Mihela yazua kasheshe Simba

Muktasari:

Mbali na Poppe, taarifa zilidai kwamba vigogo wengine wakiwemo, Kassim Dewji ‘KD’, Crecentius Magori na Mohammed Nassoro ‘Mkigoma’ wametishia pia kujiweka pembeni baada ya kubaini ubabaishaji katika dili hilo ingawa mashabiki wamelipokea kwa mikono

KITENDO cha Simba kusaini mkataba wa udhamini na Kampuni ya SportPesa ya nchini Kenya kimeibua kasheshe ndani ya klabu hiyo huku Bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ akijiweka pembeni na akitaka alipwe deni lake.

Siyo MO tu, vigogo kadhaa wa kamati ya utendaji wameamua kujitoa kwenye uongozi akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kutokana na kutoshirikishwa kwa namna yoyote katika dili hilo.

Mbali na Poppe, taarifa zilidai kwamba vigogo wengine wakiwemo, Kassim Dewji ‘KD’, Crecentius Magori na Mohammed Nassoro ‘Mkigoma’ wametishia pia kujiweka pembeni baada ya kubaini ubabaishaji katika dili hilo ingawa mashabiki wamelipokea kwa mikono miwili wakitamba kwamba Simba itafanya maajabu uwanjani msimu ujao.

Poppe ambaye amekuwa kama mkombozi wa Simba katika nyakati ngumu, kwa kuikopesha timu hiyo pesa, ameamua kubwaga manyanga kwa madai kwamba kuna ubabaishaji mkubwa katika klabu hiyo ambayo inatimiza miaka mitano sasa bila kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Hata kwenye kundi la Whatsapp la kamati ya utendaji Poppe ameamua kujitoa baada ya kutokea hali hiyo na amewatakia viongozi waliosalia kila la heri. Hata hivyo jana hakupokea simu yake kutoka ufafanuzi wa hali halisi.

Mwanaspoti linajua kwamba MO amekereka na uamuzi wa Simba kumpa taarifa siku moja kabla ya kusaini dili hilo huku wakiwa wamekiuka makubaliano waliyokubaliana awali ambayo ni kwamba wajipange na kuweka mambo sawa ndani ya miezi sita ndipo mfumo mpya wa ubinafsishaji uanze kazi.

Habari za ndani zinasema kwamba Simba na MO walikubaliana kuwa uongozi uweke michakato sawa ndani ya klabu pamoja na kufuata matakwa ya kikanuni halafu miezi sita ikishamalizika aichukue timu kwa hisa 51 pamoja na kuiimarisha kimiundombinu na biashara.

MO alikuwa akiikopesha Simba fedha za mishahara na usajili ikiwa ni moja ya makubadiliano ya kuelekea katika mfumo wa hisa uliokubaliwa katika Mkutano Mkuu wa wanachama lakini viongozi hao walimzunguka na kuingia mkataba huo bila kumshirikisha.

Habari zinasema kwamba MO alipanga kwamba atakapoingia rasmi Simba ndani ya miezi sita ijayo aingie na udhamini mnono wa Acacia ambazo habari zinadai kuwa alishakubaliana nao ndio maana akashtuka kusikia Simba wamejifunga kwa SportPesa kwa miaka mitano.

Mwezi uliopita, Rais wa Simba, Evans Aveva alikaririwa na Mwanaspoti kwamba tayari wamepokea kiasi kinachofikia Sh 1 bilioni kutoka kwa MO. Bilionea huyo alikuwa akitoa pia kiasi cha Sh 5 milioni kama posho kwa wachezaji katika kila mechi waliyoshinda.

Tatizo lenyewe

Inadaiwa kwamba viongozi wa Simba waliingia makubaliano na MO kwamba watakuwa wakimshirikisha katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya klabu hiyo wakati ambapo wanaelekea katika mchakato wa mabadiliko kwenda katika mfumo wa hisa.

Hata hivyo, kutokana na ofa ya SportPesa kuwa kubwa, viongozi hao waliamua kufanya mambo yao kimyakimya hadi kusaini mkataba huo Ijumaa iliyopita. Mkataba huo una thamani ya Sh 5 bilioni kwa muda wa miaka mitano.

Aveva alipohojiwa kama mkataba huo ungeashiria kuwa mchakato wa mabadiliko kwenda katika mfumo wa hisa umefikia mwisho, aligoma kujibu swali hilo na kuondoka katika mkutano na waandishi wa habari.

Akijibu taarifa zilizosambaa kwamba MO anadai fedha zake, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema hakuna kitu kama hicho na kwa heshima ya bilionea huyo asingeweza kusambaza taarifa hizo.

