamba na Hussein Tindwa pamoja na Anania Sangura wote wakitoka TBL.

“Muda huo Simba walikuwa wakijiandaa kucheza na timu ya Racca Rovers ya Nigeria kwenye michuano ya CAF, lakini mimi nikashtua na kukataa kusaini, hivyo nikawashauri na wenzangu tukatae.”

“Sangura alikubali ushauri wangu, lakini Tindwa akagoma na kusaini kucheza Simba, kisha akapangwa kwenye mchezo na Racca Rovers uliochezwa pale uwanja wa Uhuru, basi tulienda kuushudia.”

 

MSHTUKO UWANJANI

Anasema kama kuna kitu ambacho ameshindwa kukisahau maishani mwake ni tukio aliloenda kulishuhudia uwanjani kwenye pambano hilo la kimataifa la Simba dhidi ya Wanigeria.

Anasema kwenye pambano hilo Tindwa alianguka ghafla uwanjani wakati wa mchezo kabla ya kupoteza maisha wakati akiendelea kupewa huduma ya kwanza nje ya uwanja.

“Inasikitisha kwamba Tindwa alikumbwa na mauti, likiwa ndilo pambano lake la kwanza akiichezea Simba. Tukio hilio la kusikitisha lilinifanya niwe nawaza kuwa inawezekana kifo kile kilikuwa kinanihusu mimi, bali kwa vile siku yangu ilikuwa bado ndipo ikamkumba Tindwa, huku Sangura akisema huenda mwenzetu asingejiunga nao kama wao basi mauti yasingemkuta, japo kifo ni siri ya Mungu Muumba anayepanga kila kitu hapa duniani.”

 

KIKOSI BORA

Mbegu anaeleza kuwa alikitumikia kikosi cha TBL kwa muda wa miaka tisa tangu mwaka 1977-1985 kabla ya kujiunga na benchi la ufundi la timu ya Pilsner lakini kikosi chake bora anachokikumbuka daima ni kile cha mwaka 1977.

Kikosi hicho kiliundwa hivi;

1.Maneno Mbegu 2. Kessy Abbas 3. Mwabeshi 4. Ombary Tindwa 5. Alan Shomary 6. Salum Bob Moo 7. Leonard Shitete 8. Salum ‘Carlos’ Mwinyimkuu9. Steven Chibichi 10. Anania Sangura 11. Bakar Mrume

 

USHAURI WAKE

Mbegu anasema enzi zao walijifunza soka kwa kutumia Ubao na Chaki kama wapo darasani, lakini walikuwa na uwezo mkubwa kuliko wachezaji wa sasa ambapo kuna mbinu nyingi za kujifunza, kupitia mitandao, Tv za soka na miundo mbinu pia ni rafiki kwao, vijana wa sasa ila bado wanachemsha.

“Wengi wa wachezaji wa sasa hawana uzalendo mtu anafungwa mbele ya Rais wa Nchi. Sisi ilikuwa ni ngumu kufungwa wakati unajua mzazi wako anakuangalia, vijana na vongozi wa soka wanatakiwa wawe wazalendo kwenye michezo sio lelemala tu.”