Ndugu wengine wanaoweza kuwa wapinzani kwenye soka

Muktasari:

Kwa sababu kulikuwa na Paul Pogba wa Man United akicheza dhidi ya Florentin Pogba wa St Etienne, macho ya wengi yakawa kwa ndugu hao, Pogba wawili kwenye mechi moja.

MECHI ya Europa League kati ya Manchester United na Saint-Etienne ilikuwa ya Pogba dhidi ya Pogba.

Kwa sababu kulikuwa na Paul Pogba wa Man United akicheza dhidi ya Florentin Pogba wa St Etienne, macho ya wengi yakawa kwa ndugu hao, Pogba wawili kwenye mechi moja.

Hivi unajua kwamba kuna Pogba mwingine wa tatu? Huyu anaitwa Mathias Pogba na anacheza soka huko Uholanzi.

Kama Man United siku moja itacheza na Sparta Rotterdam basi kutakuwa na Pogba wawili uwanjani au kama St Etienne ikicheza na Wadachi hao pia itawakutanisha ndugu wawili katika mechi moja.

Hata hivyo, hupaswi kushangaa, kwenye soka kuna ndugu wengi kutoka katika familia moja, mkubwa na mdogo hivi kuna siku itapigwa mechi nyingine itakayowahusisha ndugu wawili wakiwa wapinzani ndani ya uwanja.

Hawa ndio ndugu wengine ambao ipo siku watachuana tu pae timu zao zitakapokutana.

 

Mathias Pogba, kaka yake Paul

Wakati pacha wake Florentin akiwahi kuchuana na mdogo wake, Paul kwenye mechi moja ya Europa League, Mathias naye ambaye ni mshambuliaji katika kikosi cha Sparta Rotterdam ipo siku atakumbana na mmoja wa ndugu zake hao wa familia moja katika maisha ya soka.

Mathias alizaliwa Guinea na sasa akiwa na umri wa miaka 26 aliwahi kucheza soka Uingereza katika klabu za Wrexham, Crewe, Crawley na Partick Thistle kabla ya kutimkia Uholanzi mwaka jana.

 

Paolo Suarez, kaka yake Luis

Straika Luis Suarez kipindi yupo mdogo alipaswa kukua akimtazama kaka yake Paolo, ambaye ni mkubwa kwa miaka sita kwa fowadi huyo wa Barcelona na kipindi hicho alicheza pia kikosi cha walio umri chini ya miaka 20 wa timu ya taifa ya Uruguay.

Ni mfungaji mzuri pia wa mabao kitu ambacho Suarez mdogo anaweza kukirithi kutoka kwa kaka yake mwenye umri wa miaka 36, ametamba sana kwenye ligi za Amerika Kusini na sasa yupo El Salvador akitamba katika kikosi cha Sonsonate.

 

Giliano Wijnaldum, kaka yake Georginio

Unashuhudia shughuli ya Georginio anayofanya kwenye kiungo ya Liverpool msimu huu, kwani anapokosekana tu pengo lake linaonekana dhahiri.

Hata hivyo, ana ndugu pia anayeitwa Giliano Wijnaldum, ambaye pia ana undugu na winga wa Huddersfield, Rajiv van La Parra.

Kama alivyoanza tu ndugu yake kucheza soka la mafanikio makubwa huko kwao Uholanzi na kucheza timu ya taifa ya vijana, Giliano yeye aliamua kuhamia Philadelphia Union inayoshiriki Ligi Kuu Marekani mwaka huu.

 

Felix Kroos, kaka yake Toni

Kiungo wa Real Madrid, Toni Kroos ni bingwa wa Kombe la Dunia na mmoja wa viungo bora kabisa wanaotamba kwenye soka kwa sasa, wakati mdogo wake Felix ni nahodha wa timu ya Union Berlin inayoshiriki Ligi Daraja la Pili ya Ujerumani.

Kuna kipindi alionyesha kiwango kikubwa cha soka na akaichezea Werder Bremen kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini staa huyo mwenye umri wa miaka 25 ameshindwa kuendelea kuonyesha makali ya kiwango cha juu licha ya kuchezea timu sita tofauti za taifa za vijana.

 

Rodney Sneijder, kaka yake Wesley

Familia ya Sneijder inaonekana kupenda sana majina ya kizamani ya Kingereza, ambapo Wesley mdogo wake mwingine Jeffrey anacheza kwenye timu ya vijana ya Ajax sawa na ilivyo kwa mdogo mwingine Rodney.

Rodney alionyesha kiwango bora cha soka na kufikia hatua ya kucheza Ligi Kuu Uholanzi na kuna kipindi fulani aliwahi kuichezea Dundee United mwaka 2015 kabla ya kuachana na timu hiyo na kurudi kwao Uholanzi kutokana na matatizo ya kiafya.

 

Tobias Schweinsteiger, kaka yake Bastian

Kwa muda mwingi wa msimu huu inaonekana kama kaka mkubwa Tobias atakuwa amepiga sana sala kuhusu mdogo wake kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Manchester United.

Kwani Bastian alikumbana na kizuizi kikali kikosini Man United baada ya Kocha wake Jose Mourinho kumshusha hadi katika kikosi cha wachezaji wa akiba.

Bastian alikumbwa na wakati mgumu sana kwenye kikosi cha Manchester United msimu huu kabla ya Mourinho kuanza kumtumia kwenye baadhi ya mechi.

Kaka yake ambaye ni mkubwa kwa miaka miwili fowadi Tobias, maisha yake ya soka amecheza kwenye ligi za chini tu Ujerumani kabla ya kustaafu mwaka 2015 na kuwa kocha msaidizi wa timu ya vijana ya umri wa chini ya miaka 17 ya timu ya Bayern Munich.

 

Jonas Hummels, kaka yake Mats

Kaka hao wawili wote waliondoka Bayern Munich ya Ujerumani walipokuwa na umri mdogo, lakini ni Mats tu ndiye aliyepata kurudi kwenye kikosi hicho cha Allianz Arena.

Mdogo wake Jonas anayecheza kwenye ligi ya chini klabuni Unterhaching hadi kufikia hapo mwaka jana.

Hata hivyo, majeraha yamemlazimu kujiondoa kwenye soka la kishindani sana, lakini huwezi kufahamu, chochote kinaweza kutokea.