Mchezo wa Washua, ila njaa kali

Muktasari:

Mbamba Uswege (marehemu sasa) ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Ligi ya Mpira wa kikapu ya Dar es Salaam (RBA), alifanikiwa kwa kiasi kikubwa japo aliongoza kwa kipindi kifupi kabla ya mauti kumpata kwa ajali ya gari.

       MIAKA zaidi ya kumi iliyopita kila ulipokatisha kona ya Jiji la Dar es Salaam hasa siku za wikiendi, ilikuwa lazima usikie mchezo wa kikapu ukizungumzwa. Hii ni kwa sababu uliteka akili za watu wengi ukiweka kandom soka na Dar ndio ulikuwa mkoa pekee unaotoa wachezaji wengi katika timu ya taifa ya mchezo huo kutokana na ubora wa ligi yake kwa miaka hiyo.

Mbamba Uswege (marehemu sasa) ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Ligi ya Mpira wa kikapu ya Dar es Salaam (RBA), alifanikiwa kwa kiasi kikubwa japo aliongoza kwa kipindi kifupi kabla ya mauti kumpata kwa ajali ya gari.

Enzi za uhai wake, Mbamba alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (DARBA) na alikuwa mdau mkubwa anayestahili kukumbukwa na kuenziwa katika ulimwengu huu wa mchezo huo nchini.

Viongozi mbalimbali walipita kwenye mchezo huu na kuacha mafanikio makubwa ingawa ukiangalia kwa sasa mchezo huo umekosa mvuto ni kama haupo kutokana na ujanja ujanja uliokuwa umeingia kwa baadhi ya viongozi waliotanguliza masilahi yao.

Mchezo huo ulikuwa juu, ulipata wadhamini wa maana wakiwemo TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) kupitia kinywaji chake cha Kiliamanjaro Lager, wachezaji walinufaika mno kupitia udhamini huo kabla ya wajanja kuanza kutafuna pesa pasipo kuangalia masilahi ya mtu mwingine ambaye ni mchezaji. TBL ikasusa kudhamini na hapo ndipo tatizo lilipoanzia.

DARBA inayojitambulisha kwa sasa kama Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD) hakijapata udhamini wa maana, udhamini wao umekuwa wa kuungaunga tu, timu zinakosa hata vifaa ambapo sasa hulazimika kila klabu kuwanunulia wachezaji wao wakati miaka hiyo mdhamini aligharamia kila kitu kuanzia vifaa, usafiri na posho.

Mwanaspoti ilifanya mahojiano maalumu na Mwenyekiti wa BD, Okare Emesu, ambaye ni nyota wa zamani wa Oilers, aliyezungumza mambo mbalimbali kuhusiana na mchezo huo hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

KUPOROMOKA

Okare anasema kuporomoka kwa kikapu kumetokana na mfumo mbovu wa uongozaji na watu kutojitolea hasa kwa wachezaji wakongwe ambao walistahili kuupigania mchezo huo ili uendelee kuwa kwenye kiwango bora.

“Kulikuwepo na motisha nyingi siku za nyuma ambazo hazikudumu, kwani mfumo wa uongozi inawezekana ulikosewa na kuwakimbiza wadhamini mbalimbali ambao walikuwa wanadhamini hii ligi ama mpira wa kikapu kwa ujumla.

“Sitaki kuwalaumu, ila kikubwa kinachopaswa kufanywa ni kuupigania urudi katika ubora wake kama ilivyo michezo mingine maana kikapu enzi hizo ulipendwa miongoni mwa vijana, kila mmoja ana jukumu la kurudisha mchezo wa kikapu, mpira wa kikapu haujafa ila hauna msisimko kama miaka ya nyuma,” alisema Okare.

UDHAMINI

Okare bado analia na wadhamini, japo anafahamu mdhamini yeyote hawezi kuwekeza sehemu ambayo haieleweki kwani naye huogopa kuingia hasara.

“Kampuni mbalimbali huwa tunazifuata kuzungumza nazo, lakini swali kubwa tunalokutana nalo ni jinsi gani itanufaika wakati mchezo wenyewe hautangazwi wala kujulikana sana hapa nchini. Ni swali gumu kwetu ila tumeanza kuelewa namna gani tuutangaze mchezo ili tuwapate hao wadhamini,” anasema.

