Messi akisepa tu, hawa wametia mguu

NEYMAR DA SILVA

Muktasari:

  • Lionel Messi kama ilivyo kwa binadamu yeyote mwenye mwili wa nyama na damu, ameanza kuzeeka. Mwonekano wa Messi, mwenye umri wa miaka 29, unathibitisha hilo, milango ya June 24 mshikaji atagonga miaka 30. Hapo vipi?

ETI watu huwa wanasema kumwangalia Lionel Messi akicheza ni burudani kuliko  kuwa na mpenzi wako chumbani. Hayo ni maneno ya watu, sina uhakika nayo. Lakini tukiacha utani, jamaa anapiga mzigo hatari. Tangu aingie katika dunia ya soka, Messi amedhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wanasoka bora ambao sayari hii imewahi kuwashuhudia.

Mshindi huyu wa Ballon d’Or mara tano, amekuwa mtu muhimu katika mafanikio ya Barcelona. Akiwa pamoja na wenzake, Xavi Hernandez na Andres Iniesta, walimpa kiburi Pep Guardiola akajiona mmoja wa ‘Miungu’ inayotawala dunia ya soka.

Hata hivyo, ukweli ambao hakuna binadamu anayependa kuukubali ni kwamba, wakati ni ukuta. Huu ni ukweli ambao mashabiki na viongozi wa Barcelona wanatakiwa kuanza kuuzoea.

Lionel Messi kama ilivyo kwa binadamu yeyote mwenye mwili wa nyama na damu, ameanza kuzeeka. Mwonekano wa Messi, mwenye umri wa miaka 29, unathibitisha hilo, milango ya June 24 mshikaji atagonga miaka 30. Hapo vipi?

Siku siyo nyingi Barcelona watalazimika kutafuta mtu wa kuvaa viatu vya Messi. Kama hilo likitokea, jiandae kushuhudia mmoja kati ya wanaume hawa, wakikabidhiwa viatu vya Murgentina huyu, aliyeshindikana.

5. CARLES ALENA

Tunda la La Masia, Carles Alena anatajwa kuwa staa mwingine atakayeutawala ulimwengu wa soka, ambao kwa sasa uko chini ya utawala wa Messi na Ronaldo. Alena anatabiriwa kufanya makubwa pale Camp Nou, miaka michache ijayo.

Tangu ajiunge na Barcelona akiwa na umri wa miaka nane tu, Alena (19), amekuwa akivaa kitambaa cha unahodha katika vikosi vyote vya timu ya watoto ya Barcelona, ikiwemo timu ya watoto chini ya umri wa miaka 12, pamoja na ile ya Barcelona B.

Kiungo huyu mshambuliaji, ana uwezo wa kucheza namba nane au namba 10. Pia ana uwezo wa kucheza katika winga ya kulia na kushoto, kitu kinachomfanya kuonekana kuwa Lulu ya baadaye pale Camp Nou.

Alena ana kipaji cha kusakata kabumbu ambayo ina ladha mchanganyiko wa uwezo wa Messi na Iniesta na kama ataendelea hivi, basi Barcelona hawatakuwa na haja ya kununua kiungo mwengine kuziba pengo la Messi, atakapotundika daluga.

Kitu kingine kinachombeba Mhispania huyu, ni kwamba, anatumia guu la kushoto, maarufu kama mguu wa dhahabu ambao anautumia Lionel Messi. Aidha, uwezo wake wa kutikisa nyavu ni balaa.

4. OUSMANE DEMBELE

Kiungo huyu mshambuliaji mwenye umri wa miaka 19, amekuwa akigonganisha vichwa vya wengi, kutokana na kiwango anachokionyesha msimu huu, katika kikosi cha Borrusia Dortmund.

Kinda huyu, raia wa Ufaransa, alikuwa anamezewa mate na klabu zote kubwa barani Ulaya, lakini Dortmund, ndio waliofanikiwa kuchanga karata zao vyema na kufanikiwa kunasa saini yake.

Amejaaliwa kasi ya umeme, ‘control’ ya mpira, ufundi na utundu wa kuuchezea mpira. Ousmane Dembele, anayejivunia ngozi na damu ya Kiafrika na moyo wa kifaransa, bila ubishi, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Dortmund.

Akiwa anatabiriwa kushinda tuzo ya Ballon d’Or, siku za usoni, Dembele tayari ameshaonyesha nia ya kutamani kuichezea Barcelona na wachambuzi wengi wa soka wanamwona kama mbadala sahihi wa Lionel Messi.

3. PAULO DYBALA

Paulo Dybala, tayari ni Supastaa, katika klabu yake ya Juventus. Inavyoonekana ni suala la muda tu kabla Dybala hajaingia katika orodha ya wachezaji bora duniani. Akifanikiwa katika hilo, itakuwa ngumu kwa Barcelona na Real Madrid, kuacha kummezea mate. Mchezaji huyu, mwenye kasi, ufundi na uwezo wa kuuchezea mpira atakavyo, siyo chini ya mara moja, ameweza kuonesha kuwa, yuko tayari kupigana vikumbo na kaka zake, katika kuutafuta ufalme wa soka, unaoshikiliwa na Messi na Ronaldo.

Huku fununu zikidai kwamba Barcelona na Real Madrid, zimeanza kumkodolea macho, kuna kila dalili ya kumshuhudia Dybala akikipiga pale Camp Nou au hata kukabidhiwa mikoba ya Messi, katika siku za usoni.

2. LEE SEUNG WOO

Wengi wanamtaja kuwa ni chipukizi wa Barcelona mwenye kipaji kikubwa cha kusakata soka zaidi ya Carles Alena. Lee Seung Woo, amekuwa akikonga nyoyo ya mashabiki wengi wa soka pale La Masia, kutokana na uwezo, ufundi na kasi yake, bila kusahau umaliziaji wake.

Akiwa na uwezo wa kucheza kama Straika au kiungo mshambuliaji, Lee Soeung Woo, aliwavutia na Barcelona kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 10, alipomaliza michuano ya Kombe la Danone, akiwa mfungaji Bora.

Barcelona walijikuta wakiwehushwa na kipaji cha Mkorea huyu, wakawa wanahaha kumsajili kiasi cha kujikuta wakilimwa adhabu kwa kukiuka kanuni za usajili za Fifa, zinazozuia usajili wa watoto.

Lee Seung Woo, anafunga kama Messi, anacheza kama Messi na ni ngumu kuwatofautisha wachezaji hawa.

Ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga na kutikisa nyavu. Sifa zinazomfanya kuonekana kuwa katika miaka michache ijayo, ataweza kuvaa viatu vya Messi.

1.NEYMAR

Mbrazili huyu, taratibu anathibitisha kuwa staa wa kesho wa Barcelona.

Anaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Messi na Ronaldo kwenye tuzo za Ballon d’Or, siku za usoni.

Mwaka jana aliingia tano bora lakini akajikuta akiwekwa pembeni katika tatu bora na Messi, Ronaldo na nyota wa Athletico Madrid, Antoine Griezmann.

Baadaye Ronaldo akatwaa tuzo hiyo akiwabwaga Messi na Griezmann.

Magwiji wengi wa soka wanamwona Neymar, kuwa mfalme mwengine atakayetawala ulimwengu wa Soka, baada ya Messi na Ronaldo kutundika daluga.

Wengine wanamtabiria makubwa katika kikosi cha Barcelona, wakiwuona kuwa ndiye mrithi sahihi wa Messi.