Mavugo: Mademu wa Bongo hawanipati ng’o -1

Muktasari:

Ndiyo kuna filamu tamu sana inaendelea kwa sasa. Ilianzia kwa yule Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu kilichotajwa vita ya dawa za kulevya, ikahamia sakata la kufoji vyeti, ikaingia uvamizi wa studio za Clouds FM, kisha ikaendelea kutenguliwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Nape Nnauye na sasa ipo kwa Nay wa Mitego, sijui filamu hii kali itaendeleaje. Tuachane na hayo.

WAKATI akili za Watanzania wengi kwa sasa zimesombwa na yanayoendelea kuhusu kukamatwa kwa msanii Nay wa Mitego kwa tuhuma za kuimba wimbo wa kuikashifu serikali katika filamu iliyoanzia kwenye vita ya dawa za kulevya, straika matata wa Simba, Laudit Mavugo, yeye wala hana taimu na mambo yenu hayo. Anazidi kupanga mikakati ya kutoboa mbele zaidi na soka lake.

Ndiyo kuna filamu tamu sana inaendelea kwa sasa. Ilianzia kwa yule Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu kilichotajwa vita ya dawa za kulevya, ikahamia sakata la kufoji vyeti, ikaingia uvamizi wa studio za Clouds FM, kisha ikaendelea kutenguliwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Nape Nnauye na sasa ipo kwa Nay wa Mitego, sijui filamu hii kali itaendeleaje. Tuachane na hayo.

Mavugo ni miongoni mwa wachezaji ambao ni habari ya mjini kwa sasa katika soka la Ligi Kuu Bara, hii ni kutokana na kufanya kwake vizuri.

Ni jioni tulivu kabisa Jumamosi iliyopita, pale Mwanaspoti lilipoamua kutia timu nyumbani kwa Mrundi huyo, Sinza Mori, jijini Dar es Salaam. Anaishi katika bonge la ‘Apartment’ alilopangishiwa na matajiri wa Wekundu wa Msimbazi. Ni pale karibu na hoteli ya Wanyama.

Ilikuwa siku ya mapumziko kwake na alikutwa akiwa ametulia akisikiliza muziki huku akinywa wine nyekundu. Alikuwa anapumzisha akili haswa.

Ukifika katika ‘Apartment’ hiyo, mara moja utabaini wanaoishi hapo wote wapo vizuri. Kwanza kuna mandhari ya kuvutia, ndani ya geti kuna magari ya kifahari tupu yamepaki. Kuna Hammer mwanangu, Harrier za kutosha tu na mengine yanayotamba mjini.

Getini yupo mlinzi. Aliweka ubishi kidogo kuliruhusu Mwanaspoti kuingia ndani, hata hivyo haikuwa shida sana kwani hadi gazeti hili linafika hapo, kulikuwa na mawasiliano na mchezaji huyo.

‘Apartment ‘ aliyopangiwa ni nyumba inayomtosheleza. Kuna sebule, jiko, chumba cha kulala kilichojitosheleza kwa maliwato. Hizo samani sasa, seti ya televisheni ya kisasa, sofa zilizoenda shule na friji ya wastani iliyosheheni vinywaji vya kila aina, maziwa, matunda na mapochopocho mengine.

 

MAISHA YA NYUMBANI

“Hapa ninaishi peke yangu, familia yangu yote ipo nyumbani (Burundi). Kwetu nimeacha mke ninayempenda sana, anaitwa Paulet Inamahoro, amebaki kule na wanangu; Tayla (6) na Inaya (1),” anasema Mavugo aliyeishi na mkewe huyo kwa miaka saba sasa.

“Nilikwambia uje tu kwa kuwa mimi hutulia tu nyumbani katika siku za mapumziko, sipendi kuzurura mjini. Kama hatuna mechi, hatupo mazoezini huwa napumzika, kazi yangu inahitaji nipumzike.”

Mavugo ambaye pia ni mpenzi wa kuangakia Azam TV akifuatilia habari za michezo, anasema hufanya shughuli nyingi za nyumbani mwenyewe, ila mara moja moja huwapa watu pesa wamsaidie kufua, kusafisha nyumba na kupika.

Jamaa ni ni mtu wa watu, kipenzi kikubwa cha watoto wa eneo hilo kwani awapo nyumbani, hawabanduki kwake, wanamrukia na kucheza naye bila wasiwasi na yeye anakiri kuwapenda mno.

