Kumbe Ajib na Mavugo wana siri nzito

HUTAKOSEA ukisema msimu huu Simba imesajili timu ya kazi baada ya kushusha mastaa wengi ambao wanakuja kuleta mabadiliko kwa kuhakikisha mataji yaliyokauka kwa takribani miaka minne yanarejea.

Zungumza unavyotaka usajili wote uliofanyika jina kubwa kwao ni mtu mmoja aliyekuja kufunga akitoka Burundi, Laudit Mavugo ambaye baada ya usajili wake kuvuma kwa miaka sasa ametua na tayari katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara ameshaweka alama akiwa na bao moja.

Ujio wa Mavugo unalilazimu Mwanaspoti kumtafuta na kuzungumza naye juu ya maisha yake ya soka kuanzia alipotoka Burundi na hata hapa Tanzania ambapo ameshacheza dakika 180 akianza kueleza alivyoiona timu yake hiyo.

“Tangu nimefika hapa nimegundua Simba ni timu nzuri, timu ambayo ina mashabiki wengi hata mimi nimefurahia kuja kucheza Simba,malengo yangu hapa ni kufanya kazi vizuri na kuiwezesha Simba kufikia nafasi ambayo wanaitaka,”anasema Mavugo.

“Sisi washambuliaji wa Simba kwa sasa bado hatujajenga kitu kimoja wengi ni wapya kwenye timu tutakapocheza mechi zaidi tutaweza kuelewana kimchezo na hapo ndipo mafanikio ya timu yatakuja.

“Haikuwa rahisi kabisa kuja Tanzania, unajua Vital’O ilikuwa imenibana kidogo, niliongea kwa kirefu na viongozi wa timu niliwaambia kwamba ninayetakiwa kuamua nikacheze wapi ni mimi ndiyo wakakubali nafurahi kuona sasa nipo Simba.

“Vital’O nimewafanyia kazi nzuri nimekuwa pale kwa miaka miwili na nikawafungia mabao 30 katika msimu wangu wa kwanza lakini msimu wa pili nilifanikiwa kufunga mabao 32 sasa kwa kazi hiyo timu haikuwa rahisi kwao kuniachia niondoke harakaharaka.”

Nani alimuona na kumleta Simba?

“Unajua kuja hapa Tanzania aliyelitambulisha jina langu ni kocha mmoja raia wa Serbia anaitwa Goran (Kopunovic), niliwahi kufanya naye kazi Polisi ya Rwanda alinipigia na kuniambia ameutaka uongozi wa Simba unisajili wakati huo akiwa hapa Simba, alinitaka nije hapa niungane na Ajib (Ibrahim) akitaka kututengeneza ili tucheze kwa pamoja.

Je, ulirudisha fedha ya Simba ulipokwama?

“Ukweli sikurudisha fedha na hapa ndipo ninaposema naipenda Simba kwa ajili ilinivumilia sana, unajua nilishasaini Simba muda mrefu lakini wakati huo bado nilikuwa na mkataba na Vital’O na picha Simba walikuwa nazo wakati nasaini lakini Simba walivumilia hawakunidai fedha zao wangeamua wangeweza hata kunishtaki na nikafungiwa ndiyo maana sasa walipokuja tena nilikuja kirahisi, sasa nataka kuwalipa fadhila kwa kuwafanyia kazi.

“Unajua mimi ni mchezaji mpya hapa Tanzania nitajaribu kuboresha  kiwango changu niweze kufikia malengo yangu lakini sitaweza kusema nitafunga mabao mangapi lakini nitapambana katika kila mchezo

“Kitu kinachohitajika  hapa ni kushirikiana na wenzangu wajue staili yangu ya uchezaji na mipira gani ya kunipa ili nifunge. Unajua mfungaji mzuri ni yule anayejua akae sehemu gani ndani ya eneo la hatari la wapinzani lakini pia wanaompa mipira ili afunge pia wanatakiwa kujua ni wakati gani wa kumpa mipira hiyo.”

