KONA YA MICHARAZO: Leicester City inashangaza, ila Yanga inastaajabisha

Muktasari:

  • Sitaki kuuingilia uongozi wa Yanga, lakini ni lazima mabosi na Wanayanga kwa ujumla wajiulize, kuna haja ya kufanyika mabadiliko ya benchi la ufundi kwa sasa?

ULE mzimu ambao ulioikumba Chelsea katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England (EPL) ikiwa bingwa mtetezi wa taji, ni kama umehamia kwa waliowarithi taji hilo, Leichester City msimu huu.

Katika ligi ya msimu uliopita Chelsea ikiwa na Kocha Jose Mourinho iliyumba kwenye EPL kiasi cha Mreno huyo kuonyeshwa mlango wa kutokea, lakini bado haikusaidia kitu.

Chelsea walilitema taji lao mapema na kumaliza msimu wakiwa katika nafasi ya 10, huku Leicester City ambayo haikuwa ikipewa nafasi ya kufanya vizuri wakitawazwa kuwa mabingwa kwa kishindo na kuandika historia.

Hata hivyo, mpaka sasa ligi hiyo ikiwa imeingia raundi ya nane, watetezi hao, Leicester City wapo nafasi ya 13 wakiwa wamekusanya pointi nane tu katika mechi zake wakishinda mbili na kuambulia sare mbili, huku wakifungwa mechi nne.

Ingawa ni mapema, lakini hata Chelsea msimu uliopita ilikuwa na mwenendo kama huu na kumshangaza kila mtu, japo mashabiki wa klabu hiyo walijipa moyo kwamba, wangekaa sawa na kurejea kwenye nafasi yao ya juu.

Hata hivyo, kilichotokea kila mtu anakijua, timu ilikuwa haivuki kati kwenda juu na haikushangaza sana ikiliacha taji lao ligombewe na Leicester City, Tottenham, Arsenal na Manchester City kabla ya Leicester kuwazidi kete wenzake.

Kwa namna msimu uliopita timu hiyo ilivyokuwa ikicheza uwanjani na kupata matokeo na ukiingalia sasa utapigwa na butwaa tu.

Inashangaza sana, Leicester City haichezi kama ilivyozoeleka na hata wale nyota wake waliotamba msimu uliopita ni kama wamepigwa ganzi. Jamie Vardy yupo yupo tu, licha ya kuongezwa nguvu na Mnigeria Ahmed Musa.

Cha ajabu ni kwamba timu hiyo licha ya kuyumba katika EPL, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Leicester inafanya vizuri mno ikiongoza Kundi G ikishinda mechi zake mbili za awali ikifunga mabao manne bila kuruhusu nyavu zake kuguswa. Inashangaza kidogo, lakini ndivyo ilivyo.

Mtu unaweza kudhani labda Kocha Claudio Ranieri amewekeza nguvu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ili watwae taji hilo, baada ya kuushangaza dunia kwa kunyakua ubingwa wa EPL. Labda? Ngoja tuone itakavyokuwa.

Sasa wakati unaishangaa mambo ya Leicester City na mwenendo wao katika EPL, rejea kwenye soka la Tanzania, ambayo inazidi kunoga, huku Mnyama akionyesha dhamira yake ya kufuta ukame wa mataji Msimbazi msimu huu.

Simba imekuwa ikigawa dozi kadiri inavyojisikia na unaweza kusema imekusanya, inakusanya na itakusanya pointi sana tu ili kubeba ubingwa msimu huu.

Achana na Simba iliyoonekana kuzinduka, wapinzani wao wakuu Azam na Yanga hawana mwenendo mbaya mpaka sasa, lakini tayari minong’ono imeanza juu kuhusiana na mustakabali wa makocha wake.

Achana na Zeben Hernandez wa Azam, ambaye amewaduwaza wengi kwa kuiongoza timu yake katika mechi nne bila kupata ushindi, japo mabosi wake wamemtetea wakisisitiza kuwa wanamuamini na wataendelea naye. Upande wa watetezi wa Yanga, kuna fununu na dalili za wazi kuwa Kocha Hans Pluijm hana maisha marefu Jangwani, ingawa mabosi wake wanamla kisogo kwa kukanusha taarifa za kumleta kocha mpya kutoka Zambia.

Mzambia huyo, George Lwandamina amekuwa akinukuliwa kuwa ameanza mazungumzo na watu wa Yanga ili aje kuinoa timu hiyo ikiwa ni wiki chache tangu aipe mafanikio Zesco ya Zambia kufika nusu fainali za Afrika.

Hapa ndipo panapostaajabisha, inakuwaje viongozi wa Yanga wanafanya mazungumzo na kocha mwingine wakati Pluijm anaendelea na majukumu yake na akiwa hajafanya vibaya sana mpaka sasa katika Ligi Kuu.

Inastaajabisha kwa vile, Pluijm ni mmoja kati ya makocha walioifanya Yanga kuwa ilivyo, ikizitetemesha timu pinzani za ndani na nje ya nchi. Waarabu wametunguliwa na Yanga baada ya utumwa wa miaka zaidi ya 30. Alianza Al Ahly ya Misri mwaka juzi ikafuata Mo Bejaia ya Algeria, achana na mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu Bara na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga ilitinga hatua hiyo mwaka huu ikiwa ni karibu miaka 20 tangu ilipofuzu mara ya kwanza 1998.

Sitaki kuuingilia uongozi wa Yanga, lakini ni lazima mabosi na Wanayanga kwa ujumla wajiulize, kuna haja ya kufanyika mabadiliko ya benchi la ufundi kwa sasa? Mbona Yanga haijafanya vibaya kivile, kiasi cha kutaka kumfurusha Mholanzi huyo. Hofu yangu Yanga isije ikaafanya maamuzi ambayo baadaye yatakuja kuyajutia kwani,  ikumbukwe kuwa wachezaji wa timu hiyo hawajapata mapumziko kuifanya miili yao iweze kuhimili ngwe nyingine mpya. Hata wachezaji wenyewe wanakiri kuwa wamechoka kutokana na kucheza mfululizo ndani na kimataifa, sasa hilo nalo linataka kugeuzwa kuwa ni udhaifu wa kocha?. Nani anayejua Lwandamina atakuja na mfumo gani ndani ya Yanga na itachukua muda gani kuwafanya wachezaji wamudu na kuanza kuleta matokeo bora uwanjani?.

Hii ni kama bahati nasibu ambayo Azam kila mara imekuwa ikifanya kwa kumtema Kocha Stewart Hall na kumrejesha. Ni mtazamo na ushauri tu, wala Wanayanga msichukie!