BASSOGOG : Mchezaji bora Afcon 2017, anasakwa kila kona Ulaya

Saturday February 11 2017Christian Bassogog

Christian Bassogog 

CAMERON imechukua ubingwa wa Afcon ikiwaacha midomo wazi mashabiki wengi wa soka barani Afrika. Moja kati ya chachu ya ubingwa huo ni kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Christian Bassogog.

Haikuwashangaza mashabiki wakati alipotangazwa kuwa Mchezaji Bora wa michuano baada ya pambano la fainali dhidi ya Misri. Bassogog ametokea wapi?

AZALIWA MJI MMOJA NA ETO’O

Jina lake kamili ni Christian Mougang Bassogog na alizaliwa Oktoba 18, 1995 katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Cameroon, Douala. Mji huo unasifika kwa kutoa wanasoka wengi mahiri wa Cameroon kama vile, Samuel Eto’o, Alexandre Song, Patrick Mboma, Eric Djemba-Djemba, Timothee Atouba na wengineo.

Alianza kucheza soka katika klabu ya Rainbow FC ya kwao Cameroon ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili. Alikuwa katika timu yao ya vijana. Novemba 2014 alikuwa miongoni mwa vijana 40 waliopangwa kutazamwa na Meneja Mkuu wa klabu ya Wilmington Hammerheads ya Marekani, Jason Arnold pamoja na wakala wa Marekani, Leo Cullen.

ATIMKIA KUKIPIGA MAREKANI

Baada ya kuwafurahisha watu hao, Aprili 29, 2015 Bassogog alikwenda kujiunga na klabu ya Wilmington Hammerheads ya Marekani. Akiwa na klabu hiyo, Bassogog alikuwa mchezeshaji zaidi huku akicheza mechi 16 na kupika mabao mawili.

Baadae klabu yake iliwasiliana na kampuni moja ya uwakala ya Hispania kwa ajili ya kuwatafutia timu wachezaji ambao walikuwa na tamaa ya kwenda kucheza soka la kulipa barani Ulaya na hapo ndipo klabu ya AaB ya Denmark ilipomuona.

ATUA DENMARK

Agosti 28, 2015 Bassogog alisaini mkataba wa miaka minne na klabu ya AaB. Alicheza pambano lake la kwanza Septemba 29, 2015 katika mechi ya Kombe la Denmark dhidi ya Lystrup IF. Aliingia uwanjani katika kipindi cha pili ikiwa imebakia nusu saa kabla ya pambano hilo kumalizika.

Februari 11, 2016 wakati Ligi Kuu ya Denmark ikiwa mapumzikoni, Bassogog alichaguliwa kucheza mshambuliaji katika pambano la kirafiki dhidi ya FC Sioni Bolnisi ya Georgia. Alifunga mabao mawili katika pambano hilo na kocha wa zamani wa timu hiyo, Lars Sondergaard alidai kwamba katika siku za usoni angemtumia mchezaji huyo kama mshambuliaji badala ya winga.

Februari 29, 2016 alicheza pambano lake la kwanza la Ligi Kuu ya Denmark dhidi ya FC Midtjylland. Aliingia uwanjani dakika 10 za mwisho za pambano hilo.

ATESA NA JEZI YA CAMEROON

Bassogog ameichezea Cameroon katika kipindi kifupi na kupata mafanikio. Aliitwa na kocha, Hugo Broos kwa mara ya kwanza katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia Novemba mwaka jana.

Kocha Broos akiwa nchini Gabon wakati michuano ikiendelea alikiri kwamba miezi sita tu iliyopita alikuwa hamfahamu mchezaji huyo na alimjua baada ya kuulizia kwa rafiki zake waliopo nchini Dwenmark ambao walimpa taarifa nzuri.

“Kama ungeniuliza miezi mitano iliyopita ‘Unamjua Bassogog? Ningekuuliza ‘Ni nani huyo?’ Sikumjua. Tulikuwa tunatafuta wachezaji. Nina rafiki zangu ambao ni wachezaji wenzangu wa zamani pale Denmark kwahiyo niliwapigia simu nikasema ‘Naona kuna huyu mtu anaitwa, Bassogog, ni mchezaji wa aina gani? Baadaye nikaenda kumwona na nikaona ubora wake, nikasema ‘Mechi ijayo atakuwa na sisi’.

Baada ya hapo, kocha aliridhishwa na kiwango chake kiasi cha kuitwa katika kikosi cha Cameroon ambacho kingeshiriki michuano ya Afcon nchini Gabon Januari mwaka huu. Ni katika michuano hiyo ndipo Bassogog alipotangaza jina lake zaidi.

Alianza katika mechi zote sita za michuano hiyo huku akisifika zaidi kwa kasi yake, akili yake na maono yake katika mpira.

Alifunga bao zuri la dakika za mwisho katika pambano la nusu fainali dhidi ya Ghana akimalizia shambulizi zuri la kushtukiza la timu yake. Cameroon ilishinda 2-0.

Mwishoni mwa michuano hii, Bassogog alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza wa Cameroon kuchaguliwa kuwa mchezaji bora tangu mlinzi Rigobert Song alipofanya hivyo katika michuano ya mwaka 2002.

Baadhi ya wachezaji waliowahi kuchaguliwa katika tuzo hiyo walifanikiwa kufanya mambo makubwa baadaye katika soka. Mastaa hao wa Afrika ambao walifanya makubwa baada ya kutwaa tuzo hiyo ni pamoja na Austin Okocha, Abedi Ayew, Christian Chukwu, Benni McCarthy na Rabah Madjer.

ASAKWA NA KLABU MBALIMBALI

Kutokana na kuonyesha kiwango kikubwa na Cameroon nchini Gabon, Mkurugenzi wa ufundi wa AaB, Allan Gaarde alidai kwamba klabu mbalimbali kutoka katika Ligi za England, Hispania na Italia zilikuwa zimeonyesha nia ya kumchukua.

Hata hivyo mpaka dirisha la Januari linafungwa hakukuwa na timu ambayo ilitoa dau kwa nyota wao huyo wa Cameroon ingawa inatarajiwa kuwa mwishoni mwa msimu huu katika dirisha la majira ya joto kutakuwa na ofa mbalimbali.