Tofauti

“Unajua Tanzania na Burundi kimpira, Tanzania imeendelea hata wachezaji pia, Burundi kwa sasa wachezaji sio wakongwe ni vijana wadogo, kwasasa wanafunzwa mpira katika vituo mbalimbali vya soka ili wafike juu, hapa kuna wachezaji wengi wazoefu wanajua kitu wanachotafuta.

“Ukija kwa jinsi wanavyocheza kule Burundi wachezaji wengi hasa mabeki wanatumia sana akili lakini hapa tofauti wanatumia sana nguvu na akili kidogo, nimeiona hiyo changamoto unajua nguvu inatafutwa nitafanya mazoezi ya nguvu ili niweze kujiimarisha na kuweza kupambana nao vinginevyo nitakuwa katika wakati mgumu.

Uhusiano wake na Tambwe ukoje?

“Mimi na Tambwe (Amissi) ni kama ndugu, muda mwingi tunawasiliana na kuongea mambo mengi, mimi kitu kinanikera ni kuona katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini (sio kampuni ya Mwananchi) wakisema Tambwe amesema hivi, nikimuuliza anasema hajasema hivyo, ni maneno ya vyombo vya habari sipendi kuona watu waharibu ukaribu wangu na Tambwe.

“Unajua kabla ya kuja hapa Simba nilipata ofa nyingi za timu mbalimbali moja wapo ni Gor Mahia ya Kenya,na hawa walifika mbali kiasi cha kutaka hata kurudisha fedha za Simba lakini kuna mambo yalikwama na sikutaka kwenda Kenya.

Ni kama walinidharau kitu ambacho sikukipenda, sawa walikubali kurudisha fedha za Simba baada ya hapo watamchukua mshambuliaji mmoja katika timu yao kumpeleka Vital’O katika uhamisho huo lakini mimi nakwenda kwao bila ya kupata fedha nikaona hapana hiyo ni sawa na dharau.

Ufaransa?

“Ni kweli nilienda huko lakini kuna mambo yalitokea hatukuelewana na meneja wangu, kuna mambo alinificha, nilipofika ile timu ya daraja la pili ilinijaribu kisha ikaniambia wanataka nikajiunge na timu ya watoto wanaokuzwa (Academy) sasa hilo sikukubaliana nalo niliwaambia mimi ni mtu mzima nitaileaje familia yangu bila kupata kitu nikaamua kurudi.”

Ameonaje Yanga?

“Yanga ni timu nzuri hapa Tanzania nimeona mechi yao moja wakicheza hapa,wanacheza kutafuta pointi tatu hawachezi kufurahisha mashabiki hapana,wana wachezaji wengi wazoefu wanaonyesha wamekaa pamoja kwa muda mrefu lakini staili yao ni kama yetu Simba, pia tunacheza kwa kutafuta pointi tatu pia na mpira wa kuvutia.

“Nimewaona mabeki wao ni wazuri najua siku hiyo itakuwa mechi kubwa hapa Tanzania lakini ngoja tuone itakujae siku hiyo lakini Simba watulie tutapambana.  Najua hiyo mechi inasubiriwa na mashabiki wengi lakini siwezi kuogopa hii ni kazi yangu, watu wanachotakiwa kuelewa kwamba tunacheza mchezo ambao una matokeo matatu, kufungwa, kushinda na hata kutoa sare kitakachotokea hapo kinatakiwa kupokelewe siwezi kushangaa, nikimaliza mchezo huo ninaweza kufunga au nikashindwa haya yote yanatokea asiyekubali matokeo sio mshindani.”

Omog amempa masharti gani

“Nilipokutana na kocha ameniambia amekubali kiwango changu lakini ameniambia natakiwa kucheza kwa ushirikiano na wenzangu, tuweze kucheza kama timu ili Simba ipate mafanikio.  “Nikiamka asubuhi napenda kupata chai labda na mkate, mchana napenda kupata ugali wa mahindi na nyama lakini usiku napata chakula kidogo siku imepita. Nje ya mambo ya soka napenda kutumia muda mwingi kupumzika sana na kuangalia filamu mbalimbali, kuogelea ndiyo mchezo ninaoupenda lakini nikimaliza soka napenda kufanya biashara mbalimbali nitachagua wakati huo ukifika.”