 

AlivyomnasWa penzi la mkewe

Anasema: “Ilikuwa kama mchezo hivi. Awali sikuwa namfahamu Paulet, lakini alikuwa anafahamiana na marafiki zangu aliokuwa anasoma nao. Siku iliyochokoza mambo nilikuwa nimewasindikiza hao jamaa zangu kwao, ndipo nilipomwona na kwa kweli moyo ulifanya ‘paa’.” Huku akicheka, akaendelea: “Kuna stori ndefu hapo ikafuata, lakini ndiyo hivi hadi leo tupo pamoja na tumeanzisha familia.

“Nampenda sana mke wangu. Ni mrembo na huwa sichoki kumtazama, ni mrefu wa wastani, mnene kidogo na rangi yake ni maji ya kunde. Kwenye tabia katulia sana, hapo ndipo aliponiroga zaidi.”

 

Mkewe Kuhamia Dar?

Mavugo ambaye anaishi karibu na wachezaji wengine wa Simba; Juuko Murshid raia wa Uganda na Mzimbabwe Method Mwanjali, anasema mkewe amekuwa akitamani sana kuja Tanzania, lakini amebanwa na masomo.

“Kwa sasa anasoma chuo,” anasema Mavugo na kufafanua mkewe huyo kitaaluma ni Daktari. “Hata hivyo siyo mbaya, wakati ukifika atakuja tu inaweza ikawa mara moja kama kutembea.”

 

Ameshawahi kumpiga mkewe?

Kwenye ndoa huwa kuna mengi. Wapo ambao ndoa zao hugeuka kuwa shubiri baada ya muda fulani. Kuhusu yeye, anasema: “Sijawahi kumpiga mke wangu na sitarajii, nadhani ikitokea siku hiyo nitalia sana.

“Kweli kuna kutofautiana kwa hapa na pale, lakini siyo kwa kiwango cha kukunjiana ngumi kwani huwa tunasikilizana sana,” anasema Mavugo ambaye ni shabiki wa FC Barcelona ya Hispania na Liverpool ya England.

Alipoulizwa kama alishawahi kuisaliti ndoa yake, kidogo aligeuka mtata kujibu swali hilo, kisha akasema: “Tuachane na swali hilo.”

 

Mitaani harembi bwana

“Kwa jumla mimi ni mtu mwelewa, sipendi ugomvi. Nipo hivyo hata kwa watu wengine. Sina historia ya ugomvi.

“Kule kwetu mitaani ikitokea mtu amenichokoza, huwa najifanya mjinga. Lakini kama atazidi sana lazima mambo yatabadilika na ugomvi wangu ili uishe mpaka nione damu ya mtu ndiyo nitaacha, hata hivyo tangu nije hapa Tanzania sjapata shida na mtu.”

 

Mademu wa Bongo

Anasema: “Unajua mimi ni mwanaume rijali, halafu ni maarufu, sasa mademu wananifuata sana, lakini najua ni changamoto tu. Wapo wanaonipigia simu, wengine wananifuata kabisa, lakini kwa sababu najitambua, hawawahi kunizidi akili. Unajua nikiwaendekeza nitalimalizia soka langu hapa.

“Nimeshazisikia habari za wanawake wa Dar es Salaam, hasa wale wa kimjini jinsi wanavyowamaliza wachezaji, hawatanipata. Nimekuja hapa kutafuta maisha na si starehe.”

 

Starehe yake sasa

Straika huyo anasema anapokuwa mapumziko, starehe yake kubwa ni kwenda ufukweni.

“Napenda kwenda bichi, huko nainjoi sana kwa sababu nitaogelea na kupata upepo mzuri, nikiwa nyumbani huwa nakwenda na mke wangu,” anasema Mavugo ambaye alishawahi kufanya majaribio ya soka la kulipwa Ufaransa.

 

Bongo yeye na Uwoya tu

Anasema huwa anafuatilia filamu za wasanii mbalimbali. Kwa Bongo anapenda kuangalia zaidi zile za kuchekesha kama za King Majuto na Joti, lakini zile za hadithi huwa anafuatilia mara chache na msanii anayempenda zaidi kuliko wote ni Irene Uwoya ambaye pia ni mke wa Mrundi mwenzake, Hamad Ndikumana.

“Majuto na Joti wanachekesha sana, lakini Uwoya ni msanii anayefiti sehemu yoyote ya filamu, anaigiza mwanafunzi, daktari, mwanakijiji, wa mjini yaani kote anaweza, ndiyo maana nampenda,” anasema.

Kimuziki anamzimia Diamond akimtaja kwa jina la Simba. Pia anasikiliza kazi za Ali Kiba, Darasa na Man Fongo. Kwa wanawake anapenda nyimbo za Mwasiti na Lady JD.

 

Utamu bado, itaendelea keshokutwa Alhamisi atakapokujuza mengi zaidi.