KUTOKA LONDON: Miaka 10 Emirates, Arsenal bado dhaifu

ARSENE WENGER

Muktasari:

  • Wenger alipoingia England alikuwa mwanamapinduzi, ambapo aina ya mambo aliyofanya yaliigwa na makocha wengine kutokana na uzuri, lakini ameamua kubaki mhafidhina, asiige hata mazuri sana

MIAKA 10 imetimia tangu Arsenal ihamie kwenye uwanja wao wa sasa wa Emirates, lakini bado wamekuwa nyuma ya klabu nyingine kubwa katika usajili. Klabu hiyo ni kama haipendi kutoa fungu kubwa kwa ajili ya kunasa nyota.

Awali ungeelewa, maana kocha Arsene Wenger aliulizwa iwapo anataka kununua wachezaji nyota au wajenge kwanza uwanja mkubwa na mzuri badala ya kubaki Highbury, akachagua hili la pili.

Sasa uwanja ulishakamilika zamani na hata kama ni madeni yalishaisha na klabu wanajiendesha kwa faida kubwa tu na wana wadhamini, lakini bado ngoma imekuwa ngumu kwenye usajili.

Wenger alipoingia England alikuwa mwanamapinduzi, ambapo aina ya mambo aliyofanya yaliigwa na makocha wengine kutokana na uzuri, lakini ameamua kubaki mhafidhina, asiige hata mazuri sana yanayofanywa na makocha wakubwa England. Arsenal itakuwa ngumu kubadilika iwapo Wenger hatabadilika au zaidi sana kuondoka.

Kwa aina ya ubahili walio nao, tangu msimu wa 2006/7 wametumia fedha taslim Pauni 109.2 milioni tu wakati klabu zenye ushindani wa kweli kama Chelsea wamepiga milioni 343, Manchester United milioni 445.2, Manchester City milioni 826.

Kwa sasa Arsenal wana matatizo kadhaa, moja ni kwenye beki hasa ya kati na jingine ni mshambuliaji. Mwanahisa mwenye asilimia 30 kwenye klabu hiyo, Alisher Usmanov huwa hasiti kusema pale anapoona kuna haja.

Mwaka 2012 alisema ilikuwa makosa kumruhusu Robin van Persie, mpachika mabao wao namba moja kuondoka kwenye Man United.

Majuzi alidaiwa kwamba anataka kuuza hisa zake za Arsenal ili akanunue Everton lakini sasa amesema hapana na kwamba kuna haja ya kutumia fedha zaidi kujaza mapengo na kwamba Wenger anatakiwa aungwe mkono.

Kwa aina hii ya utumiaji fedha na kutegemea wachezaji chipukizi au wasio wazuri vya kutosha, itakuwa ngumu kwa Arsenal kumaliza ukame wa ubingwa. Hata faraja ya Kombe la FA walilopata misimu miwili mfululizo liliwaponyoka msimu jana na wamekuwa patupu.

Kama ilivyokuwa miaka miwili iliyopita, msimu huu tena walifungwa kwenye mechi yao ya kwanza na walipigwa na Liverpool nyumbani Emirates. Hawa beki muhimu baada ya Per Mertesacker kuumia, lakini wanataka wampate aliye mzuri kwa bei ndogo, haiwezekani.

Wamemnunua mchezaji mmoja tu mzuri na mwenye uzoefu kiangazi hiki, naye ni Granit Xhaka kutoka Borussia Monchengladbach kwa pauni milioni 35, tena ilikuwa mapema kabisa dirisha lilipofunguliwa, watu wakadhani kwamba usajili mwingi utaendelea, lakini Wenger akaweka ‘breki’.

Baada ya kuzomewa uwanjani kwenye mechi ya fungua dimba, Mfaransa huyu

ameahidi washabiki wenye kiu kwamba atafanya usajili mwingine/mwingine kabla ya dirisha kufungwa. Kwamba atatumia kiasi kikubwa cha fedha kushawishi wachezaji wakubwa au ndio atajazia tu na magarasa hiyo haijulikani.

Alipoulizwa kuhusu mshambuliaji na jinsi alivyowakosa Jammie Vardy na Riyad Mahrez waliokataa kuondoka Leicester, alisema hapendi kuzungumzia sana habari hiyo, akiongeza kwamba huenda akafanya hivyo kwenye kitabu chake kijacho. Yaani watu wasubiri hadi kitabu kiandikwe!

Kadhalika amekuja na jingine, akisema kwamba anaamini mshambuliaji wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez anaweza kuibuka kuwa ‘Luis Suarez’ mpya na hivyo kukawa hakuna haja ya kuna ya kusajili mshambuliaji wa kati. Anaona kwamba anaweza sana kucheza hapo mara kwa mara wakisaidiana na Olivier Giroud, huku katika wingi wakiwamo kina Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain na wengineo.

Beki anatakiwa iwe isiwe lakini yeye anaona mabeki hawatakiwi kuwa ghali na kwamba klabu za England zimekuwa zikiuziwa wachezaji kwa bei kubwa mno. Lakini anashindwa kuelewa au hataki kuelewa kwamba klabu za England ndizo zina fedha nyingi kuliko klabu nyinginezo kwani Ligi Kuu ya hapa ndiyo maarufu zaidi duniani.  Hashangai iweje Manchester City watumie pauni milioni 47.5 kumnunua mlinzi John Stones na Manchester United pauni milioni 30 wakamnasa beki Eric Bailly. Amekuwa akimtaka Shkodran Mustafi wa Valencia, lakini angetakiwa kulipa pauni milioni 30, mazungumzo ya dili hilo yakawa yanaibuka na kufa.

Mara ikaja simulizi la mlinzi wa Atletico Madrid, Jose Gimenez lakini tena mkwanja wanaotaka wa pauni milioni 42 ukamkimbiza Wenger. Sasa anataka kununua watu wa kuwapa ubingwa kwa fedha ya ugoro au ya mboga; hilo aliliona wapi? Hakuna.

Anabisha pia kwamba Alexandre Lacazette wa Lyon hawezi kumnunua kwa Pauni 42 milioni. Hapo ndipo tatizo, unapokuwa na watu wanaothamini zaidi mapato kwa klabu kuliko ubingwa, ambao kimsingi ndiyo malengo ya timu yoyote. Ni sawa na chama cha siasa, lengo la msingi ni kushika dola.

Usmanov anataka usajili wa vipaji vya hali ya juu na boli lipigwe vilivyo huku wakishindana vyema na wapinzani wao wakubwa. Itakuwa ngumu katika wachezaji waliopo, ikizingatiwa saba wana majeraha na wengine wapo nje hadi mwakani, kama Danny Welcbeck na Mertesacker, kufuzu kwa Ulaya na kutwaa ubingwa labda muujiza tu utokee wawe na bahati.