“Njia pekee ya kuutangaza na kujulikana ni kupitia vyombo vya habari kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kikapu kimeporomoka na hakuna chombo cha habari ambacho kilijali hilo, sasa tumeanza upya na tunaona vyombo vya habari jinsi vinavyotoa ushirikiano kwetu, tunaamini udhamini utakuja.”

AZAM TV

“Azam TV hawajawa wadhamini rasmi bali wametupa fursa ya kurusha matangazo yetu ya mechi kila tunapocheza, inasaidia kuwajulisha wananchi kinachoendelea kwenye kikapu. Tulizungumza na NMB, T-Marc lakini bado hatujafanikiwa ingawa kuna mwelekeo kidogo,” anaongeza.

“Mfuko wa jamii wa PSPF wamejitokeza kutudhamini kuanzia mzunguko wa pili, hivyo hatutakuwa na tatizo sana ingawa bado tunahitaji udhamini zaidi ambao utakidhi mahitaji yetu ikiwemo kusaidia timu, tukipata udhamini mkubwa tutaweza kusaidia vifaa, kulipa angalau posho kwa wachezaji, usafiri na zawadi ya fedha kwa washindi maana hivi sasa hakuna,” alisema Okare.

MALIPO YA WAAMUZI

Okare anafafanua kuwa, Dar es Salaam ina waamuzi 45 wakiwepo wapya 30 na wa zamani 15.

“Kila tunapokuwa na mechi ambapo mara nyingi tunacheza wikiendi huwa tunakuwa na waamuzi zaidi ya 10 kulingana na mechi zenyewe zinazochezwa. Kunakuwepo waamuzi wanne wa mezani na kamisaa mmoja wa mchezo pia.

“Kila mwamuzi anayechezesha mechi moja hulipwa Sh 10,000 hiyo ni hata kwa wale waamuzi wa mezani, kamisaa wa mchezo peke yake ndiye hulipwa pesa nyingi Sh 15,000. Ni pesa ndogo kulingana na jinsi walivyosoma, muda wanaotumia pamoja na ugumu wa kazi ila inatubidi tushirikiane nao kulingana na hali halisi iliyopo,” alisema.

RUZUKU

FIBA/SERIKALINI

Serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwa vyama vya michezo japo kwa miaka ya karibuni ruzuku hiyo imekuwa tatizo kuvifikia vyama husika kutokana na bajeti ya serikali ingawa upande wa FIFA (soka) ruzuku yao hufikia kwenye mashirikisho ya mchezo huo.

“Tunaamini kwamba serikali haijashirikishwa sana kwenye upande wa michezo na hata kama imeshirikishwa basi kwa baadhi ya mchezo ndiyo hunifaika tofauti na huku kwetu. Ruzuku ya FIBA (shirikisho la kikapu la kimataifa) huwa inafikia kwenye mikono ya shirikisho la taifa (TBF) hivyo tunanufaika na hicho kidogo kama vifaa hasa mipira,” anasema.

AHADI YA SERIKALI

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilitoa ahadi ya ujenzi wa viwanja vitatu vya mchezo wa mpira wa kikapu ambavyo vitakuwa katika wilaya tatu, Ilala, Temeke na Kinondoni.

“Wakati wizara hii ipo chini ya Nape Nnauye, alituahidi kutujengea viwanja vitatu vya kisasa ambavyo tunaamini hata kwenye huu uongozi mpya vitatekelezwa. Uwanja wa Ndani wa Taifa utakarabatiwa, vingine vitakuwa Gymkhana ambapo ni wilaya ya Ilala na Kinondoni tumepewa eneo la Uwanja wa Tanesco.

“Tukiwa na viwanja vya kisasa naamini heshima itarudi, kwani kuna uwanja pale JK Park lakini ule unafaa kwa ajili ya watoto, hauwezi kuhimili vishindo vya wakubwa kwani timu za wakubwa zikicheza pale ni rahisi kuumia tofauti na uzito wa vijana ambapo wakidondoka maumivu yao yanakuwa madogo.

“Tunaomba sana serikali izingatie hilo maana huu Uwanja wa Ndani unatupa changamoto kubwa na mara nyingi umekuwa ukiharibu ratiba hasa kipindi hiki cha mvua ambapo mabati yake yameoza na hivyo kuvuja,” alieleza Okare.

UKATA MKALI

“Tulibadilisha akaunti ya benki kwa sababu uongozi ulikuwa mpya na baadhi ya viongozi wa zamani hawakuwepo wakati wa makabidhiano, hivyo hatukuona sababu ya kuendelea kusubiri wakati huo akaunti haina hata pesa japo hata sasa pesa inayoingia huko ni ndogo tu,”.

