Mashabiki hawa noma sana

Muktasari:

Hata hivyo hilo linawezekana likafanywa na watu wengine, lakini hii sio wapenzi na mashabiki wa soka. Jamaa wa soka achana nao kabisa, sio watu wa kuwatania kabisa kwani wako tayari kufanya jambo lolote ilimradi waridhishe nafsi zao.

MWANAMUZIKI Lameck Ditto ameimba maneno mazito katika wimbo wake wa Moyo Sukuma Damu, akiwa na maana upo uwezekano wa binadamu akabishana na moyo wake na kuacha kile anachokipenda.

Hata hivyo hilo linawezekana likafanywa na watu wengine, lakini hii sio wapenzi na mashabiki wa soka. Jamaa wa soka achana nao kabisa, sio watu wa kuwatania kabisa kwani wako tayari kufanya jambo lolote ilimradi waridhishe nafsi zao.

Wapo wanaofikia kutoa mpaka nyumba, magari na hata kuhatarisha uhai wao kwa sababu ya mahaba mazito waliyonayo katika soka na hasa klabu wanazozishabikia.

Hapa nchini hakuna siri, klabu zinazopendwa mno ni Simba na Yanga na pengine Azam ambazo nazo bwana asikuambie mtu zina mashabiki lia lia sio mchezo.

Miaka kadhaa nyuma kulikuwa na shabiki mmoja matata aliyekuwa akiishabikia Reli-Morogoro akijichora mwili mzima aliyefahamika kwa jina la Ya Mungu.

Achana na Ya Mungu ambaye kwa sasa ni marehemu, kwa sasa kuna mashabiki waliojizolea umaarufu mkubwa kwa namna wanavyoziunga mkono klabu zao uwanjani na ambao wakati mwingine wapo tayari kufanya jambo lolote.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya mashabiki hao ‘vichaa’ ambao wamekuwa wakinogesha burudani ya soka popote linapochezwa ndani na nje ya nchi;

ALLY YANGA

Klabu ya Yanga ina shabiki mmoja anayeitwa, Ally Ramadhani maarufu kwa jina la Ally Yanga ambaye stali yake kubwa ni kujipaka masizi usoni na kuweka mpira tumboni mfano wa kitambi na wakati mwingine huvaa miwani.

Shabiki huyu ni wale unaoweza kuwaita ‘vichaa’ kutokana na mapenzi yake kwa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani jijini Dar es Salaam na anapoingia huwa anabeba mabango yenye ujumbe tofauti.

Historia ya Ally ambaye ni mzaliwa wa Shinyanga kwa sababu ya mapenzi yake na Yanga amejikuta akitupwa rumande mara kwa mara na yote ni kutokana na ushabiki wake, inaweza kuwa katika mabishano hadi kutupiana ngumi.

Ambapo Ally aliweka wazi mapenzi yake kwa Yanga ni tangu alipokuwa mtoto mdogo licha ya kuwa baba yake mzazi ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa Simba damu.

Mbali na Yanga, Ally ameonyesha mapenzi yake kwa taifa akiishabikia Taifa Stars na kujitolea kusafiri nao katika nchi tofauti wanapokwenda.

MWIGULU NCHEMBA

Kiongozi mwenye wadhifa mkubwa serikalini, Mwigulu Nchemba burudani yake kubwa ipo kwenye soka. Mwigulu ni shabiki kweli wa soka na huwezi kumwambia kitu mbele ya Yanga pamoja na timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Mapenzi ya Mwigulu kwa Yanga amekuwa akijitolea katika mambo mbalimbali mfano ni msimu uliopita baada ya kocha wa klabu hiyo, Mholanzi Hans Pluijm kuvunja mkataba kutokana na ujio wa Mzambia George Lwandamina.

Tukio ambalo lilizua mjadala mbele ya mashabiki wa Yanga wakabaki na sintofahamu, ila yeye anatambua umuhimu wa watu hao, akaweka mambo sawa kwa kumwita, Pluijm ofisini kwake wakazungumza na akarudi kundini kwa kupewa Ukurugenzi wa Ufundi.

Pia ni ngumu kumkosa, Mwigulu ambaye ni Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi na kitambaa chake cha bendera ya taifa shingoni katika jukwaa kuu wakati Yanga inapokuwa uwanjani na ikitoke hayupo lazima atakuwa amebanwa na shughuli nyeti za nchi.

PROF JUMA KAPUYA

Achana na Waziri Nchemba, Profesa Kapuya ni balaa kwa ushabiki wa soka. Ni Simba damu mpaka anakera unaambiwa. Simba iwe inacheza kokote, kigogo huyo wa zamani wa serikali ya Tanzania, hakosekani. Mwingi wa utani na anayeumia haswa moyoni Simba ikipata matokeo mabaya. Wakati fulani akiwa Waziri wa Michezo inadaiwa alifanya maamuzi ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangia kuwakimbiza wadhamini wa Ligi Kuu enzi hizo, baada ya kuzirejesha timu zilizokuwa zimeshuka na kuitia matata TFF (enzi hizo FAT) kwa wadhamini hao....Yote ikielezwa ni unazi wake katika soka.