“Kwa unavyomfahamu MO (Mohammed Dewji) ni mtu wa kufanya hivyo? Hapana, hakuna kitu kama hicho,” alijibu kwa ufupi Kaburu.

MO aamua kufunguka

Mwanaspoti lilimpata MO jana jioni ambapo alisema; “Simba ni kubwa kuliko MO na Aveva, ninachopambania mimi ni Simba iwe klabu kubwa Afrika. Tunapigania kwa ajili ya Simba, sina ugomvi na kiongozi wala mtu yeyote.

“Sijashirikishwa kwenye jambo lolote katika mkataba huu, viongozi walinipigia simu Alhamisi kwamba Ijumaa watasaini mkataba, nikawaambia wanipe niusome kwanza halafu Jumamosi ndiyo tufikie makubaliano lakini hawakufanya hivyo, matokeo yake Ijumaa nikasikia wamesaini,”alisema MO kwa kifupi.

Kamati yapasuka

Mwanaspoti liliarifiwa kwamba Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imepasuka katika makundi mawili ambapo wajumbe wa kuchaguliwa wameanza kuwapiga vita wajumbe wa kuteuliwa kwamba wao ndiyo wanachochea mabadiliko ambayo hawayataki.

Habari zinasema kwamba wajumbe wa kuchaguliwa wamewatuhumu wenzao wao kutokana na ukweli kwamba kama mabadiliko yatakamilika nafasi zao ndani ya timu zitakuwa hazipo.

Wajumbe wa kuchaguliwa ni Said Tulily, Iddi Kajuna, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmin Badoo. Wajumbe wa kuteuliwa ni Mohammed Nassor ‘Mkigoma’, Musleh Al Ruwaih na Salim Abdallah.

Taarifa zaidi zilieleza kwamba huenda dili la SportPesa lilijadiliwa lakini siyo katika vikao rasmi vya kamati ya utendaji jambo ambalo ndio limechochea mgogoro huo. Wapo baadhi ya wajumbe ambao wamehisi kutengwa.

Habari zinasema kwamba Aveva aliwaita wajumbe wa kamati ya utendaji siku moja kabla na kuwaambia kwamba kesho yake wangesaini mkataba na inadaiwa kuwa walilalamika kuwa kwanini ilikuwa ghafla na hawakuwa na muda wa kupitia kwa kina vipengele vya mkataba.

Kauli ya Aveva

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti mwezi uliopita, Aveva alisema Poppe hawadai fedha yoyote kwani tayari wamemlipa madeni yote na sasa wanajipanga na maisha mapya ndani ya klabu hiyo.

Kauli hiyo inadaiwa kuzua hali ya sintofahamu kwa Poppe ambaye amehisi kwamba kutengwa kwake katika dili hilo kumesababishwa na kulipwa kwa madeni yake wakati yeye ni mtu wa timu.

Ikumbukwe kwamba Poppe alikuwa akisapoti mabadiliko klabuni hapo na alikaririwa akiahidi kununua hisa pindi mfumo huo utakapokamilika, hivyo pengine nalo limechangia kuamua kujiuzulu.

Kauli za Wajumbe

Wajumbe waliozungumza na Mwanaspoti jana walishindwa kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo huku wengine wakiomba muda zaidi ili kuweza kutoa maelezo yao.

Tulily alisema hajafahamu lolote juu ya sakata hilo wala kujiuzulu kwa Poppe. “Nasikia tu hizo taarifa lakini sina uhakika,” alisema Tulily. Kassim Dewji alisema, “Ndiyo kwanza nimetoka nje ya nchi, sifahamu chochote.”

Wajumbe wengine walidai kwamba kuna baadhi yao wamepiga cha juu kinachokadiriwa kufikia Sh200mil ili kufanikisha mchakato huo, hivyo wale ambao walikosa ndio wakavujisha na ndipo kasheshe lilipoanzia.

Mkataba wa SportPesa

Katika udhamini wa SportPesa, Simba inapata Sh 5 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano. Fedha hizo zitalipwa kwa kila mwezi ambapo katika miaka mitatu ya kwanza watapokea Sh 74 milioni na miaka miwili ya mwisho kutakuwa na ongezeko la asilimia tano. Endapo Simba itashinda taji lolote la Afrika itapata bonasi ya Sh 250 milioni huku ikitwaa taji la Ligi Kuu Bara itapewa Sh 100 milioni. Mashabiki na wanachama wa Simba wameufurahia mkataba huo kwa mtazamo wa uwekezaji pamoja na usajili kwamba sasa watakuwa na noti za kununua wachezaji wa maana na wa gharama kama Azam na Yanga.