Makinda wa kuwatazama Afcon 2017

Mchezaji Franck Kessie

Muktasari:

Wakati mikikimikiki hiyo ikiwa imevutia mastaa kibao, kuna makinda watano wanatajwa kwamba watakuwa na mvuto na mashabiki wanapaswa kuwatazama wakati wa michuano hiyo ya Afcon 2017.

MICHUANO ya kusaka ubingwa wa Afrika kwa mwaka huu wa 2017 inaendelea huko Gabon, ambapo inashuhudia uwepo wa mastaa kibao wanaocheza soka kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakirudi Afrika kuonyeshana kazi.

Wakati mikikimikiki hiyo ikiwa imevutia mastaa kibao, kuna makinda watano wanatajwa kwamba watakuwa na mvuto na mashabiki wanapaswa kuwatazama wakati wa michuano hiyo ya Afcon 2017.

5. Ebenezer Ofori (Ghana)

Anakamatia namba katika kikosi cha kwanza cha AIK ya huko Sweden, Ofori, kinda mwenye umri wa miaka 21 ameitwa kwa mara ya kwanza kuichezea timu ya taifa ya Black Stars katika michuano hiyo ya Afcon 2017. Akiwa na uwezo wa kucheza beki za pembeni upande wote kushoto na kulia, Ofori ana uwezo mkubwa pia wa kucheza kwenye sehemu ya kiungo ambapo, mwaka 2015 aliikamatia kweli kweli. Ofori ni fundi wa kupiga pasi sahihi na kwa msimu uliopita amepiga pasi sahihi kwa asilimia 88.1 huku akiwa amefunga mabao matatu na asisti nne akiwa kwenye sehemu hiyo ya kiungo.

4. Marvelous Nakamba (Zimbabwe)

Ukiweka kando kuwa na jina lenye mvuto zaidi kwenye michuano hiyo, staa huyo Mzimbabwe Marvelous Nakamba ni moja ya wachezaji wenye vipaji bora kweli kweli. Nakamba anatazamwa kuwa kama moyo wa safu ya kiungo ya Zimbabwe, ambayo juzi Jumapili iliigomea timu matata kabisa Afrika, Algeria na kutoka nao sare ya mabao 2-2. Anacheza soka lake la kulipwa katika klabu ya Vitesse inayoshiriki Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), huku akiwa ndiye mchezaji aliyepiga tackling nyingi msimu uliopita akiwa amefanya hivyo mara 125.

3.Keita Balde (Senegal)

Miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa, Senegal ipo kwenye kundi hilo kutokana na kuwa na kikosi bora kabisa na hili linaweza kuwa taji lao la kwanza la Afcon. Wana kikosi matata chenye Sadio Mane ndani, lakini kinda Keita Balde anatajwa kuwa atakuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho cha Simba wa Teranga.

Kinda huyo wa Lazio ameonyesha kiwango kikubwa kwa msimu huu akiwa amefunga mabao mengi zaidi, mabao matano kuliko alivyofanya hivyo msimu uliopita alipocheza mechi 31.

Umri wake ni miaka 21, lakini ni fundi wa kukokota mpira akiwa mwenye kasi na nguvu inayomfanya awe tishio kwa wapinzani.

2. Jordan Ikoko (DR Congo)

Baada ya kupata pigo la staa wao Yannick Bolasie kuwa majeruhi, DR Congo watakuwa na kazi ngumu kwenye michuano hiyo, lakini wanaamini Jordan Ikoko atakuwa na msaada mkubwa kwao baada ya kumjumuisha kwenye kikosi.

Ikoko alicheza timu za vijana za Ufaransa karibu zote na ameonyesha kiwango bora sana akiwa na klabu yake ya Guingamp, anayofanya maajabu kwenye Ligi Kuu Ufaransa huku Ikoko akisimama imara kabisa katika beki ya kulia na kuwa kisiki kinachofanya timu hiyo isipitike kirahisi.

1. Franck Kessie (Ivory Coast)

Inaaminika kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaosakwa sana na klabu kubwa Ulaya, lakini kwa sasa yupo Gabon. Franck Kessie anawindwa na klabu kibao vigogo barani Ulaya, lakini timu yake ya Atalanta inapambana kwa sababu inataka ada kubwa.

Umri wa mchezaji huyo ni miaka 20 na amekuwa na msimu bora kabisa kwenye Ligi Kuu Italia baada ya kufunga mabao sita. Kwenye kikosi cha Ivory Coast, Kessie anatajwa kuwa ni mrithi wa kiungo Yaya Toure, ambaye amestaafu kuichezea timu ya taifa.