Lusaka kulibamba kinoma

Muktasari:

Kwa mujibu wa bango lililokuwa limewekwa kwenye moja ya makutano ya barabara mjini Lusaka, hadi mwaka 2015 idadi ya wakaazi wa jiji hilo walikuwa milioni 2.7. Yawezekana wameongezeka lakini bado ni kama nusu tu ya watu wa Dar.

SIKU nne ndani ya nchi ya watu, lazima kuna vitu vinatakuwa tofauti na mazingira uliyozoea. Mji wa Lusaka ilikofia Yanga, hauna pilika nyingi kama baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam. Hakuna wakaazi wengi pia kama Dar.

Kwa mujibu wa bango lililokuwa limewekwa kwenye moja ya makutano ya barabara mjini Lusaka, hadi mwaka 2015 idadi ya wakaazi wa jiji hilo walikuwa milioni 2.7. Yawezekana wameongezeka lakini bado ni kama nusu tu ya watu wa Dar.

Hii ndiyo sababu maeneo mengi ya mji yana utulivu na hata pilika za biashara siyo nyingi. Kitu kikubwa kilichonivutia mjini Lusaka ni namna Uwanja wao wa Ndege ulivyowekwa mbali na mji ili kuepusha usumbufu kwa wakaazi wake.

Uwanja huo upo umbali kama wa kilometa 10 kutoka mjini na jirani na uwanja huo hakuna makaazi ya watu. Umbali wa kilometa kama tatu kutoka uwanjani ni mashamba ambayo hayaruhusiwi kulimwa pia kwani yametengwa kwaajili ya shughuli maalumu.

Hali hii ni tofauti na uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar ambapo ukitoka tu nje unaanza kukutana na makazi ya watu. Kutokana na udogo wa uwanja wao wa sasa, wamelazimika kuanza ujenzi wa uwanja mpya kama Tanzania ilivyoamua pia kujenga uwanja mpya pembezoni mwa huu wa sasa.

Wenyeji wengi wa Lusaka ni weusi tii kama walivyo Wanyakyusa wa Mbeya na ilinichukua matembezi kadhaa kukutana na wakaazi wenye asili wa weupe kama mimi. Hata hivyo ukarimu wao ni mkubwa na wana mapokezi ya kuvutia.

 

Ugali hatari

Nilichogundua ni kwamba watu wa Zambia wanapenda sana kula ugali kuliko vyakula vingine vyote unavyovifahamu. Yaani wanaweza kuamka na ugali, wakashinda na ugali na kulala na ugali. Kwa namna wanavyopenda chakula hicho unaweza kushawishika kusema kuwa hata mtu akiota usiku kwamba anakula huwa anaota kuwa anakuwa ugali.

Katika Hoteli nyingi mjini Lusaka chakula kikuu ni ugali. Vyakula kama chipsi kuku, chips nyama na vinginevyo vinapatika kwa oda maalum. Watu wengi wa hapo wanasema ugali ndiyo chakula. Wenyewe wanaita mshina. Wanapenda zaidi kula ugali na ndege aina ya kware.

Ajabu ni kwamba hata kina dada wengi mjini hapa hawana ‘shobo’ na chips bali wanapenda zaidi ugali. Kilichonivutia zaidi kwao ni kwamba mwanaume akila ugali kidogo wanamshangaa na kuona ni kama hayuko sawa.

 

Mji umepangika

Pengine kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya watu, maeneo mengi ya mji wao yamepangika. Yapo maeneo mengi ambayo yametengwa kwaajili ya shughuli za kijamii na punde ukitaka kuyatumia kwa matumizi ya kawaida unalipia kiasi kadhaa cha fedha.

Mwenyeji wangu ananieleza kwamba eneo timu ya Zanaco walipojenga uwanja wao wa Sunset wamelikodi kutoka kwa wananchi kwa muda wa miaka arobaini. Muda huo ukimalizika wanalazimika kulipia tena ili kuweza kuendelea kutumia uwanja wao.

Kilichonishangaza zaidi ni kwamba licha ya idadi ndogo ya watu, bado njiani kulikuwa na foleni kubwa. Barabara nyingi za katikati ya mji zinaruhusu magari matatu kwenda na matatu kurudi lakini bado zilizidiwa idadi ya magari. Maeneo mengi ya makutano ya barabara hayajatengenezwa vizuri jambo linalochangia magari mengi kushindwa kutembea kwa kasi inayotakiwa.

 

Uwanja wao matata

Uwanja wa Kumbukumbu ya Mashujaa wa Zambia na ndipo mchezo wa Zanaco na Yanga ulichezwa, umejengwa kisasa na unavutia. Idadi ya mashabiki wanaoketi uwanjani hapo ni ndogo kulinganisha na ile ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam lakini umetengenezwa vizuri.

Majukwaa ya uwanja huo yamepangiliwa kwa ubunifu wa hali ya juu na viti vyake vimepambwa kwa rangi za bluu, njano na kijani. Ukiingia tu uwanjani hapo utajikuta unavutika kuutazama tena na tena.

Katika vyumba vya ndani vya uwanja huo, vipo vyumba vya watu wote muhimu wanaokwenda uwanjani. Vipo vyumba kwaajili ya waamuzi, wanaandishi wa habari, viongozi wa shirikisho na hata vyumba kwaajili ya kupata chakula.

Nyuma ya uwanja huo ndipo yaliyojengwa makaburi ya mastaa wa zamani wa Zambia waliokufa katika ajali ya ndege wakati wakisafiri kwenda kushiriki mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika kwenye mwambao wa Gabon mwaka 1993.

Hata hivyo pamoja na ukubwa wa uwanja huo, Zanaco haikupata mashabiki wengi uwanjani ambao walikwenda kuwapa sapoti. Timu hiyo inayomilikiwa na Benki ya Biashara ya Zambia, inaonekana haina msisimko mkubwa miongoni mwa watu mjini Lusaka tofauti na timu kama Power Dynamo au Nkana Red Devils.

 

Magazeti yao

Katika hali ya kushangaza mjini Lusaka hakuna gazeti hata moja ambalo linachapisha habari za michezo pekee kama ilivyo kwa Mwanaspoti na magazeti mengine nchini. Magazeti mengi mjini hapo yanaandika siasa na michezo inawekwa katika kurasa za nyuma pekee.

Kilichonishangaza zaidi ni kwamba ubora wa magazeti yao pia uko chini. Kuna gazeti moja linaloitwa ‘The Mast’ lina kurasa nane tu. Inashangaza kweli kweli. Magazeti mengine ikiwemo Times of Zambia yameweka mkazo katika siasa.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba uwepo wa timu ya Zesco nje ya mji wa Lusaka nako kumechangia kupooza kwa michezo katika mji wa Lusaka. Baada ya kushangaa mengi nilitulia na kuendelea kufurahia maisha mjini hapo. Kikubwa nilichokipenda kuhusu Zambia ni hali ya ukarimu wa watu wake. Katika maeneo yote tuliyotembea hatukuweza kukutana na watu wenye vurugu kama ilivyo katika baadhi ya mitaa ya jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya Buruguni.