Madhara ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo

Jamie Vardy

Muktasari:

  • Katika nchi za wenzetu jambo hili haliwezi kupita hivi hivi tu, ni lazima watachunguza kupata ukweli wake.

MWAKA jana kule England kuliibuliwa tuhuma katika gazeti la Times zilizodai kwamba Daktari Mark Bonar, anahusika kuwapa wanamichezo kadhaa wakiwamo mastaa wa soka dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku kutumika michezoni.

Ilidaiwa daktari huyo alifanya hivyo kwa wachezaji kadhaa Arsenal, Chelsea na Leicester City. Muda mfupi tu baada ya tuhuma hizo kuibuka, Dk Bonar, alijitokeza na kukana kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Katika nchi za wenzetu jambo hili haliwezi kupita hivi hivi tu, ni lazima watachunguza kupata ukweli wake.

Kwa kawaida tume ya kudhibiti dawa hizi michezoni duniani huwa na utaratibu wa kuwapima wanamichezo kwa kuwashtukiza. Hufanya hivyo kwa wale ambao inawashuku na upimaji huo hufanyika uwanjani mara tu baada ya mshukiwa kumaliza mechi.

Baadhi ya dawa tunazozitumia kwa kunywa au kwa njia ya mshipa,  huweza kuingia katika mzunguko wa damu na kupita katika ini na kuvunjwa vunjwa kabla ya kuanza kazi yake ya kitiba.

Mtu anapotumia dawa hizi huingia katika damu ili kufanya kazi, baada ya dawa kufanya kazi hufika katika figo na kuchujwa na kutolewa kama mashudu/taka sumu za mwili pamoja na mkojo, hii ndio sababu sampuli ya mkojo hutumika katika uchunguzi.

DAWA ZILIZOPIGWA MARUFUKU

Zipo takribani dawa 192 zenye vichochezi maalumu na viambata vingine ambavyo vimepigwa marufuku kutumiwa na wanamichezo duniani. Katazo dhidi ya dawa hizo linatambuliwa pia na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Dawa jamii ya Anabolic Steroids ndio ambazo zimepigwa marufuku pamoja na jamii nyingine nne ambazo zina dawa nyingi na majina tofauti tofauti ya kibiashara toka katika kampuni mbalimbali.

Zipo dawa ambazo zimetengenezwa na wanasayansi kwa lengo la matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwamo kukata maumivu ya mwili na kukata mlipuko wa kinga ya mwili wenye mwitiko hasi.

Dawa hizo zinapatikana kwa mifumo ya vidonge, sindano na hata kwa njia ya kupakaa.

Zipo dawa za Steroids zisizotakiwa kutumiwa na wanamichezo ikiwamo zinazojulikana kitabibu kama Anabolic Steroids ambazo hutumiwa na wanamichezo kunenenepesha na kuipa nguvu ya ziada misuli ya mwili.

Kuna dawa za Steriods ambazo zinatambulika kisheria za michezo ya kimataifa kuwa kiwango kilichomo katika dawa hizo hakiwezi kumwongezea nguvu na kunenepesha misuli endapo mwanamichezo atatumia kama matibabu baada ya ushauri wa daktari.

Steroids hizo zinazotumika katika huduma za afya hutumika kuwatibu waliochelewa kubalehe, matatizo ya homoni, waliopoteza uimara wa misuli yao baada ya kuugua muda mrefu magonjwa ya ngozi.

Kundi la wanamichezo ambao mara kadhaa wamekuwa wakigundulika kutumia Steroids zilizopigwa marufuku michezoni, ni pamoja na wanyanyua vitu vizito, watunisha misuli, wanariadha na wacheza mieleka.

Dawa hizo zilizopigwa marufuku kwa wanamichezo yaani Anabolic Steroids, huifanya misuli kujaa, mifupa kuongezeka uzito, kuongeza nguvu za misuli na kumfanya mchezaji kuwa na kasi zaidi.

SABABU ZA MARUFUKU NI ZIPI?

