Manji na Mo wanatushikiaje akili zetu?

YANGA imetangazwa Bingwa wa Tanzania Bara katika msimu uliomalizika juzi Jumamosi.  Hakuna anayeshangaa Simba na Yanga kuwa ndio habari kubwa wakati huu wa kuhitimisha msimu kwani, imeshazoeleka hivyo.

Ni msimu uliotawaliwa na vituko vingi na kama kawaida karibia vituko vyote vimesababishwa na Simba na Yanga pamoja na baba yao TFF ambalo ni Shirikisho la Soka la Tanzania, lenye thamani ya soka.

Hawa ndio waliolifikisha soka letu hapa lilipo. Tuangalie baadhi ya mapungufu na vituko vilivyojitokeza kwenye msimu huu ulioisha.

UDHAMINI WA SIMBA NA YANGA.

Msimu huu Simba na Yanga wamevunja rekodi kwenye udhamini katika klabu zao. Mwaka jana mashabiki wa timu hizi walikuwa wakiwataja sana Mohamed Dewji na Yusuph Manji. Watu hawa wawili waliteka vyombo vyote vya habari, kutokana na staili za kipekee walizokuja nazo kutaka kuzikodisha na kuzinunua kabisa.

Watu hawa waliwagawanya mashabiki wa timu zao kabisa, Manji alikuja na staili  ya kuikodisha Yanga huku Mohamed Dewji akiweka mzigo wa Sh20 bilioni mezani na kuwafanya mashabiki wa Simba na viongozi wao kuliimba jina lake pale klabuni Msimbazi na hata aliipoonekana Uwanja wa Taifa.

Ni aibu kwa klabu hizi mpaka leo kuendelea kuwa ombaomba wa Manji na Dewji.

Yanga ilianzishwa mwaka 1935 huku Simba ikianzishwa 1936. Kwa umri huo, ni aibu kudhalilishwa na hawa wafanyabiashara.

Manji na Dewji badala ya kuwa wafadhili wa hizi timu, walipaswa kuwa wafanyakazi wa klabu hizi kutokana na ukongwe wake.

Walipaswa kupeleka CV zao pale Yanga au Simba kuomba kazi na si wao kutafutwa kwa ajili ya kutoa ufadhili wa pesa.

Tujiulize Yanga na Simba zina mashabiki kiasi sani? Wanashindwa kutumia mtaji huu wa mashabiki kutengeneza pesa? Jiulize nje ya ufadhili huu wa kina Manji na Dewji pamoja na viingilio, Simba na Yanga zina miradi gani mikubwa ya kuziingizia fedha?

Leo Dewji anataka kuzuia dili la Sports Pesa kisa ana machungu na Simba. Kweli? Kwani akiingiza huo udhamini wake na mambo mengine yakiendelea kwa masilahi ya Simba kuna tatizo gani?

Hata mmiliki wa Chelsea hakatai dili za pesa kama hizi, ndiyo maana kwenye fulana za Chelsea utakuta wakitangaza matairi ya magari. Hapa kwetu hawa kina Manji na Dewji wala sio wamiliki kwa asilimia hata 50 za hizi klabu ila wanataka kuzuia mabilioni ya SportPesa na wadau wengine

KADI ZA OVYO OVYO.

Simba na Yanga zimewaingiza marefa pamoja na TFF majaribuni kama kawaida yao. Pamoja na ubovu wa waamuzi wetu ila mechi za Simba na Yanga ndizo zilizoleta aibu hizi za kadi kwenye ligi.

Obrey Chirwa aliachiliwa huru na Kamati ya Masaa 72 baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano na kuambulia nyekundu dhidi ya Ruvu Shooting. Baada ya muda mfupi tukasikia kamati hiyo imemfutia Obrey Chirwa kadi yake na kumfungia mwamuzi Ahmad Simba kutoka Kagera. Kama kadi ile ingetolewa kwa mchezaji  wa timu nyingine, wala mwamuzi huyu asingelifungiwa. Viongozi wa Yanga walijua kuwa kwa kipindi kile Obrey Chirwa ndiye alikuwa tegemeo kwao wakaamua kulazimisha kadi ile ifutwe na TFF ikakubali.