Okare alisema vyanzo vya mapato kwenye chama hicho vinatokana na ada ya usajili ambapo kila mchezaji hulipa Sh5,000 kwa mwaka ambapo kila timu inatakiwa kusajili wachezaji 20, za wanaume katika ligi hiyo zipo 16 wakati wanawake ni nane.

Chanzo kingine cha mapato kinatokana na ada ya ushiriki kila klabu inapaswa kulipa Sh 100,000, ada ya uanachama ni Sh100,000 kwa klabu, zile zinazochelewa kulipa ada hizo faini yake sasa imepanda hadi Sh300,000 kutoka Sh150,000.

“Hapo kuna timu ambazo hushindwa kulipa ada hizo, hivyo uendeshaji bado unakuwa mgumu, hii yote hutokana na kukosa udhamini na ligi kutokuwa na ushindani mkubwa unaowafanya wadau wawekeze,” alisema Okare.

MIKATABA

Hivi sasa mchezaji wa kikapu anaweza kuhama timu kwa kununuliwa viatu tu na kiongozi wa timu nyingine, habanwi na anaruhusiwa kwa sababu hana mkataba na timu ya awali lakini BD wamegundua tatizo hilo kwamba husababisha kutokuwepo na nidhamu kwa wachezaji.

“Tumetengeneza mikataba kwa kila mchezaji, tumewapa maelekezo viongozi wa klabu zote kuwa kila mchezaji anapaswa kuwa ndani ya mkataba utakaomwongoza na kumfanya aheshimu kazi yake. Mchezaji atasaini mkataba wa miaka miwili ingawa FIBA wanaruhusu mkataba wa mwaka mmoja.

“Hiyo itasaidia kwa pande zote tatu, mchezaji, klabu na chama kwani taratibu za uhamisho kama anahitaji na timu nyingine zitafuatwa kwa kulipa gharama endapo atakuwa na mkataba na timu yake ya mwanzo, timu italipwa, mchezaji atalipwa na baadaye chama kuna ada italipwa kwa ajili ya uhamisho huo.

“Tunahitahi pia kila klabu iwe na uwanja wake wa mazoezi, wawe na vifaa vya mazoezi, wasimamie vifaa vya mashindano kwamba kila mchezaji awe kwenye sare husika, benchi la ufundi lenye vigezo vyote vinatakiwa na FIBA,” anafafanua.

WAMEJITENGA

NA SOKA

Soka ni mchezo unaochezwa hata na mtu mwenye uwezo wa chini na ndiye hasa anatajirika kutokana na jinsi soka linavyoongoza kwa kupendwa ulimwengu kote tofauti na mpira wa kikapu ambao unaonekana kuchezwa na vijana waliotoka kwenye familia bora lakini huishia kuwa masikini.

“Soka huchezwa sehemu yoyote hata kwenye mchanga, lakini kikapu ni lazima uwanja uwe na simenti, magoli, mchezaji awe na viatu aina ya ‘sniker’ ambavyo vinamsaidia mchezaji kuruka na kutua eneo ambalo ni gumu pasipo kuumia.

“Ili upate vifaa vya mchezo huo ni lazima uwe na uwezo mkubwa wa kifedha kwani vifaa vyake ni gharama, pia unaonekana mchezo wa matajiri kwasababu viwanja vingi vya mpira wa kikapu vipo kwenye mashule na vyuoni hizo ndizo sehemu sahihi unazoweza kupata maeneo bora ya kucheza.”

MIPANGO YAO

“Tunataka kuwekeza zaidi kwa vijana kuanzia mashuleni ambapo Balozi wetu wa Kikapu, Jokate Mwegelo anaendesha kampeni hiyo na tumeomba viwanja katika shule tatu, Mbagala Kuu, Mtakuja na Chuo cha Usafirishaji Mabibo.

“Tayari tuna Ligi za vijana ambazo zinahusisha Shule za Sekondari (SBL), Ligi ya Junior NBA inayochezwa JK Park na Kliniki nyingine za vijana ambazo zinasimamiwa na Mambo Jambo club na Mudy Mchenga Clinic, tunaamini malengo yatatimia na kuwa na vijana wenye uwezo mkubwa kwani wanafundishwa wangali bado wadogo.”