Matumla hakuna namna tena

Muktasari:

  • Katika pambano hilo Matumla aliyekuwa akipambana na Mfaume Mfaume, alianguka na kuzimia ulingoni kabla ya kukimbizwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji kuokoa maisha yake na mapema wiki hii aliruhusiwa kutoka hospitalini.

MPAKA sasa haamini kama bado yu hai, hata wazazi wake nao licha ya kumshukuru Mungu kwa kudra zake, wanasisitiza kuwa mtoto wao, Mohammed Matumla ‘Snake Boy Jr’ hatapanda tena ulingoni kuzipiga.

Bondia huyo machachari na mtoto wa bingwa wa zamani wa Dunia wa WBU, Rashid Matumla ‘Snake Man’, analazimika kuachana na ngumi kutokana na tukio lililomkumba ulingoni Februari 5 mwaka huu katika pambano lake.

Katika pambano hilo Matumla aliyekuwa akipambana na Mfaume Mfaume, alianguka na kuzimia ulingoni kabla ya kukimbizwa hospitalini na kufanyiwa upasuaji kuokoa maisha yake na mapema wiki hii aliruhusiwa kutoka hospitalini.

Kipi kilichotokea

Matumla Jr amesimulia kilichotokea kwenye pambano hilo ambapo limezua hofu kubwa kwa mabondia wengine namna mchezo huo ulivyo hatari na unavyoweza kupoteza uhai wa bondia ghafla kama utani.

Bondia huyo alibainika kuwa amepata ufa kwenye fuvu lake la kichwa na kama angecheleweshewa matibabu hali ingekuwa nyingine, lakini kwa sasa yu salama akiendelea kujiuguza nyumbani kwao Keko Magereza, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza juzi Jumatano nyumbani kwao, bondia huyo anasema kabla ya kupoteza fahamu alichezewa faulo na mpinzani wake Mfaume Mfaume aliyedai alimpiga kichwa.

“Nilichukizwa na kitendo kile nikawa nashuka ulingoni ili niondoke baada ya kufanyiwa faulo,” anasema Matumla Jr ambaye hata hivyo ameshauriwa kwa sasa asiwe anazungumza kwa muda mrefu kwani familia yake inasema akifanya hivyo anapoteza kumbukumbu.

Hata hivyo kabla hajatoka ukumbini, baba yake ambaye pia ni kocha wake, Rashid Matumla alimrudisha ulingoni.

Msikie baba mtu sasa

“Nilimrudisha ili matokeo yakatangazwe akiwepo ulingoni kwani tayari alikuwa amekataa kuendelea, kweli alirudi lakini hakuendelea ndipo kutahamaki akaanguka na kupoteza fahamu,” anasema baba mzazi.

Astaafu ngumi

Licha ya madaktari wa Taasisi ya Mifupa (MOI) kumtaka kutopigana kwa miezi minane hadi 12, lakini bondia huyo pamoja na wazazi wake wamesema wazi kuwa hatocheza tena ngumi.

“Kwanza naangalia afya yangu, lakini ngumi tena hapana siwezi kuendelea,” anasema Matumla ambaye ameruhusiwa kutoka hospitali na kurejea nyumbani tangu Februari 21.

“Kama baba yake nasema hata akipona hatapigana, tayari keshapata kovu na ngumi ni mchezo ambao naujua nimeucheza ukishaumia hata ukipona unakuwa katika hatari kwani ukipigwa katika jeraha hilo ndio basi tena,” anasema baba yake kuonyesha msisitizo kwamba mwanaye hatacheza tena.

Mama asisitiza

Mama mzazi wa Matumla Jr, Jane Mhagama, anasisitiza mwanaye kutakiwa kuwa katika sehemu tulivu ili aweze kuimarika.

“Haruhusiwi kuzungumza kwa muda mrefu, mengine juu ya afya yake niulize mimi (mama) sababu anapozungumza muda mrefu anakuwa anapoteza kumbukumbu na madaktari wamenisisitiza niwe mkali kwenye hilo,” anasema.

Neno la Mbwana

Ukoo wa Matumla ni watu wa ngumi kweli, wakati napiga stori na Matumla, baba mdogo wa bondia huyo, Mbwana Matumla ‘Golden Boy’ naye alikuwapo na kutoa neno lake.

Mbwana anasema tatizo la kupoteza kumbukumbu la mwanaye huenda likachukua miezi miwili hadi mitatu kisha kuja kuisha kwa mujibu wa madaktari, ndio maana wanataka mtoto wao awe kwenye utulivu atengemae kiafya.

Rekodi za Matumla

Matumla amecheza jumla ya mapambano 26 tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa mnamo mwaka 2010, ambapo ameshinda mapambano 16 manne yakiwa ya KO.

Pia amepoteza mapigano matano, mawili kati ya hayo yakiwa ya KO likiwamo hilo la mwisho dhidi ya Mfaume na michezo mingine mitano ametoka sare.