Kadi ile ingempata mchezaji kama Malimi Busungu wala viongozi wa Yanga wasingeenda kwenye kamati hiyo, wangemwacha tu amalize adhabu yake.

Kichekesho kingine cha kadi ni zile kadi tatu za Fakhi wa Kagera Sugar. Hakuna kumbukumbu zozote TFF zinazoonyesha kama mchezaji yule ana kadi hizo tatu ama la.

Pamoja na Simba kutokufuata utaratibu wa kukata rufaa ila ni jukumu la TFF kujua kama kweli Fakhi alikuwa na kadi tatu ama la! Simba wala walikuwa hawana haja ya kwenda kukata rufaa maana kanuni za Ligi Kuu zipo wazi na kumbukumbu zipo.

Cha ajabu TFF hawana kumbukumbu zozote zile hii ni aibu kubwa. Stori ya kadi hizi tatu imekuwa kubwa kwa sababu ya Simba na Yanga.

Ingekuwa tatizo hili lilijitokeza kwenye mechi ya Ndanda na Mbao wala usingelisikia suala hili. Mbaraka Hussein wa Kagera Sugar kafutiwa kadi yake nyekundu. Kadi hii aliipata kwenye mechi ya Kagera na Yanga.

Mbaraka alitolewa baada ya kuonekana ni tishio kwa ubingwa wa Yanga. Asingelitolewa mambo yangeweza kuwa mengine.

Kelvini Yondani ndiye aliyepaswa kutolewa nje badala ya Mbaraka. Baada ya mechi  kuisha Mbaraka anafutiwa kadi yake hii.

 RATIBA.

Jambo lingine lililopoteza ubora wa ligi yetu msimu huu ni suala la ratiba. Ni jambo la ajabu na ni katika Ligi ya Tanzania tu timu moja inacheza mechi saba kwenye uwanja wake wa nyumbani kabla ya kwenda kucheza ugenini. Simba ilipangiwa kucheza mechi saba Dar kabla ya kwenda mkoani.

Katika hali kama hiyo, mnawezaje kumudu presha za mikoani? Kilichowamaliza Simba msimu huu ni ratiba tu, sio kitu kingine.

USAJILI.

Mpaka leo nasikia Simba wanataka kumsajili tena Emmanuel Okwi. Yaani Okwi kwao ni zaidi ya mchawi, hakuna mtu mwingine yeyote nje na ndani ya nchi anayeaminiwa kuwa anaweza kuziba nafasi yake, kisa tu aliifunga Yanga.

Usajili wa Simba na Yanga haufanywi na benchi la ufundi, ni usajili unaofanywa na viongozi wa timu. Angalia sakata la usajili wa Kessy ulivyokuwa. Angalia suala la Venance Ludovick kutoka Mbao kwenda African Lyon ulivyokuwa. Yote haya yanatokea kwa sababu Yanga na Simba wametumbukiza mikono yao kwenye hizo sajili.

WASEMAJI WA KLABU.

Ukiacha mpira wa uwanjani, nje ya uwanja Simba na Yanga ndio waliokuwa wanasikika zaidi. Hii ni kutokana na wasemaji wao kuwa waongeaji sana, walikuwa ni watu wa propaganda zaidi ya siasa ambapo, wanazungumza mpaka mambo mengine si tu kwamba hayawahusu bali hawayajui kabisa.

Unaona mtu anatokwa na povu jingi lakini hakuna hoja ya msingi inayosikika, unaona kabisa ni mtu aliyemezeshwa kitu na watu fulani akakiteme tu mbele ya umma.

Wasemaji wa Simba na Yanga hawazizungumzii timu zao kitaalamu bali ni kushambuliana wao kwa wao. Wote walifungiwa na hapo kidogo kelele kwenye redio zikaanza kupungua kwani, ilikuwa ni zaidi ya mipasho.