Mpasia nyavu anayekosekana Anfield huyu hapa

Muktasari:

Kocha Brendan Rodgers alikuwa na safu yake ya ushambuliaji iliyofahamika kwa kifupisho cha neno SAS kwa maana ya Daniel Sturridge na Luis Suarez ambao ilibaiki kidogo tu waipe timu hiyo taji la Ligi Kuu England misimu mitatu iliyopita. Baadaye, Suarez aliondoka na kwenda kuunda MSN, mtambo wa mabao kwenye kikosi cha Barcelona.

LIVERPOOL ina rundo la washambuliaji mafundi wa mpira na kwamba kitu wanachohitaji ni kumpata tu mtu wa kutupia mipira wavuni.

Kocha Brendan Rodgers alikuwa na safu yake ya ushambuliaji iliyofahamika kwa kifupisho cha neno SAS kwa maana ya Daniel Sturridge na Luis Suarez ambao ilibaiki kidogo tu waipe timu hiyo taji la Ligi Kuu England misimu mitatu iliyopita. Baadaye, Suarez aliondoka na kwenda kuunda MSN, mtambo wa mabao kwenye kikosi cha Barcelona.

Hivyo, basi katika zama hizi za Mjerumani Jurgen Klopp anachopaswa kufanya ni kutengeneza fowadi yake matata na kwa washambuliaji waliopo sasa, anahitaji mtu wa kutupia tu mipira wavuni na hawa hapa wanamfaa sana kocha huyo.

 

Alexis Sanchez

Fowadi huyo wa Arsenal angepaswa kuwa chaguo la kwanza kwenye orodha ya wapya wanaopaswa kusajili wa Klopp klabuni Liverpool. Sanchez anaweza kuwa mrithi sahihi wa Luis Suarez katika kuongoza safu ya ushambuliaji katika timu hiyo ya Anfield, shida kubwa iliyopo ni kama Arsenal watakubali kuuza silaha yao kwa maadui. Uwe na huduma ya Sanchez kwa kasi ile na kisha akacheza pamoja na Philippe Coutinho, Sadio Mane, Adam Lallana na Roberto Firmino fowadi ya Liverpool itakuwa matatizo makubwa kwa safu za mabeki za wapinzani.

 

Alexandre Lacazette

Hakuna ubishi, Lacazette ni aina ya washambuliaji ambao hakika kuna klabu kubwa za Ligi Kuu England zitahangaikia huduma yake mwishoni mwa msimu huu. Kwa muda mrefu Liverpool wamekuwa wakimpigia hesabu za kumsajili. Huduma ya fowadi huyo anayekipiga kwenye kikosi cha Olympique Lyon imetajwa kwamba inaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 35 milioni kitu ambacho kinampa nafasi Klopp kuchanga karata zake na kumsajili fowadi huyo ili kumaliza tatizo la ufungaji katika kikosi chake.

Wale viungo wa Lyon tu Lacazette anatisha, je akicheza kucheza na Coutinho itakuwaje?

 

Javier Hernandez

Hakuna klabu ya Ligi Kuu England ikawa kwenye mshangao kama kutakuwa na timu yoyote ndani ya ligi hiyo itaamua kumsajili Javier Hernandez maarufu kama Chicharito. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho hivi karibuni aliweka bayana kwamba kaka ingekuwa ni yeye asingethubutu kabisa kumpiga bei fowadi huyo ambaye ni makini kweli katika kutimiza wajibu wake wa kupasia nyavu. Chicharito alionyesha hilo kwenye alipokuwa Man United kisha Real Madrid kwa mkopo na sasa yupo Bayer Leverkusen.

Kufunga mabao halijawahi kuwa jambo gumu kwa supastaa huyo wa Mexico, hivyo kama Klopp atafanikiwa kuinasa huduma yake na kwa viungo wale alionao, Liverpool itakuwa moto wa kuukalia mbali.

 

Mauro Icardi

Kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, straika huyo wa Inter Milan, Icardi alidaiwa kukaribia kabisa kujiunga na Liverpool huko Anfield. Uhamisho huo haukutokea baada ya fowadi huyo Muargentina kubadili mawazo yake na kuamua kubaki Italia kuendelea kuwakimbiza.

Uhodari wake wa kutikisa nyavu na uchu wa kuwatesa makipa umemfanya afananishwe na Luis Suarez, huku mabao yake aliyofunga kwenye Serie A msimu huu yakiipa matumaini Inter Milan ya kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Icardi ni moja ya washambuliaji makini wanaosakwa na timu nyingine kubwa ikiwamo Arsenal.

 

Jamie Vardy

Straika huyo wa Mwingereza ni shida anapokuwa kwenye mudi na hakika ameonyesha dhahiri uwezo wake wa kutikisa wavu.

Vardy alikuwa amepungua kasi yake ya ushambuliaji, lakini kwa kiwango chake cha hivi karibuni kufunga mabao manne katika mechi tano za zimeonyesha kwamba bado kuna kitu kinachoweza kuvunwa kwa kutegemea huduma ya staa huyo wa Leicester City.

Vardy ni aina ya mchezaji ambaye Liverpool wanamhitaji kwa sababu ina wapishi wengi wa mabao na mtu ambaye inamkosa ni yule mwenye uwezo wa kutumbikiza mipira wavuni tu, Vardy hiyo kazi anaiweza vizuri kweli kweli.

 

Pierre-Emerick Aubameyang

Straika huyo wa Borussia Dortmund anaweza kuwa lulu kwa kusakwa na timu zote vigogo mwishoni mwa msimu, lakini hakitakuwa kitu cha ajabu kama atanaswa na kocha wake wa zamani.

Klopp alidai anaweza kutumia ukaribu wake na Borussia Dortmund ili kuinasa saini ya fowadi huyo wa Gabon ili akakipige kwenye Ligi Kuu England.

Kuwa na huduma ya Aubameyang unakuwa na uhakika wa mabao 20 kwa msimu, hivyo kama Liverpool itanasa saini yake itakuwa imepiga bao na kuwa tishio kwenye Ligi Kuu England kwa sababu kwa wapishi waliopo klabuni Anfield, akija Aubameyanga atafunga hadi mshangae.

 

Andrea Belotti

Straika, Andrea Belotti alikuwa mjadala mkubwa wakati alipodaiwa kuwa na mpango wa kutua Liverpool kwa ada ya Pauni 19.5 milioni mwaka jana.

Lakini, sasa dau lake limepanda maradufu kiasi cha Arsenal kuambiwa kwamba kama wanahitaji saini ya mchezaji huyo basi watoe Pauni 55 milioni wakati walipojaribu kumsajili kwenye dirisha la usajili. Klabu ya Torino itakuwa ipo tayari kumtoa mshambuliaji huyo kama kutakuwa na dili la maana litakalowekwa mezani huku saini yake haitakuwa rahisi kwa Liverpool kwa sababu kutakuwa na timu nyingine vigogo vitakavyohitaji kumnasa mchezaji huyo mwenye miaka 23.

Hivi karibuni Torino waliweka kipengele cha kulipiwa Euro 100 milioni kwa timu itakayohitaji saini ya Belotti.