MAMA YANGA

Ukienda nje ya nchi au Mkoa wowote ambao Yanga wanacheza kamwe huwezi kumkosa shabiki wao maarufu, Mwantumu.

Mwantumu ambaye jina lake maarufu ni Mama Yanga, kimwonekano ana mwili mkubwa na amejazia wenyewe wanapenda kusema mtoto Mashallah kwa sababu ya maumbile yake. Mwanamke huyu, huwezi kumwambia kitu kuhusu klabu yake hiyo ambayo itawakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.

Moja ya matukio aliyokutana nayo ni pamoja na kuzimia wakati klabu yake ikicheza katika vipindi tofauti na hasa inapokutana na Watani wao wa jadi Simba.

Mwantumu ambaye kauli yake kubwa anayopenda kuzungumza anataka kuisaidia Yanga na siyo Yanga imsadie ndiyo maana amekuwa akisafiri nayo na kujigharamia kwa kila kitu mwenyewe akisikia unaikejeli klabu yake, yuko tayari kufanya lolote kama kujibizana maneno na hata kuzipiga.

MBOTO

Msanii wa Bongo Movie anayejulikana kwa jina la Mboto ni shabiki mkubwa wa Yanga ambapo kutokana na mapenzi yake, haishiwi vituko.

Mtaalamu wa kutoa maneno ya utani pindi klabu yake inpofanikiwa na hata kupoteza huwa hajali.

STEVE WA KULIALIA

Shabiki wa soka nchini, Steven Charles maarufu kwa jina la Steve wa Kulialia. Awali alikuwa akiishabikia Yanga, lakini sasa ni Azam damu.

Huyu shabiki ana vituko na hasa hiyo staili yake ya kulia kila timu yake inapopata matokeo mabaya.

Kipigo cha mabao 5-0 cha Yanga mbele ya Simba ndiyo kilimfanya shabiki huyo kuwa maarufu zaidi ndani na nje ya nchi lakini akaja kuzua mjadala mkubwa baada ya kuhamia Azam.

Ambapo Steve aliweka wazi sababu ya kuachana na Yanga ni chuki alizokuwa akifanyiwa na baadhi ya wadau wenzake wa klabu hiyo ya Jangwani pamoja na pesa anazopewa na matajiri hao wa Azam.

AMOS MAKALA

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala mbali na wazifa wake mkubwa ndani ya nchi, huwezi kumwambia kitu mbele ya ushabiki wake kwa klabu ya Simba.

Makala amekuwa akijitolea kwa Simba katika matukio mbalimbali na alishaweka wazi kuwa yuko tayari kukacha kupanda basi la Yanga hata kama atakuwa katika hatari kubwa.

Kiongozi huyo alitoa kituko na kusema, ikitokea amepata matatizo katikati y Mbuga ya Mikumi, akaliona basi la Yanga na mnyama Simba, yuko tayari kukimbilia juu ya mti lakini siyo kupanda usafiri huo wa watani zake wa jadi.

BI HINDU

Kati ya wanawake walio mstari wa mbele kuhakikisha klabu yao ya Simba inafanya vizuri ni mwanamama maarufu nchini, Bi Chuma Suleiman na anatambulika zaidi kwa jina la Bi Hindu.

Bi Hindu ni shabiki na mwanachama mkereketwa wa Simba na kwa kawaida huwa hayuko tayari kuona mambo hayaendi sawa ndani ya timu yake.

KIvutio zaidi kwake ni maneno yake ya shombo bila kujali anayatolea wapi, we muulize Rais wa Simba, Evans Aveva atakufafanulia kwani hivi karibuni wakati vuguvugu la mabadiliko ndani ya Msimbazi, Bi Hindu mbona aliwachana bwana!

DOGO OKWI

Kijana mmoja anayejulikana kwa jina la Okwi mtoto, alifanya maamuzi magumu akiwa na miaka tisa hivi akitoka kwao Kigoma akazamia ndani ya treni na kuja jijini Dar es Salaam lengo ni kumwona aliyekuwa straika wa Simba, Emanuel Okwi raia wa Uganda.

Mbali na kumwona Okwi ni kuishuhudia Simba kwa macho yake na sasa ameshafikisha kama miaka mitano tangu alipochukuliwa na kuhifadhiwa na shabiki mwenzake, amekuwa hakosekani uwanjani pindi Wekundu hao wa Msimbazi wanapokuwa uwanjani sambamba na kufanya vituko tofauti.

MACHO

Ukitaka uishi bila amani basi mchokoze shabiki huyu wa Simba anayejulikana kwa jina la Macho.

Macho ni shabiki wa Simba wenyewe wanapenda kusema ‘Kindakindaki’ anajua mipango yote ‘figisufigisu’ za klabu hiyo na akikutamkia jambo lazima litokee.

Ukitaka kwenda tofauti na ujue jamaa huyu ni mtata, toa maneno ya kuikejeli Simba lazima pachimbike.