Mmemtoa Pluijm? Mmechemka sana

Thursday October 27 2016

 

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm ameamua kubwaga manyanga kuendelea kuinoa timu hiyo baada ya kuenea kwa taarifa kuwa timu hiyo inajiandaa kumleta nchini Kocha George Lwandamina kutoka Zambia abebe mikoba yake.

Ni uamuzi ulioleta mshtuko kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo, ingawa uongozi wa Yanga umeshabariki barua yake ya kujiuzulu.

Lwandamina anayeinoa Zesco United anabebwa na rekodi yake ya kuifikisha timu hiyo kwenye hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kuachana na Pluijm kwa sasa ni uamuzi ambao unatia shaka na huenda ikawa si sahihi kwa kipindi hiki ambacho ndiyo kwanza Ligi Kuu inaanza kupamba moto.

Yafuatayo ni baadhi tu ya majibu ya kwa nini uamuzi wa Yanga kuachana na Pluijm kwa sasa siyo sahihi.

 

Nafasi kwenye Ligi

Pluijm anaondoka huku akiiacha Yanga ikiwa kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu.

Bado kuna mechi nyingi zimebaki ambazo pengine timu hiyo ingeweza kubadili upepo na kutetea ubingwa wake na wala ilikuwa haijafanya vibaya kiasi cha kumhukumu au kufanya uamuzi mgumu kiasi kile.

 

Misimamo

Hans Pluijm ni miongoni mwa makocha wachache ambao walikuwa hawapendi kuyumbishwa kwenye misimamo na uamuzi wanaouchukua.

Ni yeye ambaye alivunja tabia ya baadhi ya wachezaji kujiona mastaa ndani ya kikosi cha timu hiyo na aliondoa tabia ya wachezaji fulani kujimilikisha namba kikosini.

Mfano wa hili ni pale aliporuhusu uongozi wa timu hiyo kuachana na kiungo Haruna Niyonzima baada ya kuchelewa kujiunga na kambi ya Yanga.

Pia Pluijm hivi karibuni, alizuia kusajiliwa kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa kwenye timu yake licha ya vigogo wengi ndani ya Yanga kupigania asajiliwe.

Alikuwa na uzoefu wa soka la Afrika alijua tabia za viongozi, mashabiki na wachezaji ndiyo maana ikawa rahisi kwenda nao sawa.

Misimamo yake ndiyo ilileta mafanikio ndani ya Yanga na kuifanya klabu pekee ya Afrika Mashariki na Kati iliyotinga kwenye nane bora ya Kombe la Shirikisho.

 

Mafanikio

Pluijm anabakia kuwa mmoja wa makocha walioipa mafanikio makubwa Yanga katika kipindi chake alichoinoa.

Ndani ya misimu miwili, Pluijm ameiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, kuifikisha robo fainali ya mashindano ya Kagame, kuipa Kombe la Shirikisho Tanzania (FA) pamoja na kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.

Hata uwepo wake tu ndani ya benchi la ufundi ilikuwa inawatisha timu pinzani na ilifanya kazi ya Yanga kuwa rahisi.

 

Kiboko ya Simba

Akiwa kama kocha mkuu wa Yanga, Pluijm amekutana na Simba mara tano kwenye Ligi Kuu. Katika mechi hizo tano walizokutana, Yanga imeibuka na ushindi mara mbili, Simba wakipata ushindi mara moja huku wakitoka sare mara mbili.

Pluijm ndiye kocha pekee wa Yanga ndani ya kipindi cha miaka 10, kuifunga Simba mara mbili mfululizo ndani ya msimu mmoja ambapo ilikuwa ni msimu uliopita.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kupata tena ushindi kama huo kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

 

Ubabe kwenye Ligi

Huwezi kuwa bora kwenye mashindano ya kimataifa kama hufanyi vizuri kwenye ligi za ndani labda itokee bahati tu kama ilivyokuwa kwa Chelsea msimu wa 2011/2012 ilipotwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiwa imefanya vibaya kwenye Ligi ya Uingereza.

Licha ya kuiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, Pluijm anajivunia rekodi yake nzuri ya kupata ushindi mara nyingi kwenye mechi za ligi hiyo.

Chini ya Mholanzi huyo, Yanga imecheza jumla ya mechi 57 za Ligi Kuu. Katika idadi hiyo ya mechi, imeibuka na ushindi mara 41, kutoka sare michezo 11 na kupoteza michezo mitano ndani ya kipindi cha misimu mitatu.

 

Usajili makini

Kocha ni binadamu na kuna nyakati hufanya makosa hasa kwenye usajili wa wachezaji. Ingawa upo usajili wa baadhi ya wachezaji ambao ni wazi kuwa Hans Pluijm alichemka kama ule wa kiungo Issofou Boubacar, asilimia kubwa ya usajili uliofanywa na kocha huyo umeleta tija ndani ya Yanga.

Mfano wa usajili huo ni ule wa Deus Kaseke, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Vincent Bossou, Andrew Vincent, Hassan Kessy, Juma Mahadh na Malimi Busungu.

Kuna wakati mwingine unaweza kumwamini sana binadamu lakini ukampa majukumu akakuangusha vilevile. Hiyo inatokea haswa kwenye soka.

 

Nafasi kwa vijana

Haijulikani hatma ya wachezaji vijana pindi Lwandamina atapoanza jukumu la kuinoa Yanga lakini ni lazima tuheshimu mchango wa Pluijm katika kutoa nafasi kwa wachezaji vijana.

Pluijm licha ya kukabiliwa na changamoto ya kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na yale ya ndani, alijitahidi kuwapa nafasi vijana.

Vijana wanaojivunia kubebwa na Pluijm ni Geofrey Mwashiuya, Saimon Msuva, Juma Mahadh, Andrew Vincent, Benedictor Tinoco, Juma Abdul, Hassan Kessy, Beno Kakolanya, Pato Ngonyani, Yusufu Mhilu, Deus Kaseke na Said Juma ‘Makapu’.

Ni wazi kuwa Pluijm ameifanyia mambo mengi makubwa na mazuri Yanga ambayo yanamfanya abakie kwenye nyoyo za mashabiki wake ingawa anaachana na klabu hiyo.

 

Mashabiki

Kwa mtazamo wa haraka haraka, kocha huyo anaondoka kama mshindi ndani ya Yanga.

Kitendo cha kuletewa mrithi wake bila taarifa kimewaudhi mpaka mashabiki ambao si wa Yanga, wanaona kama amedhalilishwa.

Ukiondoa Mbrazili Marcio Maximo, Pluijm pia aliweza kurudisha imani ya mashabiki wengi wa Yanga, alikuwa mhamasishaji,ana lugha za kistaarabu na alibeba nembo ya biashara.