Ni ukweli usiopingika kuwa dawa hizi hizileti ushindani wa haki michezoni kama wengine watakuwa wanazitumia na wengine hawazitumii. Hii ndiyo sababu zinaitwa dawa haramu.

Madhara makubwa ya kiafya ya dawa hizi ikiwamo athari katika moyo na damu, ni sababu nyingine ya kupigwa marufuku kutumika michezoni.

Steroids zilizopigwa marufuku na viambata vyake zina madhara makubwa kiafya na ya muda mrefu katika mwili. Kadiri mtu unavyotumia kwa wingi, ndivyo madhara yanavyozidi kuongezeka. Ipo jamii nyingine ya Steriods zilizopigwa marufuku ziitwazo Steroid Precursors  ambazo ni Adrostenedione (andro) na Dehydroepiandrosterone (DHEA) ambazo pia huongeza ukubwa na nguvu ya misuli. Baadhi ya athari za dawa hizi zinaweza kudhibitiwa lakini nyingine zikiisha tokea ni vigumu kuzidhibiti.

Wanamichezo vijana walio katika umri wa balehe wakitumia dawa hizi wanapata tatizo la kutoongezeka urefu, kokwa/korodani kunyauka na kuota matiti (kwa wavulana).

Vile vile athari kama hii inapojitokeza huambatana na uharibifu wa maumbile ya kiume, ukosefu wa nguvu za kiume na ugumba.

Kuota matiti kwa mwanamichezo wa kiume huambatana na matatizo ya kisaikolojia kama vile kukosa kujiamini, kujichukia, kujitenga, kuwa na msongo na kupata sonona (hali ya mtu kuwa na huzuni na kupoteza hamu ya kuishi).

Vile vile kuota nywele katika uso na kupata chunusi nzito usoni. Kwa mwanamichezo wa kike madhara anayoyapata ni kuwa na sauti nzito, kukomaa na kukamaa misuli kama mwanaume.

Madhara mengine kijumla ni maumivu sugu ya maungio na kupata majeraha kirahisi ya nyuzi ngumu za miishilio ya misuli inayojipachika katika mfupa (tendon) na kuwa na kinga dhaifu.

Vile vile hupata matatizo ya ugandishaji damu pale unapopata jeraha, shinikizo la juu la damu, matatizo katika ini, hasira zilizopitiliza na kuhisi uzito mwilini unaomfanya mwanamichezo kuwa mvivu.

MAMBO YA KUZINGATIA

Inashauriwa kwa wanamichezo wanaoshiriki michezo ya kimataifa kuwa waangalifu na dawa wanazotumia hasa wanapoandikiwa kutumia dawa fulani na daktari asiye wa michezo.

Vizuri kuwa na mawasiliano ya karibu na daktari wa timu, mjulishe matibabu yoyote unayopewa na madaktari wengine wanaokutibu.

Epuka kutumia virutubisho au vinywaji vya kuongeza nguvu za utendaji (Energy Drinks) vinavyouzwa kiholela mtaani kwani kuna baadhi zina kiwango kisichotakiwa kutumiwa kwa wanamichezo.

Pale unapoumwa na ugonjwa wowote vema kumjulisha daktari anayekutibu akifahamu wewe ni mwanamichezo, hii itamsaidia kuthibitisha kuwa uliandikiwa dawa hizo kwa matibabu tu na si vinginevyo.

Dawa za matibabu za Steroids za hospitalini huwa ni salama na zimepitishwa na mamlaka ya chakula na dawa za ndani na kimataifa.

Hata tume ya kudhibiti matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni duniani inatambua hilo,  hivyo haina tatizo kwa mwanamichezo anayetumia dawa za Steroids kama matibabu ya tatizo la kiafya. Kwa mwanamichezo ni vyema kuzingatia kanuni na kiapo kinachokataza kutumia dawa hizi.

Epuka kutumia dawa za steroids au virutubisho kiholela bila kuandikiwa au kushauriwa na wataalamu wa afya. Ni vyema pia timu zetu zikawa na orodha zilizopigwa marufuku ili kuwaelimisha wachezaji.